AFCON 2027; Mambo matano yanayoweza kuiingizia Tanzania mabilioni
Muktasari:
- Tanzania, Kenya na Uganda zitakuwa wenyeji wa mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika Juni 19 hadi Julai 17, 2027.
FAINALI za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, zinaweza kufungua milango ya neema kwa wenyeji, ikiwemo Tanzania ambayo inaendelea na mikakati yake kababe ya maandalizi, ikiwa imesalia miezi michache kabla ya michuano hiyo kupigwa kwa mara ya kwanza Afrika Mashariki.
Tanzania, Kenya na Uganda zitakuwa wenyeji wa mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika Juni 19 hadi Julai 17, 2027.
Kwa upande wa Tanzania, maandalizi yanahusisha viwanja vya Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, Arusha na Fumba, Zanzibar, pamoja na viwanja vya mazoezi, hoteli, barabara na huduma nyingine muhimu kwa timu na mashabiki.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iliyoripotiwa na Septemba 24, 2026, Serikali ilikuwa imetumia Sh104 bilioni, zikiwemo Sh74 bilioni kwa ajili ya haki ya kuandaa mashindano hayo na Sh30 bilioni kwa haki za matangazo.
Wakati fedha hizo na uwekezaji mwingine ukiendelea kuelekezwa katika maandalizi, swali muhimu ni namna Tanzania itakavyobadilisha fursa hiyo kuwa manufaa ya kiuchumi kwa wananchi wake, badala ya kuishia kuwa mwenyeji wa mechi kwa muda wa wiki chache.
Uzoefu wa nchi nyingine unaonyesha mashindano makubwa yanaweza kuchochea shughuli za kiuchumi, lakini manufaa ya muda mrefu hayaji yenyewe. Yanahitaji mipango inayounganisha utalii, biashara, ajira, miundombinu na uwekezaji binafsi.
MAPATO YA UTALII
Moja ya fursa kubwa zinazoweza kupatikana AFCON 2027 ni kuongezeka kwa wageni wanaotembelea Tanzania, kutumia huduma za hoteli, kusafiri na kutembelea vivutio vya utalii.
Mashabiki watakaokuja nchini kushuhudia mechi wanaweza kutumia fedha katika malazi, chakula, usafiri, matembezi na ununuzi wa bidhaa mbalimbali. Ikiwa sehemu ya wageni hao watatumia muda wao kutembelea vivutio vya utalii, mapato yanaweza kusambaa katika maeneo mengi zaidi ya miji itakayokuwa mwenyeji wa mechi.
Kwa mfano, shabiki anayekuja Dar es Salaam kwa ajili ya mechi, anaweza kuongeza siku za kukaa nchini ili kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Serengeti au Mlima Kilimanjaro, kutegemea muda wake na gharama za safari. Vivyo hivyo, wageni wanaotembelea Zanzibar wanaweza kutumia huduma za hoteli, mikahawa, waongoza watalii na watoa huduma za matembezi ya baharini.
Takwimu za Tanzania zinaonyesha sekta ya utalii tayari ina mchango mkubwa katika uchumi. Kwa mujibu wa Ripoti ya Utafiti wa Sekta ya Utalii ya mwaka 2025 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na taasisi nyingine, Tanzania ilipokea watalii wa kimataifa 2,294,495 mwaka 2025, kutoka 2,141,895 mwaka 2024. Mapato ya utalii yalifikia Dola 4.41 bilioni mwaka 2025, kutoka Dola 3.90 bilioni mwaka uliotangulia.
Takwimu hizo zinaonyesha ukubwa wa sekta ambayo AFCON inaweza kusaidia kuitangaza zaidi. Hata hivyo, ongezeko lolote la wageni au mapato litakalohusishwa na mashindano hayo linapaswa kupimwa baada ya mashindano, badala ya kudhaniwa mapema.
Uzoefu wa Ivory Coast, mwenyeji wa AFCON 2023, unatoa mfano mwingine. Ripoti ya CAF ya mwaka 2023/24, ikinukuu tathmini ya Nielsen, ilikadiria kuwa mashindano hayo yalikuwa na athari chanya ya takribani Dola 1.5 bilioni katika uchumi wa nchi hiyo.
Hiyo ni athari iliyokadiriwa na ripoti, si lazima iwe fedha zote zilizoingia moja kwa moja katika akaunti za Serikali. Hata hivyo, inaonyesha namna matumizi ya wageni na shughuli zinazochochewa na mashindano yanavyoweza kuhusishwa na uchumi mpana.
Kwa Tanzania, faida kubwa itapatikana iwapo wageni watavutwa kutumia huduma nyingi za ndani na sehemu yao itarudi kutembelea nchi hata baada ya AFCON kumalizika.
KUONGEZA AJIRA
Maandalizi na uendeshaji wa mashindano makubwa huhitaji nguvu kazi katika sekta mbalimbali. Ujenzi na ukarabati wa viwanja, hoteli, barabara na maeneo ya mazoezi huongeza mahitaji ya mafundi, wahandisi, madereva, walinzi na wafanyakazi wengine.
Wakati wa mashindano, hoteli na mikahawa huhitaji wahudumu, wapishi, wasafishaji na wafanyakazi wa mapokezi. Usafiri huhitaji madereva na waongoza watalii, huku kampuni za matangazo, vyombo vya habari na waandaaji wa matukio zikihitaji wataalamu na wafanyakazi wa muda.
Fursa hizo zinaweza kuwanufaisha vijana, wajasiriamali wadogo na kampuni za ndani, lakini ni muhimu kutofautisha ajira za muda mfupi na zile zitakazoendelea baada ya mashindano.
Wakati wa Kombe la Dunia la 2010 Afrika Kusini. Tathmini iliyotolewa na Serikali ya nchi hiyo Julai 2010 ilieleza uwekezaji wa Rand 11.7 bilioni katika viwanja vipya sita na ukarabati wa viwanja vingine vinne ulihusishwa na ajira 66,000 za ujenzi na mishahara yenye thamani ya Rand 7.4 bilioni.
Tanzania inaweza kuongeza manufaa kwa kuweka utaratibu unaowezesha kampuni za ndani kushiriki katika zabuni za huduma na bidhaa zinazohitajika. Wajasiriamali wanaweza kuuza mavazi, zawadi za utalii, vyakula na bidhaa zenye utambulisho wa Tanzania.
Hata hivyo, ili fursa hizo ziwanufaishe wananchi wengi, ni muhimu kufuatilia idadi ya ajira zilizotengenezwa, sehemu ya zabuni zilizoenda kwa kampuni za ndani na kiwango cha bidhaa zinazozalishwa nchini zilizotumika.
SOKO LA WAKULIMA
Wageni wanapoongezeka, mahitaji ya chakula, vinywaji visivyo na kilevi, bidhaa za usafi na vifaa vya matumizi ya kila siku nayo huongezeka. Hali hiyo inaweza kuipa sekta ya kilimo na ufugaji soko la uhakika zaidi, hasa iwapo hoteli, mikahawa na kampuni za upishi zitanunua bidhaa kutoka kwa wazalishaji wa ndani.
Kwa mfano, hoteli inayopokea mashabiki wa soka itahitaji nyama, samaki, mayai, maziwa, mboga za majani, matunda na nafaka. Ikiwa itakuwa na mikataba na wakulima na wafugaji wa Tanzania, sehemu ya fedha zinazotumiwa na wageni inaweza kuingia moja kwa moja kwa wazalishaji hao.
Fursa hiyo haipaswi kuishia katika hoteli kubwa pekee. Vikundi vya wakulima, vyama vya ushirika, wazalishaji wa asali, wajasiriamali wa vyakula na kampuni ndogo za usindikaji vinaweza kuunganishwa na minyororo ya ugavi ya taasisi zitakazohudumia mashindano.
Ili mfumo huo ufanye kazi, wazalishaji wanahitaji kukidhi viwango vya ubora, usafi, kiasi na muda wa kuwasilisha bidhaa. Serikali na sekta binafsi zinaweza kusaidia kutokana na mafunzo, mikataba ya ununuzi na mifumo inayowaunganisha wazalishaji na wanunuzi.
Kipimo muhimu hakitakuwa tu idadi ya wageni waliofika, bali pia kiasi cha bidhaa zilizonunuliwa kutoka kwa wazalishaji wa ndani na mapato yaliyowafikia wakulima, wafugaji na biashara ndogo.
KUIMARISHA MIUNDOMBINU
AFCON inahitaji miundombinu inayoweza kuhudumia timu na mashabiki kwa viwango vinavyokubalika kimataifa. Hii inahusisha viwanja, barabara, usafiri, hoteli, huduma za afya, mawasiliano na mifumo ya usalama.
Ingawa uwekezaji huo unahitaji fedha nyingi, unaweza kuwa na manufaa ya muda mrefu iwapo miundombinu itatumika vizuri baada ya mashindano.
Barabara iliyoboreshwa ili kurahisisha safari za mashabiki inaweza baadaye kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuwafikia watalii. Hoteli mpya inaweza kuendelea kupokea wageni wa kawaida na washiriki wa mikutano, huku viwanja vikitumika kwa ligi za ndani, mashindano ya kimataifa na matukio mengine.
Hata uwekezaji unaoendelea katika maeneo ya utalii unaweza kuhusishwa na fursa hiyo. Oktoba 2026, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji alikagua miradi ya kuboresha miundombinu katika Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia wa Pugu Kazi Mzumbwi, Kisarawe.
Kwa mujibu wa taarifa ya ziara hiyo, Sh2.2 bilioni zilitolewa kwa miradi ya hifadhi hiyo, huku TFS ikitakiwa kukamilisha kazi hizo kwa muda uliopangwa.
Miundombinu ya aina hiyo inaweza kuongeza chaguo za mapumziko na utalii kwa wageni watakaokuja nchini. Lakini manufaa yake hayatapimwa kwa kukamilika kwa ujenzi pekee. Yanahitaji pia kuangalia idadi ya wageni wanaotumia huduma hizo, mapato yanayozalishwa, gharama za uendeshaji na uwezo wa miundombinu kujihudumia kifedha kwa muda mrefu.
Uzoefu wa Afrika Kusini unaonyesha umuhimu wa kuangalia matumizi ya miundombinu baada ya mashindano. Serikali ya nchi hiyo iliripoti kuwa maandalizi ya Kombe la Dunia yalihusisha maboresho ya barabara, reli, viwanja vya ndege na mifumo ya usafiri wa umma, ikiwemo mfumo wa mabasi yaendayo haraka wa Rea Vaya jijini Johannesburg.
Kwa Tanzania, somo ni kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa kuelekea AFCON inatatua mahitaji halisi ya wananchi na biashara hata baada ya mashindano kumalizika.
TANZANIA KUJITANGAZA
AFCON itaiweka Tanzania mbele ya watazamaji wa televisheni, watumiaji wa mitandao ya kijamii, wadau wa michezo na wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali. Fursa hiyo inaweza kutumika kutangaza vivutio vya utalii, fursa za biashara na uwezo wa nchi kuandaa matukio makubwa.
Kwa mfano, matangazo ya mashindano yanayoonyesha Dar es Salaam, Zanzibar na Arusha yanaweza kuwafanya baadhi ya watazamaji kutaka kutembelea maeneo hayo. Wafanyabiashara wanaofika nchini kwa ajili ya mashindano wanaweza pia kupata fursa za kukutana na wawekezaji, kampuni za usafiri, hoteli na watoa huduma wengine.
Ivory Coast ilipata mwonekano mkubwa wa kimataifa kupitia AFCON 2023. Katika takwimu zilizojumuishwa kwenye ripoti ya CAF, asilimia 98 ya waliohojiwa walisema mashindano hayo yalikuwa na athari chanya katika taswira ya nchi, huku asilimia 97 wakisema yalisaidia kuitangaza Ivory Coast kama kivutio cha utalii.
Hata hivyo, maoni hayo ya waliohojiwa hayamaanishi kiasi sawa cha uwekezaji mpya kilimiminika nchini humo. Kutangaza nchi ni hatua moja; kuvutia uwekezaji kunahitaji mazingira mazuri ya biashara, huduma bora, utulivu na sera zinazoeleweka.
Tanzania inaweza kutumia fainali za AFCON kuandaa maonesho ya bidhaa za ndani, mikutano ya wawekezaji na kampeni za utalii zinazowalenga wageni wanaofika nchini. Kampeni hizo zinapaswa kuendelea hata baada ya mashindano ili kugeuza mwonekano wa muda mfupi kuwa mahitaji ya kudumu.