Diego Costa ambwatukia mwandishi wa habari
Kazan, Russia. Straika wa Atletico Madrid na timu ya taifa ya Hispania, Diego Costa alighadhibika kutokana na maswali ya mwandishi mmoja wa habari, baada ya kumalizika kwa mchezo wa kundi B, kati ya Hispania na Iran, ambapo straika huyo alifunga bao pekee na ushindi na kushuhudia Hispania ikiipiga Iran 1-0.
Costa ambaye hivi sasa ana mabao matatu, bao moja nyuma ya Cristiano Ronaldo, alishindwa kuzuia hisia zake baada ya mwandishi huyo kudai kwamba, straika huyo wa zamani wa Chelsea alikuwa anatisha wapinzani wake katika mchezo huo. Costa hakumchelewesha: "Kwani wewe uliangalia mechi gani? Kama ni kuhusu kipindi cha kwanza nadhani unahitaji kurudia kuangalia mechi tena, maana hao unaosema nilikuwa nawatisha, walianza kutuchokoza, muda wote walikuwa wanatukanyaga, tulikuwa tunachezewa rafu kila mara."
Hispania itaingia dimbani Juni 25, kumalizia ratiba ya makundi dhidi ya Morocco inayonolewa na Herve Renard. Morocco tayari imeshayaaga mashindano huku Hispania wakiwa wameshafuzu kuingia hatua inayofuata katika kampeni ya kusaka ubingwa wa Kombe la Dunia na kurudia mafanikio waliyopata kwenye michuano ya 2010, nchini Afrika Kusini.