Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Taifa Stars inavyopaswa kujipanga upya

STARS Pict

Muktasari:

  • Kikosi cha kocha Miguel Gamondi kina wachezaji wenye uzoefu wa kimataifa, vijana wenye vipaji na baadhi wanaocheza katika ligi za nje ya nchi, lakini changamoto kubwa ni namna ya kuunganisha uwezo wao na kuunda timu yenye ushindani dhidi ya vigogo wa Afrika.

TANZANIA 'Taifa Stars' inaelekea kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 ikiwa na nafasi ya kutumia faida ya kucheza nyumbani kufanya vizuri zaidi ya ilivyowahi kufanya katika historia yake, lakini ili kufikia hatua hiyo, Taifa Stars inahitaji kufanya kazi kubwa ndani na nje ya uwanja kabla ya mashindano hayo kuanza.

Kikosi cha kocha Miguel Gamondi kina wachezaji wenye uzoefu wa kimataifa, vijana wenye vipaji na baadhi wanaocheza katika ligi za nje ya nchi, lakini changamoto kubwa ni namna ya kuunganisha uwezo wao na kuunda timu yenye ushindani dhidi ya vigogo wa Afrika.

Ushiriki wa Tanzania katika AFCON 2025 nchini Morocco ulionyesha kuwa Stars inaweza kupiga hatua baada ya kufanikiwa kufika hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, mafanikio hayo yanahitaji kujengwa upya na si kutegemewa kama dhamana ya kufanya vizuri katika mashindano yajayo.

Hadi Novemba hii kabla ya kuivaa Nigeria, mwenendo wa timu unaonyesha bado kuna kazi kubwa. Stars ilifungwa mabao 2-0 na Guinea-Bissau katika mchezo wa kufuzu AFCON 2027, kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 na Madagascar. Matokeo hayo, licha ya kutobadilisha nafasi yake ya kushiriki fainali kwa sababu ya kuwa mwenyeji, yameonyesha baadhi ya maeneo yanayohitaji maboresho.


STAR 01

UBORA WA WACHEZAJI UPO, LAKINI ...

Ukiangalia majina yaliyopo katika kikosi cha sasa, Tanzania ina wachezaji wenye uwezo wa kuunda timu imara. Eneo la kiungo lina Feisal Salum 'Fei Toto', Himid Mao, Novatus Miroshi, Yusuph Kagoma na Charles M'Mombwa, ambao wanaweza kutoa mchanganyiko wa uzoefu, nguvu, ubunifu na uwezo wa kudhibiti mchezo.

Feisal anaweza kuwa mhimili wa kutengeneza mashambulizi na kuunganisha safu ya kiungo na washambuliaji. Himid Mao ana uzoefu wa kupambana katikati ya uwanja na kusaidia timu kupata uwiano wa kiuchezaji, huku Miroshi akiwa na faida ya kucheza soka katika mazingira ya ushindani wa nje ya nchi.

Changamoto kwa Gamondi ni kupata muunganiko sahihi wa wachezaji hao badala ya kuwategemea kwa majina yao. Timu inahitaji viungo wanaoweza kushambulia na kukaba kwa pamoja, kupunguza nafasi za wapinzani na kufanya uamuzi wa haraka inapopata mpira.

Katika safu ya ushambuliaji, Tanzania ina Simon Msuva, Kibu Denis, Clement Mzize, Selemani Mwalimu, Cyprian Kachwele na Bernard Kamungo. Hawa wana aina tofauti za uchezaji, jambo linaloweza kumpa kocha machaguo ya kutumia mifumo tofauti kulingana na mpinzani.

Kamungo ni miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuleta tofauti kutokana na kasi, uwezo wa kucheza pembeni na kutengeneza nafasi. Akiwa na FC Dallas nchini Marekani, alifikisha mechi 23 na dakika 1,703 katika msimu wa 2026, akitoa pasi sita za mabao, rekodi iliyokuwa bora kwake tangu aanze kucheza katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo.

Msuva ana uzoefu mkubwa wa kimataifa na uwezo wa kucheza katika maeneo ya ushambuliaji, huku Kibu akiwa na nguvu na uwezo wa kucheza katika nafasi za pembeni. Kwa upande wa Mzize na Kachwele, wanahitaji kupewa nafasi ya kuendelea kukua na kuonyesha uwezo wao katika mechi zenye ushindani mkubwa.

Hata hivyo, tatizo kubwa lililoonekana katika michezo ya hivi karibuni ni matumizi ya nafasi za kufunga. Katika mchezo dhidi ya Guinea-Bissau, Stars ilipata nafasi lakini ikashindwa kuzitumia, jambo ambalo hata Gamondi alilikiri kuwa moja ya matatizo makubwa ya timu yake.

Hapa ndipo benchi la ufundi linapaswa kuongeza kazi ya ufundishaji wa washambuliaji, kuanzia umaliziaji wa nafasi, kufanya uamuzi ndani ya eneo la hatari hadi kujenga mashambulizi yanayoweza kumweka mfungaji katika nafasi nzuri.

Tanzania inahitaji kuwa na washambuliaji wenye uwezo wa kutekeleza majukumu tofauti badala ya kumtegemea mchezaji mmoja. Hilo litasaidia kupunguza tatizo la timu kukosa makali pale mshambuliaji wake mkuu anapokosa nafasi ya kucheza au anapozuiwa na mabeki wa wapinzani.


STAR 02

SAFU YA ULINZI INAHITAJI UIMARA ZAIDI

Katika safu ya ulinzi, Taifa Stars ina wachezaji kama Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Ibrahim Abdulla, Haji Mnoga, Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Mohamed Hussein na Nathaniel Chilambo.

Mwamnyeto ana uzoefu wa kucheza mechi kubwa ndani na nje ya nchi, huku Mnoga akiwa na uzoefu wa soka la nje. Dickson Job na Ibrahim Abdulla 'Bacca', pia ni miongoni mwa wachezaji wanaoweza kusaidia kujenga safu yenye ushindani.

Hata hivyo, jambo muhimu ni kujenga maelewano kati ya mabeki wa kati, mabeki wa pembeni na viungo wa ulinzi. Katika mashindano kama AFCON, timu zinazokosa mawasiliano na nidhamu ya kujilinda hujikuta zikitoa nafasi rahisi kwa wapinzani wenye washambuliaji wenye kasi na uwezo wa kutumia makosa.

Gamondi anapaswa kuhakikisha Stars inakuwa na mpangilio mzuri wa kujilinda, hasa inapopoteza mpira wakati wa kushambulia. Aidha, ni muhimu kufanya kazi kwenye mipira ya adhabu na kona, kwa kuwa maeneo hayo yanaweza kuamua matokeo ya mechi ngumu.


STAR 03

MAKIPA NA USHINDANI WA NAFASI

Eneo la makipa pia linahitaji maandalizi ya kutosha. Aishi Manula, Zuberi Foba na Abdallah Hamisi ni miongoni mwa makipa walioitwa katika kikosi cha Novemba.

Ushindani wao unapaswa kujengwa kwa kuzingatia kiwango cha sasa, uwezo wa kuokoa mashuti, kucheza kwa miguu na kuongoza safu ya ulinzi. Kipa katika mashindano makubwa hapimwi kwa kuokoa mipira pekee, bali pia namna anavyowasiliana na mabeki na kuanzisha mashambulizi kwa usahihi.

Benchi la ufundi linahitaji kufanya tathmini ya kina ili kupata kipa namba moja mapema, bila kuzuia ushindani wa makipa wengine wanaoweza kupewa nafasi kulingana na kiwango chao.


STAR 05

GAMONDI AWE NA MFUMO UNAOTAMBULIKA

Changamoto nyingine kubwa kwa Taifa Stars ni kujenga utambulisho wa kiuchezaji. Timu inapaswa kuwa na mfumo unaotambulika, iwe inakutana na wapinzani wanaomiliki mpira au wanaocheza kwa kujilinda na kusubiri mashambulizi ya kushtukiza.

Gamondi anahitaji kuamua aina ya soka analotaka Stars icheze na kuhakikisha wachezaji wanazoea mfumo huo kupitia mazoezi na mechi za ushindani.

Si lazima Tanzania icheze kwa kushambulia muda wote, hasa inapokutana na timu zenye wachezaji wenye viwango vya juu. Muhimu ni kuwa na uwezo wa kubadilisha mbinu kulingana na mazingira ya mchezo, huku ikidumisha nidhamu ya kiufundi.

Pia, kocha anapaswa kupunguza mabadiliko yasiyo ya lazima katika kikosi cha kwanza ili kujenga maelewano. Wachezaji wanapokuwa na muda wa kucheza pamoja, hujenga uelewano wa kiuchezaji unaosaidia timu kufanya maamuzi kwa haraka.


STAR 04

MECHI ZA KIMATAIFA ZITUMIKE KWA MAANDALIZI

Tanzania ina faida ya kuwa mwenyeji wa AFCON 2027 pamoja na Kenya na Uganda, hivyo tayari imepata nafasi ya kushiriki fainali hizo. Hata hivyo, mechi za kufuzu zinazoendelea zinapaswa kutumiwa kama sehemu ya maandalizi ya kweli.

Mechi dhidi ya Nigeria zilizopangwa Novemba 13 na 17, 2026 ni miongoni mwa vipimo muhimu kwa Stars. Michezo hiyo inaweza kuonyesha kiwango cha timu dhidi ya mpinzani mwenye uzoefu na historia kubwa katika soka la Afrika.

Baada ya hapo, TFF na benchi la ufundi zinapaswa kupanga mechi za kirafiki dhidi ya mataifa yenye mitindo tofauti ya uchezaji, ikiwemo timu zinazomiliki mpira vizuri, zinazoshambulia kwa kasi na zenye nguvu katika mipira ya juu.

Mechi hizo zitasaidia kubaini mapungufu kabla ya mashindano kuanza badala ya kuyasubiri yaonekane wakati wa fainali.


STAR 06

WACHEZAJI WA NJE WASAIDIWE KUUNGANA NA WA NDANI

Uwepo wa wachezaji wanaocheza nje ya Tanzania kama Kamungo, Novatus Miroshi, Msuva, Haji Mnoga, Alphonse Mabula, Tarryn Allarakhia na Ben Starkie, ni fursa ambayo benchi la ufundi linapaswa kuitumia vizuri.

Wachezaji hao wanakutana na mazingira tofauti ya soka, mifumo mbalimbali ya ufundishaji na viwango tofauti vya ushindani. Hata hivyo, kucheza nje ya nchi pekee hakumaanishi mchezaji anastahili nafasi ya moja kwa moja katika kikosi cha kwanza.

Gamondi anapaswa kuangalia kiwango cha kila mchezaji, nafasi anayocheza katika klabu yake na namna anavyoweza kuendana na mahitaji ya timu ya taifa.

Wakati huohuo, TFF inahitaji kuweka utaratibu wa kufuatilia maendeleo ya wachezaji wote wanaoweza kuiwakilisha Tanzania, ili benchi la ufundi liwe na machaguo mapana na yenye ushindani.


STAR 07

WASISAHAU MASHABIKI, FAIDA YA UENYEJI

Kucheza nyumbani ni faida kubwa kwa Tanzania, lakini haitoshi peke yake kuhakikisha mafanikio. Stars inahitaji kujenga timu itakayoweza kutumia nguvu ya mashabiki bila kubebwa na presha ya kutaka kushinda kila mchezo.

Mashabiki wanatarajia kuona timu inayopambana, yenye nidhamu na inayocheza kwa kujiamini. Hivyo, maandalizi ya kisaikolojia ni muhimu kama yalivyo mazoezi ya kiufundi na kiungozi.

Kwa upande mwingine, Serikali, TFF na wadau wa soka wanapaswa kuhakikisha timu inapata mazingira bora ya maandalizi, ikiwemo vifaa, huduma za afya, lishe, uchambuzi wa wapinzani na ratiba inayowaruhusu wachezaji kujiandaa vizuri.


STAR 08

LENGO LIWE ZAIDI YA KUSHIRIKI

Kwa kuangalia aina ya wachezaji waliopo, Taifa Stars ina msingi wa kuunda kikosi chenye ushindani zaidi kuliko kinachoweza kuonekana kupitia baadhi ya matokeo ya hivi karibuni. Lakini msingi huo unahitaji kujengwa kwa mpango, uthabiti na uwajibikaji.

AFCON 2027 inapaswa kuwa zaidi ya fursa ya Tanzania kuandaa mashindano makubwa. Inapaswa kuwa nafasi ya Taifa Stars kuthibitisha kuwa maendeleo ya soka nchini yanaweza kuzaa matokeo ndani ya uwanja.

Lengo halipaswi kuwa kushiriki tu kwa sababu ya uenyeji, bali kujenga timu inayoweza kushindana, kufuzu hatua za mtoano na kujaribu kuvuka mafanikio ya kihistoria ya kufika 16 bora katika AFCON iliyopita.