Hili la mpira rasmi wa Ligi, tunaipongeza TFF
Muktasari:
- Hili ni jambo kubwa na la kihistoria kwa Tanzania kuwa na mpira maalumu ambao utatumika katika michezo ya ligi msimu huu.
Shirikisho la Soka nchini (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu Bara, zimeandika historia mpya katika maendeleo ya soka nchini kwa kuzindua rasmi mpira maalumu utakatumika katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2025/26.
Hili ni jambo kubwa na la kihistoria kwa Tanzania kuwa na mpira maalumu ambao utatumika katika michezo ya ligi msimu huu.
Hatua hii ni ya kupongezwa kwa nguvu zote kwani inaonyesha dhamira ya dhati ya TFF kuinua viwango vya soka kitaaluma na kimataifa.
Mpira huu maalumu unaifanya Ligi Kuu kuwa na utambulisho wake kama zilivyo ligi kubwa duniani kama English Premier League (EPL), La Liga, Serie A na Bundesliga, ambazo zote hutumia mipira maalumu iliyoundwa kwa ubora wa hali ya juu.
Tunaamini TFF na bodi ya ligi zitaendelea na juhudi hizi katika maeneo mengine ya maendeleo ya soka ili kuongeza mvuto katika soka la Tanzania na hasa kuitangaza ligi kuu zaidi.
Katika dunia ya sasa ya soka, kila kitu kinafungamana na ubunifu na teknolojia na hata m na hata mpira wa kisasa unahitaji kuwa na ubora unaokubalika na FIFA na CAF, na uwe na uwezo wa kudumu, kuwa na uthabiti wa kuruka, urahisi wa kudhibiti, pamoja na uwezo wa kustahimili hali tofauti za hewa.
Iwapo mpira uliotangazwa na TFF umekidhi vigezo hivi, basi ni wazi Tanzania ipo kwenye njia sahihi ya kufikia ubora wa Afrika na hata kimataifa.
Kwa mujibu wa Makamu wa Kwanza wa rais TFF, Athuman Nyamlani wakati wa hafla ya uzinduzi huo, alisema mpira huo ni wenye ubora ambao umekidhi viwango vinavyohitajika na umezingatia uhalisia wa viwanja vyetu.
Mipira hiyo itagawanywa kwa timu shiriki za Ligi Kuu Bara na ligi nyingine na hivyo kuachana na kutumia mipira tofautitofauti katika mashindano yanayosimamiwa na shirikisho hilo.
Ni jambo la kutia moyo kuona kama mipira hii maalumu haitatumika tu Ligi Kuu ya wanaume, bali pia Championship, First League na Ligi Kuu ya Wanawake ili kuhakikisha mfumo mzima wa soka nchini unakuwa wa kisasa na unaoendana na viwango vya kimataifa.
Katika miaka ya hivi karibuni, TFF imekuwa mstari wa mbele kuendeleza soka linakua kwa kazi na hatua hii itayafanya mashindano inayoandaa kuwa na ushindani zaidi na kuzidi kukua.
Moja ya faida kubwa ya kuwa na mpira maalumu ni kuimarika kwa ubora wa mchezo. Wachezaji wanapozoea aina moja ya mpira, inawasaidia kucheza vizuri na makocha nao hupata nafasi ya kuboresha mbinu zao.
Mbali na hilo, pia inaongeza thamani ya biashara na haki za matangazo. Watangazaji, wadhamini na wawekezaji huvutiwa zaidi na ligi ambayo ina bidhaa maalumu na zenye alama ya kipekee.
Kwa mfano, uwepo wa nembo ya TFF, Bodi ya Ligi na wadhamini wakuu kwenye mpira hutengeneza taswira nzuri ya kibiashara.
Tunaamini baada ya kuandika historia hii, itakuwa endelevu na kila msimu kutakuwa na mpira maalumu na ikiwezekana katika mpira kuwe na maneno yanayoonyesha ni msimu gani ili kuweka kumbukumbu sawa baada ya misimu kupita.
Tunaipongeza TFF na kuihimiza iendelee na juhudi hizi katika maeneo mengine pia ikiwemo viwanja, marefa, benchi za ufundi na maendeleo ya vijana.