Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

WAKALI WAO; Kumi bora kuwahi kutokea Afcon

WAKALI Pict

Muktasari:

  • Michuano hiyo inashirikisha timu za taifa za nchi 24 ikiwamo Tanzania itafanyika kwenye viwanja tisa tofauti vilivyopo katika miji sita kuanzia Desemba 21 hadi Januari 18 mwakani.

IMEBAKI kama wiki tu kabla ya kuanza kwa fainali za 35 za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 zinazofanyikia Morocco.

Michuano hiyo inashirikisha timu za taifa za nchi 24 ikiwamo Tanzania itafanyika kwenye viwanja tisa tofauti vilivyopo katika miji sita kuanzia Desemba 21 hadi Januari 18 mwakani.

Kwa miaka mingi, nyota wengi wakubwa wamezipamba fainali hizo za Afcon kwa uwapo wao, kitu kinachotarajiwa hata msimu huu mambo yawe bam-bam kule Morocco, kwani kuna majina makubwa kama ya Mohamed Salah, Sadio Mane, Mbwana Samatta, Victor Osimhen na Bryan Mbeumo na wengineo watakaokuwa na matumaini ya kufuata nyayo za waliotangulia na kujijengea hadhi ya mashujaa wa kitaifa katika michuano hii.

Hapa chini Mwanaspoti linakuletea orodha ya nyota 10-Bora zaidi kuwahi kucheza fainali za Afcon:


10. ANDRE AYEW

Dede wa Ghana, hakuwahi kunyanyua taji baada ya kufika fainali mara mbili na kupoteza, lakini kiungo huyo wa zamani wa Marseille na Swansea City ni kati ya wachezaji waliowahi kung’ara katika fainali za Afcon, akijitolea kwa hali na mali kwa timu ya taifa ya Ghana, Black Stars.

Amecheza AFCON nyingi zaidi ya mchezaji mwingine yeyote (mara 8), pia anashikilia rekodi ya pamoja ya mechi nyingi zaidi (36). Zaidi ya hayo, alichaguliwa kwenye Kikosi Bora cha Michuano mwaka 2015 baada ya kumaliza akiwa mfungaji bora.


9. LAURENT POKOU

Pokou alitikisa AFCON katika miaka ya 1970, akiifungia Ivory Coast mabao 14 na kuwa mfungaji bora wa muda wote wa michuano hiyo, rekodi aliyodumisha kwa miongo kadhaa.

Yuko chini kidogo katika orodha hii kwa sababu alishiriki matoleo matatu tu ya AFCON na hakuwahi kushinda taji, lakini bado ni gwiji wa kweli. Hili linathibitishwa na ukweli kwamba mpira wa fainali zilizopita ulipewa jina lake.

WAKA 04

8. JAY-JAY OKOCHA

Utasema nini kuhusu winga huyo wa zamani wa kimataifa wa Nigeria. Anajulikana zaidi kwa kuwavutia mashabiki barani Ulaya alipochezea PSG na Bolton, lakini Okocha pia alikuwa bora sana barani Afrika.

Alishinda AFCON mara ya kwanza kabisa mwaka 1994 akiwa na Super Eagles. Hata hivyo, kiwango chake bora zaidi kilikuja baadaye, alipokuwa Mchezaji Bora wa fainali za Afcon za mwaka 2004 baada ya kuiongoza Nigeria kufika nusu fainali, pia aliingia katika Kikosi Bora cha michuano hiyo 2000 na 2002.

WAKA 06

7. ROGER MILLA

Mkongwe huyo wa zamani wa Cameroon, wala hahitaji utambulisho. Ingawa nyakati zake maarufu zaidi zilikuja katika Kombe la Dunia, pia aliacha alama kubwa AFCON.

Katika matoleo matano aliyoshiriki, mshambuliaji huyo wa Cameroon alishinda mataji mawili (1984 na 1988), na alikuwa Mchezaji Bora wa Michuano mwaka 1988 pamoja na 1986.

WAKA 05

6. ABEDI PELE

Ayew wa pili kwenye orodha hii, huyu ni baba wa Andre. Abedi Pele alipata jina hilo mapema kutokana na kipaji chake kikubwa cha soka, na mara nyingi aliishi kulingana na jina hilo AFCON.

Baada ya kuchangia ushindi wa Ghana mwaka 1982, alikuwa nyota wa mashindano mwaka 1992, akifunga katika raundi tatu mfululizo na kuiongoza Ghana hadi fainali. Hata hivyo, alikosa fainali kwa kusimamishwa baada ya kupata kadi ya njano katika nusu fainali, na Ghana ikapoteza bila yeye.

Baada ya kuchaguliwa Mchezaji Bora wa Michuano, aliendelea kuingia katika vikosi bora vya Michuano vya 1994 na 1996 na kujithibitisha kama gwiji wa kweli wa AFCON.

WAKA 07

5. RASHID YEKINI

Kuanzia Osimhen hadi Yakubu Aiyegbeni hadi Obafemi Martins, Nigeria imekuwa na washambuliaji wengi wakubwa, lakini hakuna aliyefikia kiwango cha Yekini, mfungaji bora wa muda wote wa taifa hilo.

Mabao 13 kati ya 37 aliyofunga kwa Super Eagles yalifungwa Afcon. Mshambuliaji huyo aliyefahamika kama Baba wa Mabao aliiongoza Nigeria kushinda taji mwaka 1994 na kufika fainali nyingine tatu katika enzi ya dhahabu ya miaka ya 1980 na 1990.

Alikuwa mfungaji bora mara mbili na anahesabiwa miongoni mwa washambuliaji wakubwa zaidi kuwahi kushiriki AFCON.


4. ESSAM EL HADARY

Hakuna mchezaji aliyezoea mafanikio ya AFCON kama El Hadary. Kipa huyo wa Misri ana rekodi ya kipekee kabisa.

Ameshinda taji mara nne (rekodi ya pamoja). Ingawa hakupata dakika za kucheza mwaka 1998, alikuwa mhimili mkubwa Misri ilipotwaa mataji matatu mfululizo kuanzia 2006 hadi 2010, akichaguliwa kuwa Kipa Bora wa Michuano kila mara.

Zaidi ya hayo, mwaka 2017 akiwa na umri wa miaka 44, alikuwa mchezaji mzee zaidi kuwahi kucheza AFCON na akaisaidia Misri kufika fainali baada ya kuokoa penalti dhidi ya Burkina Faso nusu fainali.

WAKA 03

3. SAMUEL ETO’O

Kama hukujua tangu mwanzo wa karne hii, basi fahamu sasa: Samuel Eto’o alikuwa mchezaji wa kiwango cha juu sana.

Yeye ndiye mfungaji bora wa muda wote wa AFCON, akiwa na mabao 18 katika mechi 29 katika matoleo sita. Alishinda mataji mawili (2000 na 2002) akiwa na Cameroon.

Mwaka 2000 ulikuwa bora zaidi kwake, alipofunga kwenye robo fainali, nusu fainali na fainali. Ingawa mabao mengi aliyofunga baadaye yalikuwa hatua ya makundi, bado yote yanahesabika!

WAKA 02

2. RIGOBERT SONG

Nafasi ya pili inachukuliwa na Song, ambaye wengi wanaamini alikuwa na mchango mkubwa zaidi kuliko Eto’o katika mafanikio ya Cameroon.

Beki huyo alicheza dakika zote katika AFCON za 2000 na 2002 na pia kushiriki 1996, 1998, 2004, 2006 na 2008. Jumla ya mechi 35 mfululizo, rekodi kubwa sana.

Alikuwa Mchezaji Bora wa Michuano mwaka 2002 na aliingia kwenye Vikosi Bora vya 2000 na 2006.

WAKA 01

1. AHMED HASSAN

Akimpita Song kwa nafasi ya kwanza ni Ahmed Hassan wa Misri, aliyefanikisha mambo ya ajabu kabisa AFCON.

Alishinda mataji manne (1998, 2006, 2008, 2010), akikosa mechi tatu tu kati ya 35 katika kipindi cha miaka 12.

Katika mechi 32 alizocheza, alifunga mabao manane, sita kati yake yakiwa katika hatua za mtoano. Alikuwa mchezaji wa pili katika historia (baada ya Roger Milla) kuchaguliwa Mchezaji Bora wa Michuano mara mbili.

Kwa mafanikio hayo yote, Ahmed Hassan ndiye mchezaji bora zaidi kuwahi kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika.