Prime
Usaliti wa usajili wa haraka!
Msimu wa usajili unaendelea wakati klabu zikijiandaa kwa msimu mpya, huku mamilioni ya fedha yakitumika kuhamasisha, kusajili na kuvunja mikataba ya wachezaji na makocha.
Lakini sehemu kubwa ya mamilioni hayo yanakwenda kwa wachezaji, klabu na makocha wa nje, wakati sehemu ndogo ikibakia nchini kwa klabu, makocha na wachezaji wazawa.
Ni kweli kwamba sehemu nyingi duniani huo ndio utamaduni wa kipindi hiki muhimu katika soka, lakini kwa wenzetu ni kama nusu ya mamilioni hayo huenda nje na nyingine hubaki ndani ya nchi kwa kuwa nyiota wa viwango vinavyolingana hupishana kutoka nchi moja kwenda nyingine.
Ndio maana kwao mpira wa miguu ni biashara na una mchango wa kueleweka kwenye uchumi wan chi hizo tofauti na huku ambako hata ajira bado hainufaishi kwa kiwango kizuri vijana wetu wanaoshubudia wachezaji wa kigeni wakimiminiwa mamilioni.
Hii si kwa bahati mbaya, bali inatokea katika nchi ambazo hazioni umuhimu wa kupanga mambo kwa ajili ya mafanikio ya miaka mingi ijayo.
Bado tunafikiria mafanikio makubwa ndani ya muda mfupi, tukitaka kujihusisha na kutukuzwa kwa mafanikio hayo ya haraka ambayo ni kama vipodozi ambavyo hudumu usoni kwa muda mfupi.
Wakati nchi nyingine zikihimiza kuwepo kwa mfumo mmoja wa kuandaa watoto na kukuza vijana, kwa maana ya kulazimisha klabu zianzishe shule za soka, kwetu mamlaka za mpira wa miguu nazo zinataka ziwe na timu ya vijana kuanzia umri mdogo hadi juu badala ya kuratibu na kuteua watoto wenye kipaji kikubwa na kuwapa uzoefu.
Ni muda mrefu tangu hadithi za Leseni za Klabu zianze na msisitizo wake katika soka la watoto, vijana na wanawake lakini hakujapangwa mkakati wa utekelezaji wake na hatua ambazo tunatakiwa tupige kila baada ya miaka fulani,
Ni kama vile hatujui kwamba soka la watoto ndio soka lijalo na ndilo linaweza kutengeneza kizazi kipya cha wanasoka watakaoweza kupambana na miamba mingine ya Afrika, sit u katika mashindano ya barani humu, bali pia katika kutafuta nafasi kwenye klabu kubwa za nje ya Afrika.
Morocco leo inasumbua soka la Afrika kwa kuwa imeweka sera hiyo ya kuandaa watoto na kulea vijana. Ikisaidiwa na utawala wa kifalme, Morocco imejenga shule za watoto za soka kwenye kila kanda huku Shirikisho la Soka la Morocco likiwa na shule kuu (centre of excellence) kwa maana kwamba huchukua vile vipaji bora kabisa na kuvikusanya kwenye shule hiyo kuu kwa ajili ya masuala ya kimataifa.
Huu ni mfano mmoja wa utekelezaji wa kanuni za Leseni za Klabu, Nchi za kusini mwa Afrika nazo zina mfumo wake wan a zote huungana pamoja chini ya Shirikisho la Soka la Kusini mwa Afrika (COSAFA) kuendesha mashindano ya timu za taifa ya umri na wanawake.
Hawa huanza kupata uzoefu wa mashindano ya kimataifa mapema na ndio maana tushaanza kuelekeza macho yetu kusini mwa Afrika kusaka wachezaji wa kuwanunua kwa bei mbaya. Kwa nini? Kwa sababu wenzetu walianza mikakati muda mrefu na wakati wa mavuno ushafika. Wanakula walichopanda.
Bado kwetu tunategemea wachezaji wazuri kuibuka kama uyoga na wala tusijue walifanyaje hadi kuibuka ghafla. Hatujui akina Clement Mzize, Selemani Mwalimu, Abushir, Feisal Salum na wengine wengi waliibukaje na hatuna kiburi cha kujivunia mafanikio yao kwa kuwa hatujachangia kuibuka kwao.
Kipindi hiki cha usajili tulitarajia kusikia mamilioni ya fedha yakielekezwa kwa nyota wetu wazawa na mengine yakiingia kwenye klabu baada ya kuuza wachezaji nyota wa kigeni tuliowasajili kwa makini na kuvutia klabu kubwa za nje.
Sio hawa wanaoondoka kwa sababu hawajaweza kuonyesha ubora na badom tukalazikmika kutumia mamilioni ya feda kuvunja mikataba au hawa wanaoondoka baada ya mikataba yao kumalizika.
Kila ukitafakari kipindi hiki cha usajili unaona tunakosea kwa kiasi kikubwa kuliko kupatia. Na hii ni kwa sababu hatutaki kuweka miakakti ya muda mrefu ambayo huenda tsione mafanikio yake. Tunataka kuweka mipango ya muda mrefu isiyo ya uhakika ambayo inaweza kutupa mafanikio ya uongo.
Fikiria inawezekanaje mamlaka za soka zikalea wachezaji tangu wakiwa wadogo hadi kufikia ujana eti kwa lengo la kukaa pamoja na kusahau wengine wengi walioko mitaani ambao pengine wana uwezo mkubwa zaidi.
Timu za taifa ni sehemu ambazo wachezaji wanatakiwa wagombee kufika na si kulelewa ili wawemo ndani. Ni sehemu ya kushindania kuingia.
Unaweza kufanikiwa na kundi hilo la wachezaji lakini mafanikio yakawa ya wakati huo tu. Lengo linatakiwa liwe na kutengeneza kundi kubwa la wachezaji wa baadaye ambao watapambana kupata nafasi ya kuitwa timu za taifa.
Wakati huu tunapoelekea kumaliza kipindi cha usajili ni muhimu kwa mamlaka kutafakari upya kuhusu sera zake za kuandaa, kulea na kukuza wachezaji kwa kulinganisha na kiwango cha fedha kinachotoka ndani kwenda nje badala ya kubakia humuhumu kunufaisha wadau tofauti na taifa kwa ujumla.
Kama klabu zote 16 za Ligi Kuu zinakimbilia kusajili wachezaji kutoka nje zikijua zinaweza kusajili hadi 12, ni kiasi gani cha fedha kinatoka kwenye uchumi wetu mdogo? Kama klabu 12 tu zitaajiri makocha wa kigeni, ni kiasi gani cha fedha kitatoka kwenye uchumi wetu?
Tunahitaji tafakari mpya ya sera zetu na tayari Fifa na Shirikisho la Afrika (CAF) yalishatoa mwelekeo; Leseni za Klabu.