Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uchovu hauondolewi kwa kusajili wachezaji 40

ZENGWE Pict


Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza mabadiliko ya kanuni za Ligi Kuu yanayolenga kukabiliana na jukumu kubwa la kitaifa mwakani wakati Tanzania, Kenya na Uganda zitakapoandaa fainali za mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON).


Fainali hizo zitakuwa za kwanza kwa ukanda wa Afrika Mashariki kuziandaa na zitafanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 17 wakati fainali itakapochezwa kuamua bingwa wa Afrika katika soka.


Ni kwa jinsi hiyo, TFF imeona ifanye mabadiliko ya kanuni inayohusu idadi ya wachezaji wanaosajiliwa na klabu ili kuziwezesha kucheza mechi mfululizo na kuondokana na hoja ya uchovu. TFF imesema klabu zitaruhusiwa kusajili wachezaji 40.

Rais wa TFF, Wallace Karia aliwataka wasemaji wa klabu na maofisa habari kutoendeleza hoja za wachezaji kuchoka wanapocheza mechi mfululizo kwa kuwa sasa klabu zina idadi kubwa ya wachezaji na zitaweza kuwapumzisha pale zitakapokuwa na mechi mfululizo.

ZENG 01

Kwa sasa klabu zinasajili wachezaji 30 na si zote zinazomudu kusajili idadi hiyo kubwa, huku kila mara kukiwa na kesi za madai ya mishahara na ada za kusaini mikataba, kesi ambazo hufikishwa Fifa.

Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), timu zinatakiwa zipate angalau saa 72 kutoka mechi moja hadi nyingine ili kuwapa wachezaji muda wa kupumzika na kurejesha nguvu mwilini.

Hii haimaanishi kupumzisha wachezaji waliocheza mechi iliyopita tu, bali timu nzima kwa kuwa maandalizi huhusisha wachezaji wote. Hata ikitokea wachezaji hadi saba wanakaa benchi, moto wanaoupata nje ya uwanja ni sawa na wale waliomo uwanjani na tofauti kubwa ni katika kushiriki moja kwa moja.

ZENG 03

Hoja hiyo ya kuongeza idadi hadi kufikia wachezaji 40 haikuchakatwa vizuri kwa maana ya kuangalia uhalisia wake, uzoefu, mataizo na utamaduni wa mpira wa miguu, badala yake watungaji waliangalia faida peke yake.

Kwanza, kwa kuangalia uhalisia, suala hilo haliwezekani kufanyika kwa ufanisi kwa asilimia kubwa kwa kuwa hata idadi Azam zitaweza kusajili wachezaji 40 lakini nyingi zitashindwa, hivyo hakutakuwa na usawa katika ushindani hata kama suala hilo ni la kikanuni.

Simba, Yanga, Azam n ahata Singida Black Stars zinaweza kuchomoa nyota wengi walio kwenye klabu nyingine na kuwavundika kwa kuwa zitakuwa zinajua wakiwa huko wanaweza kuzisumbua na hivyo dawa ni kuzidhoofisha klabu ambazo haziwezi kumudu gharama za kuwatunza nyota wake.

ZENG 02

Katika hali halisi inawezekanaje Timu ikawa na idadi ya wachezaji wanaoweza kuunda vikosi vitatu? Yaani hata mazoezini, kocha akiamua kuchezesha vikosi viwili kamili, kuna wachezaji 18 watakaa benchi hata mazoezini.

Hata ufuatiliaji wa mwalimu katika maendeleo ya wachezaji hautakuwa na ufanisi. Wako wachache atakaoweza kuwafuatilia kwa karibu lakini wengi watakosa ufuatiliaji wa karibu.

Na hilo kundi la wachezaji 18 wanaoweza kukaa benchi hata mazoezini, litadumazwa kwa kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara na hivyo kumpa shida kocha wa timu ya taifa kujua vizuri maendeleo ya wachezaji anaodhani anaweza kuwateua.

ZENG 05

Kwa hiyo, athari haiishii kwa wachezaji pekee, bali hata kwa timu ya taifa.

Katika uzoefu, ni kweli Fifa iliongeza idadi ya wachezaji na idadi ya wanaofanyiwa mabadiliko, lakini suala lile lililikuwa wakati wa dharura ya ugonjwa wa virusi vya corona, Covid.

Fifa ilifanya hivyo kwa wakati huo kwa kuwa katika timu idadi kubwa ya wachezaji wanaweza kuambukizwa na kwa kanuni za afya walio na maambukizi hawaruhusiwi kujichanganya na wengine.

Safari hii hakuna dharura yoyote. Tulishajua tutaandaa fainali za CHAN tangu miaka mitatu iliyopita hivyo tulitakiwa tuwe tumeshafanya maandalizi ya kutosha kukabiliana na athari zake kwa soka la ndani.

ZENG 04

Msimu wa mwaka 2024/25 mechi ya mwisho ya Ligi Kuu ilifanyika Juni 15 kutokana na matatizo ya uendeshaji, hasa uahirishaji hovyo wa mechi kutokana na maombi ya klabu au kurekebisha mambo. Mechi ya mzunguko wa pili kati ya Simba na Yanga ilivurugwa na uholela na mzozo wake ulidumu kutoka mwezi Machi hadi Juni.

Ligi ilikuwa inasimamasimama kwa sababu ya mechi za timu ya taifa, kambi za Taifa Stars nje ya nchi, ushiriki wa klabu zetu katika mashindano ya kimataifa na mashindano mengine kama Ligi ya Muungano, Kombe la Mapinduzi na zile mechi za Fifa Series.

Haya ni mambo yanayoweza kuepukika ikiwa kutakuwa na nidhamu ya kuheshimu ratiba, kuendesha mambo kisayansi na kutokubali maombi yasiyoheshimu utamaduni wa mpira ya kuahirisha mechi.

Ulaya timu zinazocheza Ligi ya Mabingwa Jumanne, hupangiwa mechi za ligi za ndani Ijumaa, wakati zile zinazocheza Jumatano hucheza mechi za ndani Jumamosi, huku zile zinazochezaji Kombe la Europa Alhamisi hucheza mechi za ndani Jumapili.

Hawakubali maombi ya timu ya kupata muda wa kutosha eti kwa sababu zina mechi ngumu dhidi ya Real Madrid, Manchester City, Juventus au Bayern Munich. Labda itokee wiki hiyo zikawa hazina mechi, kitu ambacho ni kigumu.

Haiwezekani timu ikawa na mechi tano za viporo au hadi sita eti kwa sababu ilikuwa na mechi muhimu za kimataifa. Huu ni uzembe ambao hauwezi kumalizwa kwa kubadilisha kanuni bali kuwawajibisha wanaosababisha hali hiyo.

Msimu wa ligi kwa nchi nyingi huanza mwezi Agosti na kumalizika Mei mwaka unaofuata. Lakini kwa uholela wetu, huwa tunamaliza Juni na tunaona sawa. Badala ya kuangalia kasoro zetu tunakimbilia kubadilisha kanuni ili tuendelee na mazoea ya kuahirisha mechi ovyo.

Suala la uchovu wa wachezaji haliwezi kutibiwa na idadi kubwa ya wachezaji wanaosajiliwa timu moja, bali tathmini ya kina ya sababu zinazotufanya tuchelewe kumaliza msimu na nidhamu ya kuheshimu na kutekeleza mipango, sheria na kanuni zetu.

Tunahitaji umakini na si kudhanidhani na kupitisha kanuni ambazo haziendani na utamaduni wa mpira wa miguu.