Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Teknolojia inapogeuzwa jukwaa la matusi Simba, Yanga

Muktasari:

Sakata la msemaji wa Simba, Haji Manara na mtangazaji wa Clouds FM, Shaffii Dauda ni jipya kati ya mizozo mingi ambayo huhusisha waandishi wa habari na watendaji wa klabu hizo na ambayo kwa kiasi kikubwa hufanana.

Sakata la msemaji wa Simba, Haji Manara na mtangazaji wa Clouds FM, Shaffii Dauda ni jipya kati ya mizozo mingi ambayo huhusisha waandishi wa habari na watendaji wa klabu hizo na ambayo kwa kiasi kikubwa hufanana.

Na kwa mujibu wa Manara, mzozo huo ulisababishwa na mtu katika moja ya makundi ya wapenzi wa michezo, aliyechomoa kipande cha sauti yake na kukiweka hadharani, kinyume na utamaduni wa hayo makundi.

Hakatai kwamba hakusema hayo, lakini anamlaumu mtu aliyechomoa sauti kutoka katika kundi la watu wanaoelewana na kuweka hadharani ambako kuna watu wenye akili, hisia na mawazo tofauti.

Bila shaka, Dauda ni lazima alichukizwa na maudhui katika sauti hiyo na ndio maana akajibu mashambulizi vikali na kusababisha mzozo uonekane kuwa mkubwa, hasa baada ya watu wengine kujiunga katika lawama dhidi ya Manara, wakichukizwa na kitendo cha kuponda wachambuzi, ambao sakata hili limejumuisha hata waandishi wa habari.

Kilicho dhahiri ni kuwa Manara alitoa maneno hayo na ana kawaida ya kutumia sauti zaidi katika mijadala ya makundi ya WhatAssap kuliko kuandika ujumbe hivyo ilikuwa rahisi kumnasa katika mzozo huo.

Lakini ilifikia vipi hadi Manara akamuita mtu ambaye amepewa majukumu makubwa kwa mwajiri wake, jina la takataka? Ni kitu gani kilisababisha Manara afikie hatua hiyo ya “kumsengenya” Dauda hadi kumuita “takataka?”

Hii ni tabia ambayo inazidi kukua katika makundi ya WhatAssap na hata katika mitandao mingine ya kijamii. Watu sasa hawajadili hoja na wala sababu ya mtu fulani kuibua hoja fulani. Wakati Simba ilipokuwa katika mazungumzo na wachezaji wake watatuTshabalala, John Bocco na Shomari Kapombe, ubashiri ulikuwa mwingi kuhusu hali ya baadaye ya nyota hao.

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali, kila mwandishi au mchambuzi angeweza kuchambua suala Fulani kutokana na vyanzo vyake na ufahamu wake kuhusu mikataba ya wachezaji na umuhimu wa kuwabana mapema kabla ya kushawishiwa na klabu nyingine.

Kwa hiyo haikuwa ajabu kwa Dauda kuona kuwa pengine suala hilo lilitokana na viongozi kuwa makini hadi mikataba kukaribia kuisha na wachezaji kusadikiwa kuwa wanataka kipato zaidi. Inawezekana Dauda alikwenda mbali zaidi kuzungumzia udhaifu huo, kitu ambacho kingemuudhi zaidi mlengwa, yaani mtendaji mkuu wa klabu.

Mwingine angepata habari kuwa wachezaji hao labda walikuwa safarini kuondoka kama ilivyokuwa kwa wawili kati ya hao walipotoka Azam na kujiunga na Simba. Haya ni mambo ya kawaida. Ilikuwaje basi mitazamo hiyo tofauti iishie katika takataka.

Kwangu si ajabu kwa kuwa nimekumbana na matusi hayo mara nyingi, wakati mwingine nikihamaki na kujibu vibaya na wakati mwingine nikiyaachia kwa kuona hakuna umuhimu wa kufanya hivyo.

Watu hawataki kujadili hoja na wameshachukulia mitandao ya kijamii ni sehemu ya kutupa uchafu, kebehi, kukera, kudhalilisha, kushambulia na mambo mengine yasiyo na maana. Wengine wameona mitandao ya kijamii ni sehemu ya kujifaharisha, kuonyesha uwezo na ujinga mwingine.

Kwa hiyo mtu anapotoa hoja Fulani, mtu wa kwanza kuizungumzia atasema ama nyie mikia, nyie utopolo, wewe mbona ulikuwa kiongozi mbovu na ukifuatilia hadi mtu wa 20 kutoa maoni unaweza hata usijue mtuma post alitaka kuzungumzia nini.

Hawa ndio watu wanaotaka mpira wetu usonge mbele bila ya kujadili masuala muhimu yanayouzunguka. Na mambo yanapoharibika, huishia kulaumu viongozi wala wasijue tatizo liko wapi.

Nilidhani maendeleo ya teknolojia yangetoa jukwaa zuri zaidi la mijadala makini kuhusu michezo yetu, lakini inasikitisha sana kwamba teknolojia imekuwa jukwaa la kudhalilishana, kukebehi, kushambuliana, kutukanana na hata kuwa chanzo cha uhasama.

Ni muhimu sana kutumia teknolojia hii kwa maendeleo badala ya kuwa sehemu ya takataka, na kibaya zaidi kuwa jukwaa la kujianika udhaifu wetu, ujinga wetu, umbumbumbu wetu na hata hisia zetu potofu.

Na kuponda utendaji au uchezaji wa timu moja, au kjusifia nyingine hakumaanishi kwamba anayefanya hivyo ni mjinga anayefaa kutukanwa bali kuchukuliwa kama mtu anayeibua hoja ili ijadiliwe kwa mapana na marefu.

Yanga na Simba zisitufanye tuweke pembeni akili zetu, bali zitufanye tuwe tunafikiria kwa kutazama picha kubwa zaidi.