Prime
Somo la uwajibikaji Kombe la Dunia hili hapa
Kwa binadamu wa kawaida, kila siku ni fursa ya kuongeza kitu fulani katika maisha. Kitu hicho chaweza kuwa kuelewa jinsi ya kuishi na watu wa aina fulani, kupata elimu zaidi kuhusu kazi yako, kujifunza kwa wengine kuhusu uendeshaji wa mambo na njia za kujipatia kipato zaidi.
Mchezaji hupata mbinu zaidi kila siku anapoingia uwanjani au kuangalia mechi na hivyo anaporudi uwanjani huwa ni tofauti na yule wa jana hata kama alilojifunza bado hajaweza kulifanya kwa ukamilifu.
Ndivyo na taasisi zetu zinavyotakiwa ziwe zinajifunza kwa wengine katika uendeshaji, usimamizi, uwajibikaji na uwazi ili ziwe na mabadiliko chanya kila iitwapo leo.
Kwa kuangalia fainali za Kombe la Dunia tunaona mengi mapya, baadhi tukiwa tunaweza kuyafanya kulingana na uwezo wetu na mengine hatuyawezi kwa sababu ya hali yetu Ya kiuchumi.
Tumezoea kusubiri hukumu za Kamati ya Saa 72 kila raundi ya Ligi Kuu inapoisha. Wachezaji, waamuzi, makocha, viongozi na hata mashabiki hujikuta katika adhabu za kufungiwa, kutozwa faini, kushushwa daraja au kupelekwa mbele ya kamati nyingine za nidhamu na maadili kwa ajili ya hatua zaidi.
Na mara nyingi wanaofikiwa na rungu hilo huwa ni waamuzi ambao huadhibiwa baada ya wajumbne wa hiyo kamati kuangalia marudio ya picha za video ili kujua mwamuzi hakufanya uamuzi sahihi au alishindwa kutafsiri sheria.
Ni jambo la kushangaza kwamba hawa wanaotumia teknolojia ambayo haina idhini ya mamlaka za mpira duniani, wanawaadhibu waamuzi waliokuwa wanakimbia uwanjani bila ya teknolojia yoyote inayoweza kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi.
Hawa hawasubiri kiongozi wao awatetee kwamba kwa mazingira waliyokuwa nayo uwanjani, wasingeweza kuona tukio vizuri kiasi cha kufanya maamuzi sahihi.
Na viongozi hao hawasikii kuwajibika kuwatetea, bali hutulia kuangalia maamuzi yasiyoweza kupingwa na yeyote kwa mujibu wa kanuni.
Lakini hilo halipo kwa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa). Pamoja na ukweli kwamba Fifa imewekeza kwenye teknolojia kusaidia marefa kufanya maamuzi sahihi, bado inajisikia kuwajibika kutoa ufafanuzi wa matukio tata, ikijua kabisa kuwa waamuzi walikuwa sahihi.
Kamati ya Waamuzi ya Fifa imekuwa ikitoa ufafanuzi katika mikutano inayofanyika baada ya mechi, kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu matumizi ya kanuni na hivyo kuondoa tuhuma dhidi yake.
Maelezo rasmi hujikita sababu za refa kufanya uamuzi fulani na kueleza kama alikuwa sahihi au alitumia vizuri sheria za soka na hata kabla ya mashindano yake kuanza, shirikisho hilo hufanya mikutano kidigitali na makocha na waamuzi kueleza jinsi sheria fulani zitakavyotafsiriwa na hivyo kuwaweka tayari kupokea maamuzi,
Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya Fifa, Perluigi Collina hujitokeza kutoa ufafanuzi wa maamuzi ya refa yanayotawaliwa na tafsiri tofauti na kusababisha shirikisho hilo lituhumiwe kuwa linajaribu kuibeba timu na mtu ambaye hatajwi.
Katika mechi kati ya Misri na Argentina kulitokea maamuzi tata ambayo yaliinufaisha Argentina ambayo ni bingwa mtetezi. Katika tukio la kwanza mchezaji wa Misri Marwan Attia alionekana akimchezea rafu Lisandro Martinez na refa kuipa Argentina penati.
Collina alisema uamuzi huo ulikuwa sahihi kwa kuwa uchunguzi wa picha za marudio ulionyesha refa alikuwa sahihi.
Katika tukio la pili, mshambuliaji wa Misri, Mohamed Salah alionekana akichezewa rafu na beki wa Argentina, Julian Alvarez, lakini refa hakupuliza filimbi. Collina alisema rafu hiyo ilikuwa ni mgusano wa kawaida
Pia utata mwingine uliibuka katika mechi kati ya England na Norway iliyoisha kwa Simba watatu kushinda kwa mabao 2-1. Katika bao moja la England mpira ulionekana kama umegusa waya za kamera inayozunguka juu uwanjani na ulipotua ulmfikia mchezaji wa England aliyeanzisha shambulizi la bao.
Wachezaji wa Norway walilalamika mpira huo ulipoteza mwelekeo baada ya kugusa kametra hiyo, lakini Collina alieleza baadaye kuwa kifaa kilichowekwa ndani ya mpira (chip) hakikuonyesha kuwa mpira uligusa sehemu yoyote wakati ukiwa juu na hivyo refa alikuwa sahihi kuendelea na mchezo.
Hii ni baadhi ya mifano inayoonyesha Fifa inajaribu kuweka uwazi na kuongeza uwajibikaji badala ya kukalia kimya mijadala kuhusu utata katika uamuzi.
Hiki ni kitu ambacho mamlaka zetu za soka hazina budi kuiga ili kuondoa malalamiko na tuhuma zisizo na msingi kila baada ya kumalizika kwa mechi za ligi.
Ni lazima kiongozi wa waamuzi aagizwe kutoa ufafanuzi wa maamuzi ya marefa wake na awe na ujasiri hata wa kusema kulikuwa na tafsiri potofu katika uamuzi fulani badala ya kuwaachia wajumbe wa Kamati ya Saa 72 kuamua kila kitu.
Uamuzi ni taaluma nyeti sana kati ya nguzo nne za mpira wa miguu na hauna budi kulindwa kwa wivu mkubwa, huku uwazi na uwajibikaji ukifanyika kwa makini ili kurudisha Imani kwa wadau wa mpira.
Kama teknolojia ya Mwamuzi Msaidizi wa Video (V.A.R) inatushinda kwa sababu ya gharama, hata uwajibnikaji utushinde? Kamati ya Waamuzi inafanya nini kama hata kazi ya kujadili, kutetea na kuadhibu marefa haifanyi? Kwa nini Kamati ya Waamuzi haina wivu na taaluma yake?
Ni wakati sasa kwa kamati kuchukua hatua ili waamuzi wasiwe kichefuchefu midomoni m,wa wadau wa soka.