Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zungu: Kipa anayefuata nyayo za Diarra

ZUNGU Pict

Muktasari:

  • Mtindo wake wa uchezaji unafanana kwa kiasi kikubwa na ule wa kipa wa Yanga, Djigui Diarra raia wa Mali, jambo linalomfanya amfuatilie kwa karibu ili kujifunza na kufikia kiwango chake.

KIPA mwenye matumizi mazuri ya miguu “footwork”, huwa na nafasi kubwa ya kufanya uamuzi wa haraka kuokoa mipira na kuanzisha mashambulizi bila kupoteza utulivu na uwiano wa mwili.

Hiyo ndiyo aina ya uchezaji inayomtofautisha kipa wa KVZ, Idrissa Mguya ‘Zungu’, na makipa wengine wanaoshiriki Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) msimu huu 2026-2027, huku akiamini kuwa si wengi wenye uwezo wa kucheza kwa mtindo huo.

Zungu anasema ana mambo matatu anayoyapa kipaumbele katika nafasi yake ambayo ni kujiamini, utulivu na kufanya uamuzi wa haraka ili kuisaidia timu kupata matokeo mazuri. Hata hivyo, anadai kuwa hajapata nafasi ya kutosha kuonyesha uwezo wake kutokana na kutoaminiwa zaidi na baadhi ya watu.

Mtindo wake wa uchezaji unafanana kwa kiasi kikubwa na ule wa kipa wa Yanga, Djigui Diarra raia wa Mali, jambo linalomfanya amfuatilie kwa karibu ili kujifunza na kufikia kiwango chake.

Zungu ana uwezo wa kuzuia mashambulizi kwa kutumia miguu, hujiamini akiwa langoni na hupendelea kuanzisha mashambulizi kutoka nyuma.

Anasema hutumia muda mwingi kumfuatilia Diarra kwa sababu wanafanana katika namna ya kucheza, hivyo amekuwa akijifunza mambo mengi kupitia kipa huyo.

“Mtindo wangu wa uchezaji ni moja ya vitu vinavyonitofautisha na makipa wengine wa Ligi Kuu Zanzibar. Ninaamini kuna wengi wanaonitazama na kunichukulia kama mfano wa kuigwa,” anasema Zungu.

Kwa upande mwingine, anasema soka kwake ni zaidi ya burudani, kwani ni njia ya kubadili maisha yake, kusaidia familia na kupata fursa ambazo huenda mazingira au elimu yasingeweza kumpatia.

Nyuma ya kipaji chake kuna safari yenye changamoto na mabadiliko ya nafasi uwanjani. Zungu anasema awali alikuwa akicheza nafasi ya beki wa kati na hakuwahi kufikiria kuwa siku moja angekuwa kipa.

Hata hivyo, watu wa mtaa anaotoka waliona uwezo wake na kumshawishi kuwa angefanya vizuri zaidi akiwa langoni kuliko kucheza nafasi ya beki wa kati. Ushauri wao ulimpa msukumo wa kuichukua nafasi hiyo kwa uzito na kuanza kufanyia kazi uwezo wake.

“Watu wa mtaani kwetu ndio walionipa hamasa kubwa. Wao waliamini kile ambacho mimi mwenyewe sikuwa nakiamini. Walifanya kazi kubwa kunishawishi kuwa ninaweza kucheza nafasi ya kipa,” anasema.

Anaeleza kuwa baada ya kuamua kuichukulia nafasi hiyo kwa uzito, alianza kugundua uwezo wake na kuongeza juhudi katika mazoezi ili kujiimarisha zaidi.


ZUNG 01

CHANGAMOTO

Kabla ya kujiunga na KVZ, Zungu aliwahi kuzitumikia timu kadhaa za Zanzibar, zikiwemo Malindi na Fufuni. Pia aliwahi kucheza katika kikosi cha Simba cha vijana wenye umri chini ya miaka 20, ambako alikumbana na changamoto ya kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Licha ya changamoto hiyo, hakukata tamaa. Anasema mtindo wake wa uchezaji umekuwa ukifanya baadhi ya watu kuwa na wasiwasi kuhusu uwezo wake, hasa kutokana na namna anavyojiamini na kujitoa katika maeneo hatari ambayo makipa wengi huenda wasithubutu kufika.

Anaeleza kuwa kuna mambo ambayo watu wengine huyachukulia kuwa hatari, lakini kwake ni sehemu ya namna anavyoamini anaweza kuucheza mpira na kuisaidia timu.

Zungu anasema hali hiyo ilichangia kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara alipokuwa Simba, kwani kocha aliyekuwepo alikuwa na wasiwasi kuhusu namna alivyokuwa akicheza. Hata hivyo, anasisitiza kuwa alipopata nafasi ya kucheza, hakuwahi kuigharimu timu.

“Aliyekuwa Kocha wa Simba U-20, Nicholas Nyagawa alikuwa akiniambia ‘Zungu, ukicheza mimi ndiye ninayepata wasiwasi sana. Unaweza kurudishiwa mpira huku mchezaji wa timu pinzani akikufuata kwa kasi, lakini wewe huna haraka. Unaniogopesha sana,’” anasema.


ZUNG 02

MAISHA NDANI YA FUFUNI

Zungu alijiunga na KVZ katika dirisha dogo la usajili la msimu wa 2025-2026 akitokea Fufuni, timu anayoitaja kuwa ndiyo iliyompa nafasi kubwa ya kuonyesha kipaji chake na kumsaidia kung’ara, licha ya changamoto za kiuchumi zilizokuwa zikiikabili.

Anasema Fufuni ilimpa mazingira mazuri ya kucheza kwa amani na kujiamini, akieleza kuwa viongozi na wenzake walimheshimu na kumpa uhuru wa kutumia uwezo wake uwanjani.

Kwa mujibu wa Zungu, kuondoka kwake Fufuni hakukutokana na kutoridhishwa na mazingira ya timu hiyo, bali maslahi madogo yaliyohusiana na uchanga wake katika ligi hiyo, kwani ulikuwa msimu wake wa kwanza kushiriki Ligi Kuu Zanzibar.

Anasema hakuna timu aliyowahi kuitumikia iliyompa amani na kujiamini kama Fufuni, ambako alihisi ana uhuru wa kucheza kwa mtindo anaouamini.

“Hakuna timu ambayo nimecheza nikiwa na amani na kujiamini kama Fufuni, kwa sababu walinipa uhuru wa kufanya kile nilichohisi ni sahihi uwanjani,” anasema.


ZUNG 03

UHAKIKA WA NAMBA

Licha ya kupata mazingira aliyoyapenda Fufuni, Zungu anasema alikuwa na uhakika mkubwa zaidi wa kucheza katika kikosi cha kwanza akiwa huko kuliko ilivyo sasa KVZ.

Tangu ajiunge na KVZ, amecheza mechi moja pekee kati ya saba ambazo timu hiyo imecheza katika ZPL msimu huu. Mechi hiyo ni dhidi ya JKU, iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Anasema ushindani ndani ya kikosi cha KVZ unaweza kuwa sababu ya kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara, kutokana na uwepo wa makipa wenye uzoefu mkubwa katika ligi hiyo.

Hata hivyo, Zungu anakiri kuwa hapendezwi na hali ya kukaa benchi kwa muda mrefu, akiamini inaweza kuathiri kiwango chake. Anatamani kocha amuamini na kumpa nafasi ya kuonyesha uwezo wake.


ZUNG 04

KOSA LILILOIGHARIMU TIMU

Katika safari yake ya soka, Zungu anakumbuka kosa moja alilofanya katika mchezo wa Fufuni dhidi ya Mwenge, uliochezwa kisiwani Pemba, ambalo liliigharimu timu yake.

Anaeleza kuwa alirudishiwa mpira na beki wake, lakini kutokana na kujiamini kupita kiasi, alichelewa kuchukua hatua kabla ya mchezaji wa timu pinzani kuufikia na kuupiga hadi wavuni.

Anasema tukio hilo lilimfundisha umuhimu wa kuwa makini zaidi katika kila hatua, akitambua kuwa soka ni mchezo wenye makosa ambayo yanaweza kubadili matokeo wakati wowote.

Pamoja na kosa hilo, anasema hakukata tamaa wala kujilaumu kupita kiasi, bali alilichukulia kama somo na kufanya marekebisho ili kuepuka kurudia makosa kama hayo.


ZUNG 05

KINACHOMTESA AKIFUNGWA

Zungu anasema kila anapofungwa hujitahidi kupata muda wa kutulia na kuchambua namna bao lilivyofungwa ili kubaini sehemu alizokosea na kufanya marekebisho kabla ya mechi inayofuata.

Anasema utaratibu huo humsaidia kujijenga upya kisaikolojia na kuhakikisha kuwa tukio la kufungwa halimuathiri katika michezo inayofuata.

Hata hivyo, anakabiliwa na ushindani mkubwa wa kuwania nafasi ya kwanza ndani ya kikosi cha KVZ, ambacho pia kina kipa Hamad Ubwa ‘Baro’, anayeelezwa kuwa miongoni mwa makipa wanaofanya vizuri msimu wa 2025-2026 akiwa amecheza michezo mitano bila kuruhusu bao (clean sheets).

Mbali na uwezo wake wa kuokoa mipira, Zungu anasema anapenda kuanzisha mashambulizi kutoka nyuma kwa lengo la kuipa timu utulivu na kuisaidia kushambulia kwa kasi.


MALENGO

Lengo kubwa la Zungu ni kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara, akisema anavutiwa na ushindani mkubwa wa ligi hiyo na presha inayowalazimisha wachezaji kujiandaa na kuwa bora wakati wote.

Anasema kutimiza ndoto hiyo kutakuwa mafanikio kwake binafsi, lakini pia kutawapa furaha na fahari watu wa mtaa anaotoka, ambao anawatambua kuwa miongoni mwa waliochangia safari yake ya kuwa mchezaji wa soka.