Prime
Tanzania na fainali mbili ndani ya miaka miwili

Muktasari:
- Ndani ya miaka miwili - kati ya 2023 na 2025 timu mbili za Tanzania zimefika fainali ya mashindano ya Afrika, kitu ambacho hakuna aliyedhani kingetokea miaka miwili tu nyuma yake.
LICHA ya maumivu makali ambayo wana Simba na Watanzania kwa ujumla waliyapata mwishoni mwa juma kwa kulikosa Kombe la Shirikisho la Afrika, lakini ni dalali njema kwa mpira wetu kwamba hatuko mbali na nchi ya ahadi.
Ndani ya miaka miwili - kati ya 2023 na 2025 timu mbili za Tanzania zimefika fainali ya mashindano ya Afrika, kitu ambacho hakuna aliyedhani kingetokea miaka miwili tu nyuma yake.
Kabla ya kuuanza muongo huu wa 2020, Tanzania haikuwa tishio sana kwenye mashindano ya Afrika kutokana na kukosa mwendelezo. Kwa mfano, tangu kuanzishwa kwa hatua za makundi kwenye mashindano ya Afrika 1997, kufuzu makundi kwa timu za Tanzania lilikuwa jambo gumu sana.
Yanga 1998, Simba ikafuzu 2003...hakuna tena timu iliyofuzu hadi 2018/19 pale Simba ilipofika hadi robo fainali...hii yote ilikuwa Ligi ya Mabingwa. Japo baada ya hapo hakukuwa tena na kusubiri kwa miaka mingi, lakini bado hakukuwa na mwendelezo mzuri wa kufuzu.

Hakukuwa na hatua ya makundi kwa timu za Tanzania 2019/20, ikawepo 2020/21 kwa Simba kufika hadi robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na Namungo hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. Lakini baada ya hapo hali ikabadilika. Simba ikafika robo fainali ya Kombe la Shirikisho 2021/22, na hakukuwa tena na kurudi nyuma kuanzia hapo.
Yanga wakafika fainali ya Kombe la Shirikisho 2022/ 23 huku Simba wakifika robo fainali ya Ligi ya Ma-bingwa...na nusu fainali ya African Football League. Hatua ya makundi ikawa sio tena mafanikio kwa timu za Tanzania kwani msimu wa 2023/24 kwa mara ya kwanza timu mbili za Tanzania zikafuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa...na ilibaki kidogo Yanga ifike nusu fainali.
Japo msimu huu wa 2024/25 Yanga haikufika robo fainali, lakini ilifuzu hatua ya makundi...na Simba ndio hiyo ikacheza fainali. Hicho ni kiwango kipya ambacho timu za Tanzania zinajiwekea ikiwa na maana kwamba sasa kipimo hakitakuwa tena hatua ya makundi au robo fainali. Ni ubingwa.
TUMETOKA MBALI
Hadi tunazoea sasa kuona timu zetu zinafika fainali, kazi haikuwa rahisi na safari haikuwa fupi. Mashindano ya Afrika kwa klabu yalianza 1965, pale Klabu Bingwa Afrika ilipoanzishwa. Timu za Tanza-nia zilianza kushiriki 1968 pale Cosmopolitan ya Dar es Salaam ilipokata tiketi kufuatia ubingwa wa ligi ya 1967.

Hata hivyo, baada ya kuanza kwa sare hapa nyumbani walishindwa kwenda ugenini kwa sababu za kiuchumi. Mwaka 1969 Yanga ikashiriki baada ya kuwa mabingwa wa ligi ya 1968. Walijipanga vizuri kwa kuweka kambi nchini Romania ambako walimpata na kocha Profesa Victory Stanculescu. Wakafika robo fainali na kutolewa kwa kurusha shilingi baada ya sare ya 1-1 nyumbani na ugenini dhidi ya Asante Ko-toko ya Ghana.
Shilingi ilirushwa kwa sababu hakukuwa na sherry ya kupigiana penalti wakati huo. Timu zikitoka sare katika mechi mbili, inarushwa shilingi. Sheria ikaondolewa 1970 na kuwekwa sheria mpya ya kucheza mchezo wa tatu, kama michezo miwili ya kwanza ya nyumbani na ugenini itaisha kwa sare.

Sheria hiyo mpya ikawahukumu tena Yanga, kwani walifika tena robo fainali 1970 na kukutana tena na Asante Kotoko. Baada ya sare ya 1-1 nyumbani na ugenini, ukaja mchezo wa tatu uliopangwa kufanyika Ethiopia...Yanga ikafungwa 2-0 na kutolewa.
Mwaka 1974 ikawa zamu ya Simba iliposhiriki kwa mara ya kwanza na kufika hadi nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika.
Wakatolewa na Ghazl El Mahalla ya Misri kwa penalti 3-0 katika uwanja wa nyumbani, kufuatia kila timu kushinda 1-0 nyumbani.
Baada ya hapo hakukuwa tena na miujiza hadi 1993 pale Simba ilipofika fainali ya Kombe la CAF. Hayo yalikuwa mashindano mapya yaliyoanza 1992, na yalishirikisha timu zilizoshika nafasi ya pili kwenye ligi zao. Mwaka 1995, Malindi ya Zanzibar ikifundishwa na Salum Madadi, pia ilifika nusu fainali ya mashindano haya.
HAYA NI MAFANIKIO MAKUBWA
Ukiangalia tulikotoka na kulinganisha hali ilivyo sasa, utaona kwamba kama taifa tumepiga hatua kubwa sana. Kutoka kufuzu kwa kusuasua hadi kuzoea fainali. Haya ni mafanikio mkubwa sana. Kilichobaki sasa ni kuhakikisha kombe linakuja nchini.
Katika nchi tatu za asili za Afrika Mashariki yaani Tanzania, Kenya na Uganda wenzetu walifika mbali mapema kuliko sisi.

Kwa mfano, Gor Mahia ya Kenya ilishinda ubingwa 1987 wa Kombe la Washindi Afrika. Haya yalikuwa mashindano yaliyohusisha timu zilzishinda Kombe la FA katika chi zao. Yalianza 1975.
Villa ya Uganda ilifika fainali ya Klabu Bingwa Afrika 1991, tena ikiwatoa wawakilishi wa Tanzania, Pamba ya Mwanza kwenye raundi ya pili. Gor Mahia 1987 na Villa 1991 yalikuwa mafanikio makubwa kwa timu za Afrika Mashariki, huku Tanzania ikiachwa nyuma. Fainali ya Simba 1993 ikafungua njia kidogo, lakini hizi fainali mbili za sasa zimejenga madaraja na sasa hakuna kinachosubiriwa zaidi ya ubingwa.