Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi ya Raheem Shomary kutoka Simba U20 hadi Misri

RAHEEM Pict

Muktasari:

  • Ni kama ilivyo kwa Raheem Shomary Mkinyagi, beki Mtanzania anayekipiga Ghazl El Mahalla ya Misri. Kwake maisha ya ndani na nje ya uwanja yamebadilika.

KUISHI mbali na nyumbani sio rahisi. Hata hivyo, katika harakati za kujitafuta kimaisha, inabidi iwe hivyo. Utabadilisha utamaduni, lugha na hata mtindo wa maisha uliozoea ukiwa nyumbani.

Ni kama ilivyo kwa Raheem Shomary Mkinyagi, beki Mtanzania anayekipiga Ghazl El Mahalla ya Misri. Kwake maisha ya ndani na nje ya uwanja yamebadilika.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka Misri, beki huyo wa zamani wa KMC, anafunguka mambo mengi ikiwamo anavyoishi Misri, anayojifunza katika ligi hiyo namba moja kwa ubora Afrika, ubora wake, changamoto na uzoefu wake nchini humo.

RAHE 01

AUKUMBUKA UGALI

Kila taifa lina utamaduni wake ikiwamo mambo ya msosi. Shomari anasema anakula vyakula vingi tofauti Misri, lakini anachokimisi zaidi ni ugali na huko haupatikani.

"Vyakula havina utofauti sana na nyumbani. vingi vinapatikana mfano wali, kuku, samaki, nyama. Pia napenda chakula chao kinaitwa Koshary. Ni kitamu sana na naweza pia kukipika," anasema na kuongeza;

"Sijawahi kuona ugali huku, naumisi sana. Hata hivyo, kwa asilimia kubwa vyakula vingine vipo na navipika kwani naishi mwenyewe. Ni mara chache sana nitaenda kununua chakula. Vitu huku vingi ni ghali tofauti na nyumbani, hasa mavazi na viatu vya soka."

RAHE 06

HAKUNA KAMBI

Imezoeleka timu za Ligi Kuu Bara kuingia kambini wiki moja au zaidi kabla ya mechi ili kujiweka sawa kimbinu na utimamu wa mwili. Hata hivyo, kwa Misri ni tofauti na Shoamri anafunguka;

"Hapa hakuna kambi, mambo ni tofauti. Tunafanya mazoezi na kurudi nyumbani. Siku moja kabla ya mechi ndiyo tunakutana hotelini na mara baada ya mchezo kila mmoja anatawanyika na kurudi nyumbani kuendelea na ratiba nyingine," anasema na kuongeza;

"Nyumba tunazoishi, hasa wachezaji wa kigeni kwa asilimia kubwa ni gharama za klabu na kama kuna mchezaji anataka kuishi mazingira tofauti basi anaongezea kiasi cha fedha na kuchagua ni nyumba gani anataka kuishi," anasema Shomari, nyota wa zamani wa KMC.

Shomari akizungumzia suala la ubaguzi alisema kwa Misri, hajakutana na hali kama hilo na kuweka wazi soka sasa linakutanisha mataifa mengi.

RAHE 02

KIARABU FRESHI

Haikuwa rahisi kwake kuwasiliana na wachezaji wenzake na kumwelewa kocha na licha ya kupewa mtu wa kumtafsiria, bado alikuwa anatumia lugha ya Kiingereza, ambayo pia anakiri ilikuwa kikwazo kwake.

"Changamoto kubwa ambayo nilikutana nayo Misri ni namna ya kuwasiliana, huku lugha yao kubwa ikiwa ni Kiarabu. Nilipata mkalimani ambaye pia alikuwa ananisaidia kwa Kiingereza, ambacho pia ni changamoto kwangu," anasema na kuongeza;

"Kutokana na changamoto hiyo, ilinilazimu kuingia darasani kupata elimu ya lugha hizo mbili, ambazo sasa nina uwezo wa kuzungumza. Nilitumia miezi minne tu kufanikisha hilo," anasema Shomari ambaye ana miezi sita tangu amejiunga na timu hiyo akitokea KMC. 

RAHE 07

Shomari anasema gharama juu ya kujifunza lugha hiyo ilikuwa juu yake, kwani ndiye aliyelazimika kusoma ili apate urahisi wa kuelewana. Kazi iliyompeleka huko ni kucheza; bila kuelewa, asingefikia mafanikio.

Beki huyo anasema kwa sasa anaweza kuzungumza lugha zote mbili kwa usahihi na amekuwa akiwasiliana vizuri na benchi la ufundi pamoja na wachezaji wenzake bila ya kuhitaji msaada wowote.

RAHE 03

NYOTA SITA KIKWAZO

"Mwanzo ilikuwa ngumu sana kuingia hata kwenye kikosi cha wachezaji 20, kwa sababu wenzetu wana utaratibu wao, wachezaji wa kigeni kutoka nje ya Misri kwenye kikosi cha nyota 11 uwanjani wanatumika watano pekee," anasema na kuongeza;

"Nilifika kwenye timu nilikuta tayari ina wachezaji sita wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali na tayari wameshaanza kuaminiwa kutokana na kufanya vitu vikubwa. Hivyo kazi yangu ilikuwa ni kupambana ili niingia kwenye kikosi cha wachezaji 20 wa kikosi cha kwanza. Nilifanikiwa."

Anasema baada ya kuingia kwenye idadi hiyo, kazi iliyofuata ni kutafuna nafasi ya kucheza. Akapata nafasi ya kucheza kwa dakika chache na hivi karibuni akapata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza.

"Kwa sasa ligi imesimama. Tunaendelea na maandalizi kwa ajili ya ligi ndogo ya ndani na napata nafasi ya kucheza na nayatumia mashindano haya kupambana kuonyesha nilichonacho ili niendelee kuaminiwa hadi ligi itakaporejea na nipate nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza."

RAHE 04

WABONGO WAMEJIAJIRI

Anasema Watanzania Misri wapo wengi kutafuta maisha na wengi wamejiajiri ikiwamo kufundisha lugha hali iliyomsaidia pia kujua Kiarabu.

"Nafurahi nimekutana na ndugu zangu huku ambao wamejiajiri kufundisha lugha, wamenifundisha na sijatumia gharama kubwa kujifunza. Nawashukuru Watanzania wenzangu kwa kile walichonifanyia," anasema na kuongeza;

"Wanafundisha Kiarabu kwa Kiswahili na Kiswahili kwenda Kiarabu, pia Kiingereza. Hii fursa imenifaa sana kwani sasa nimekuwa mchezaji ninayeelewa lugha ya nchi ninayocheza."

RAHE 05