Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tshabalala na Kibabage wanavyowachanganya binadamu

JICHO Pict


BAO zuri lilifungwa na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ katika ushindi wa mabao 6-0 ambao Yanga waliupata kwa Mbeya City mwishoni mwa wiki iliyopita. Ilikuwa mechi ya kisasi na Yanga waling’ata meno zaidi.


Linakuwa bao la tatu kwa Tshabalala msimu huu. Mabao yake na kiwango chake akiwa Yanga kinaacha maswali. Huku mitaani watu wamekuwa wakibishana. Mashabiki wa Simba wamekuwa wakijihoji kama yalikuwa maamuzi sahihi kuachana na Tshabalala baada ya kile kilichoonekana kuchokana baina yao na mchezaji.


Ndiyo, hakukuwa na sababu za msingi sana kwa Simba kuachana na Tshabalala. Nadhani walikuwa wamemchoka tu. Simba na Yanga huwa hazishindwi kuwabakiza wachezaji wake muhimu wanaowahitaji. Labda zitokee timu kutoka nje na kutoa madau makubwa kama ilivyowahi kutokea kwa kina Clatous Chotta Chama, Fiston Mayele, Tuisila Kisinda, Jose Luis Miquissone na wengineo. Humu ndani kwa ndani huwa hawashindwi jambo lao.

Nafahamu Simba walikuwa na kiu ya kuleta mabadiliko katika kikosi chao baada ya Yanga kuwasumbua kwa kutwaa mataji ya ligi kuu mara nne mfululizo. Kulikuwa na hamu ya kuleta changamoto mpya kikosini na Tshabalala alikuwa miongoni mwa wachezaji ambao walitolewa kafara.

Ilidaiwa walishindwana katika dau. Usikubali sana katika hili. Wakubwa wakitaka kubaki na mchezaji wao huwa hawawezi kushindwana.

Na sasa Tshabalala amekuwa katika kiwango bora katika kikosi cha Yanga. Anaonekana ameshinda vita dhidi ya mlinzi wa kigeni, Chadrack Boka.

JICH 01

Chini ya Roman Folz Tshabalala alianza kusugua benchi kimtindo lakini chini ya Pedro Concalves nyota yake imeonekana kuwaka. Sikumbuki kama kuna msimu aliwahi kufunga mabao matatu licha ya kusifiwa vilivyo kwa ubora wake upande wa kushoto.

Kuna wachezaji wengi walikuja kwa mbwembwe pale Yanga dirisha kubwa lililopita. Akina Doumbia. Hata hivyo mpaka kufikia hii Aprili Tshabalala anaweza kuwa usajili bora zaidi uliofanywa na Injinia Hersi Said na genge lake.

Labda tuendelee kumpa muda Alan Okello aliyewasili Januari ambaye anaendelea kujitutumua kwa sasa. Vinginevyo Tshabalala ndio uhamisho bora mpaka sasa.

Wakati sintofahamu yake ikiendelea kwa mashabiki wa Simba kule upande mwingine kuna sintofahamu pia. Kule kwa watani zao Nickson Kibabage anaonekana kung’ara katika upande wa kushoto wa Simba.

Hauwezi kumlinganisha Kibabage na Tshabalala kwa sababu nyingi tu lakini ukweli ni kila mmoja anang’ara katika timu yake mpya. Kibabage aliwasili Januari akitokea Singida Big Stars alikorudishwa na Yanga.

JICH 02

Pamoja na furaha ya Wanasimba kwa ubora ambao wachezaji wapya kama Anicet Oura na Libasse Gueye wanaouonyesha kwa sasa lakini Kibabage pia anawakosha.

Ameleta nguvu mpya kikosi kwa sababu ya kasi yake na kujituma kwake. Mimi hajaniachia maswali na nawashangaa wanaomshangaa Kibabage kwa kuwaongezea kitu. Awali waliwazodoa viongozi wao kwa kumchukua mchezaji ambaye Yanga walimtema lakini sasa Kibabage anawaziba midomo.

Binafsi nilishangaa pia uamuzi wa Yanga kuachana na Kibabage kama ambavyo nilishangaa uamuzi wa Simba kuachana na Tshabalala.

Kibabage aliondoka Yanga akiwa hajaharibu kitu na huku akiendelea kuimarika kila siku akipambania nafasi yake na Boka.

Hata maamuzi ya Yanga kumchukua kutoka Singida Big Stars na kuachana na David Bryson yalionekana kama vile yapo sahihi.

Kitu kizuri ambacho akina Injinia wanaweza kujitetea ni kwamba Yanga waliendelea kucheza vizuri bila yeye. Na alipokuja Tshabalala aliwafichia aibu zaidi kwa sababu vile vile Boka alipata majeraha hapo katikati. Kama wangekuwa wamemchukua mchezaji mwingine ambaye angechuja katika nafasi hiyo watu wangemkumbuka Kibabage.

JICH 03

Ni kama tu Kibabage anavyopambana kuwafichia aibu mabosi wa Simba walioachana na Tshabalala. Walau Simba hawajilaumu sana kuachana na Tshabalala kwa sababu Kibabage amepambana kuziba pengo. Suala la kufunga au kutofunga ni jambo tofauti. Kwa mlinzi kufunga ni suala ongezeko tu lakini kitu cha msingi ni kuumudu mchezo kwa ujumla.

Tshabalala amejikuta katika eneo sahihi na wakati sahihi. Na labda mabao yake yanawakumbusha tu watu wa Simba kwamba wanakosa uzoefu wake lakini kwa ujumla Kibabage amekuwa nguzo muhimu katika ujenzi wa Simba mpya.

Amepeleka uhai upya katika timu ambayo hivi karibuni wachezaji wengi wapya wamekuwa wakifeli.

JICH 04

Kuthibitisha timu zao zimelamba dume majuzi nilikuwa na wachezaji hawa wawili pale Kigali katika mechi za kirafiki za FIFA. Kocha, Manuel Gamondi aliamua kwenda na Kibabage badala ya Pascal Msindo na akanieleza namna anavyokoshwa na wepesi wa Kibabage katika kujenga mashambulizi na kulihami lango lake.

Bado Tshabalala alikuwa chaguo la kwanza la kocha kwa sababu ya utulivu na uzoefu wake.

Hata hivyo Kibabage kwenda mbele ya Msindo ambaye ni fundi wa mpira pale Azam ilikuwa ni ishara nyingine Kibabage amekuwa akifanya vizuri katika jezi ya Simba tangu kuwasili kwake.

Kuna mambo machache ambayo inabidi ayafanyie kazi ikiwemo tatizo kubwa la walinzi wetu kutopiga krosi sahihi katika wakati sahihi.

JICH 05

Kitu kizuri katika yote haya ni wachezaji wenyewe, Tshabalala na Kibabage hawakuondoka vibaya katika, hasa Tshabalala ambaye amecheza Simba kwa miaka mingi. Hakutukana mtu, hakukejeli watu, hana maneno mabaya dhidi ya timu yake ya zamani. Kifupi hana baya kwa watu wa Simba. Alijaribu kubaki lakini haikuwezekana. Maisha yameendelea.

Pamoja na yote haya niliyoandika kitu cha kuchekesha zaidi nitakuja kuandika siku nyingine. Kiwango cha mlinzi wa kushoto wa TRA. Valentin Nouma. Nilimtazama pambano la TRA na Simba pale Arusha alikuwa wa moto. Huyu naye aliondoka Simba baada ya kushindwa kumpora namba Tshabalala.

Kuna mashabiki wa Simba wanahoji kama mabosi wa Simba walikuwa sahihi kuachana na Nouma. Ni kweli.

JICH 06

Hata mimi nimekiangalia kiwango chake siku ile na kujiridhisha ni beki mzuri. Baada ya lile pambano nilisikia uvumi Yanga wanaisaka saini yake ili awe mbadala wa Boka ambaye anaweza kuondoka klabuni.

Vyovyote ilivyo nimegundua ukichukua walinzi wa pembeni na wazawa katika nafasi ya upande wa kushoto tumekuwa na wachezaji bora kuliko upande wa kulia.

Wachukue Tshabalala, Kibabage, Boka, Nouma, Msindo na wengineo hawa ni bora zaidi kuliko ule upande wa akina Shomari Kapombe na wadogo zake. Katika ligi yetu kushoto ni bora zaidi kuliko kulia. Nafungua mjadala.