Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

GSM ametanua misuli kwa Shalulile, tusubiri majibu

JICHO Pict


GHALIB Said Mohamed ametanua msuli na kuinasa saini ya mshambuliaji wa kimataifa wa Namibia, Peter Shalulile. Habari ilikuja kuleta mshtuko mkubwa kwa mpira wetu. Hata kule Afrika Kusini imeleta mshtuko mkubwa. Hata kwao Namibia itakuwa imeleta mshtuko mkubwa. Kule Namibia Shalulile ni 'Mbwana Samatta' wao.


Kwa nini huku tumeshtuka? Licha ya kwamba Shalulile ameondoka bure Mamelodi Sundowns tuliamini dau lake ni kubwa. Dau la kupata saini yake yeye kama yeye 'signing fee'. Halafu pia mshahara wake. Hapo hapo kulikuwa na timu ambazo zilikuwa zinamtaka Afrika Kusini na Libya. Ghalib alimshawishi nini Shalulile? Inabakia kuwa siri yake.


Kikubwa zaidi ni ameweka pesa ndefu kumpata. Ameamua kuweka pesa nje ya mawazo ya watu wa Yanga. Inadaiwa ameweka zaidi ya Dola 750,000 kuinasa saini yake na mshahara wake wa jumla akiwa nchini. Kiasi hiki kama asingetoa hakuna ambaye angemlaumu. Ameamua tu kwenda mbali nje ya utaratibu wa kawaida wa usajili wa mastaa wetu.

Afrika Kusini na kwao Namibia wameshtuka kwa sababu hizo hizo. Sawa Shalulile hakuwa anapata nafasi katika kikosi cha kwanza cha Mamelodi Sundowns msimu uliopita lakini bado anabakia kuwa mmoja kati ya washambuliaji wenye majina makubwa katika soka la ndani la Afrika. Kwangu mimi ndiye mshambuliaji bora wa ndani wa soka la Afrika na nafasi yake kwa sasa imechukuliwa na Fiston Mayele.

Ghalib alihitaji kutanua mbavu zake kumpata Shalulile. Lazima amepambana. Na hii inathibitisha kitu kimoja tu. Matajiri wetu wa timu tatu kubwa nchini, Simba, Yanga na Azam wana uwezo wa kuwapata hawa kina Shalulile lakini kiwango chao cha uwekezaji wameamua kiwe na kawaida tu. Afrika mpira haulipi moja kwa moja. Unalipa kwa njia ya nyuma. Matajiri wachache waliowekeza katika mpira wa Afrika wanafanya hivyo kutangaza majina yao kwa sababu za kisiasa au kibiashara.

JICH 01

Unajiuliza Patrice Motsepe ile timu yake inamlipa nani kwa kiasi anachowekeza pale Mamelodi Sundowns? Anaweza kununua mchezaji mmoja kwa Dola 3 milioni. Inamlipaje wakati kuna nyakati analazimika kuingiza mashabiki bure pale Pretoria kwa ajili ya kuitia timu nguvu inapocheza mechi kubwa. Timu yenyewe kwanza ina mashabiki wachache.

Motsepe anafanya kama rafiki yake Moise Katumbi. Wanachukua pesa zao katika migodi wanayomiliki wanaingiza katika timu.  Kwa sasa siasa zimemwendea vibaya Katumbi kiasi kwamba hataki hata kuingiza pesa ndefu pale TP Mazembe. Ingekuwa anaitumia timu kibiashara huu ndio ulikuwa wakati wa yeye kuingiza pesa. Hapo hapo unajiuliza Ghalib anapata nini kwa kuwekeza kwa kina Shalulile?

JICH 03

Wakati fulani tulijidanganya kwa biashara yake ya jezi. Je ni kweli tukikupa wewe biashara ya jezi unaweza kuiendesha Yanga? Siyo kweli. Naamini anawekeza katika Yanga kwa ajili ya kutengeneza jina ambalo litafanya kazi katika biashara zake nyingine. Ndio maana hata Afrika Kusini na Namibia ambako Shalulile ametoka hawawezi kuamini Tanzania kuna tajiri wa kuwekeza kwa Shalulile akapata faida moja kwa moja.

Ni kama ilivyo kwa Waarabu wa Saudia. Hauwezi kuona moja kwa moja faida wanayoipata kwa kuweka pesa nyingi kwa kina Cristiano Ronaldo. Wanachukua pesa ya mafuta wanaitia katika mpira. Kina Ronaldo wamecheza huku mishahara yao ikiwa haikatwi kodi. Mwarabu ana jambo lake katika kuutangaza mpira. Hawa kina Al Nassr hawana hata mashabiki wengi kihivyo.

Vipi kuhusu Shalulile mwenyewe? Huyu ndiye mfungaji bora wa muda wote katika Ligi kuu ya Afrika Kusini. Lakini pia amewahi kuwa mfungaji bora mara nne katika ligi kuu ya Afrika Kusini. Sio mbaya kuhatarisha pesa yako kumchukua Shalulile. Pale Mamelodi ni kwa sababu tu Motsepe anaweka pesa ndefu kwa wachezaji wakubwa wenye uwezo ndiyo maana Shalulile aliishia benchi msimu uliopita. Lakini Tembo akikonda hawezi kumfikia Mbuzi.

JICH 04

Shalulile anaweza bado kuwa na mabao mengi katika ligi yetu. Hii nadhani anaweza kuimudu vizuri tu katika umri wa miaka 32 kama ambavyo Clatous Chama anaimudu katika umri wa miaka 35. Swali labda lije katika michuano ya kimataifa. Walinzi wa Kagera Sugar bila ya kuwakosea heshima hawawezi kukabiliana na moto wa Shalulile. Swali litakuja katika mechi za kimataifa.

Uzuri wa mechi za kimataifa ni utaendana na uzuri wa timu yake Yanga. Akifunga mabao saba tu ya mechi za kimataifa atakuwa amewavusha vizuri tu Yanga na uwekezaji wa Ghalib utakuwa umelipa. Nawaelewa Yanga kwa kulipa kiasi kikubwa kwa Shalulile. Dunia ina uhaba wa washambuliaji. Afrika ina uhaba wa washambuliaji. Kila mahala kuna uhaba wa washambuliaji.

Haishangazi kuona sio Yanga tu waliokuwa wanaisaka saini yake. Hata watani zao walitamani kumpata. Ni jambo la kawaida. Licha ya umri wa miaka 32 lakini inatia majaribu makubwa ya kuweka kiasi kikubwa cha pesa kwake kwa sababu ya rekodi zake. Ni aina ya wachezaji ambao kama kuna uwezekano wa kumpata unafanya kila unaloweza kumpata.

JICH 02

Nini akitegemee katika mpira wetu? Shalulile ategemee kupata presha kubwa kutoka kwa mashabiki wa timu yake Yanga na mashabiki wa watani zao, Simba. Ndivyo mpira wetu ulivyo. Hata hivyo halitakuwa jambo la ajabu kwake kwa sababu hata Afrika Kusini mpira wao una presha kubwa kutoka kwa mashabiki. Mashabiki wanataka matokeo zaidi.

Akitaka hata mashabiki elfu tano wa kumpokea pale uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere atawapata. Lakini uwanjani atakumbana na presha nyingi na lawama nyingi hata katika mambo yasiyomhusu. Ndio mpira wetu ulivyo.  Hatuna tofauti sana na watu wengine duniani ambao mpira upo moyoni.

Ujio wake pia unathibitisha namna ambavyo mpira wetu umevuka mipaka na kuwafikia watu wa mataifa makubwa kisoka Afrika. Watu wa Afrika Kusini inawezekana wameshangaa kwa Shalulile kuja kwa sababu za kipato zaidi lakini ukweli ni kwamba wameanza kuwa na ufahamu mkubwa na soka letu. Miaka ya karibuni Simba na Yanga zimeshindana na Kaizer Chiefs na Orlando Pirates katika michuano ya kimataifa.

Hapo hapo usisahau Yanga walikwenda Afrika Kusini miaka ya karibuni wakaiteketeza Kaizer Chiefs na kutwaa kombe la Toyota. Usisahau kumekuwa na wachezaji wa Afrika Kusini walioanza kuja nchini. Akina Skudu Makudubela, Rushine De Reuck, Neo Maema na wengineo. Timu zetu mbili kubwa pia zina makocha kutoka Afrika Kusini.

Lakini zaidi nadhani wameanza kusikia habari nje kuhusu maisha yetu. Sio tu pesa ipo, lakini tunaishi vizuri. Chakula kizuri. Mitaa mizuri isiyo na watu wanaotembea na bastola. Dada zetu wazuri. Sehemu nzuri za kutumia pesa zipo. Wao wapo mbele yetu lakini na sisi tumo katika orodha ya miongoni mwa nchi zenye raha Afrika.