Kifo cha Amapiano Bongo kimekaribia!
Muktasari:
- Mastaa kama Marioo, Harmonize, Diamond Platnumz, Jux, Rayvanny, Mbosso, Zuchu, Lava Lava, Nandy, Whozu na Alikiba ambao walitamba na ngoma za Amapiano, sasa wamepunguza mwendo.
Nyimbo mpya za wasanii wengi wakubwa wa Bongo Fleva zinazotoka kwa sasa, utabaini zama za Amapiano zinaelekea ukingoni baada ya kutamba kwa takriban miaka mitano hivi.
Mastaa kama Marioo, Harmonize, Diamond Platnumz, Jux, Rayvanny, Mbosso, Zuchu, Lava Lava, Nandy, Whozu na Alikiba ambao walitamba na ngoma za Amapiano, sasa wamepunguza mwendo.
Hata nyimbo chache za Amapiano zinazotoka kwa sasa hazipati kuvuma sana kama ilivyokuwa kati ya mwaka 2020 hadi 2024, ni kama mashabiki wameanza kukinai au kuchoka aina hiyo ya muziki.
Inatajwa sababu ya muziki huo kuchokwa ni wasanii kutokuja na kitu kipya cha tofauti na kile ambacho tayari kimeshafanyika awali, huku baadhi ya tungo nyingi zikiwa na masihara mengi ndani yake.
Muziki wa Amapiano ulianza mnamo 2012 huko Gauteng, Afrika Kusini ingawa kumekuwa na utata ni wapi hasa asili ya muziki huo nchini humo, wapo wanaodai ulianzia katika vitongoji vya Johannesburg - Soweto na kisha kusambaa barani Afrika.
Utakumbuka wasanii wa mwanzo wa Bongofleva kufanya vizuri na Amapiano ni Damian Soul - Mapopo (2020), Marioo - Mama Amina (2020), Ommy Dimpoz - Dede (2020), Harmonize - Mang’dakiwe Remix (2021) na Diamond - IYO (2021).
Baadaye mastaa wengine nao walijaribu kuwapa mashabiki wao ladha hiyo, kati ya hao kuna Chino Kidd, Abigail Chams, Billnass, Mimi Mars, Phina, G Nako, Ruby, Rosa Ree na Jux.
Jux ni kati waimbaji wa Bongo Fleva walionufaika sana na Amapiano, mathalani wimbo wake kwanza na wa pekee hadi sasa kwa video yake kutazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube, ni ya ngoma yake ya Amapiano, Enjoy (2023) akimshirikisha Diamond.
Vilevile ilishinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2023 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana, ikiwa ni msimu wa pili mfululizo kwa wimbo wa Amapiano kushinda kipengele hicho baada ule wa Rayvanny akishirikiana na Diamond pia, Nitongoze (2022).
Mbali na Jux, staa mwingine wa Bongo Fleva aliyefanya vizuri na ngoma yake ya Amapiano, ni Diamond ambaye wimbo wake, Komasava (2024) uliweka rekodi kwa kuwa wa kwanza Afrika Mashariki kuingia chati ya Billboard U.S Afrobeats Songs.
Wimbo huo aliowashirikisha Khalil Harisson na Chley wa Afrika Kusini pamoja na Jason Derulo kutokea Marekani, ulimtangaza sana Diamond kimataifa, mathalani aliutumbuiza katika tuzo za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) 2024 zilizofanyika Morocco.
Hata hivyo, kwa sasa wanamuziki wengi wa Bongo Fleva wamerejea katika muziki wao wa nyumbani uliozoeleka na mashabiki wao kwa miaka mingi, hii ni ishara kuwa Amapiano inaenda ikitoweka polepole.
Marioo ambaye alivuma na kusifika kwa kuachia ngoma kali za Amapiano, naye sasa anaelekea kuyahana mahadhi hayo, katika Extended Playlist (EP) yake mpya, MMMCXII (2026) yenye nyimbo tisa, ni mmoja tu ndio wa Amapiano.
Kwa upande wake Harmonize ambaye alikuja na ngoma nyingi za Amapiano hadi kufikia hatua ya kulalamikiwa na baadhi ya mashabiki, yeye ndio ameachana kabisa aina hiyo ya muziki, ni muda mrefu sasa hajaachia Amapiano.
Si Harmonize tu, mastaa wengine kama Whozu, Nandy, Rayvanny, Jux na Mbosso, wana takribani mwaka mmoja bila kuachia ngoma za Amapiano, kitu ambacho ni tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Kama ambavyo Kwaito ilikuja na kuvuma kisha kupotea kabisa ndani ya Bongo Fleva, ndivyo ambavyo na Amapiano inavyoenda kuwa kwani dalili tayari zipo.
Damian Soul ambaye ndiye msanii wa kwanza Bongo kuvuma na Amapiano kupitia ngoma yake, Mapopo (2020), amesema yeyote mwenye uelewa na uwezo bado anaweza kufanya aina hiyo ya muziki ingawa haiwakilishi Tanzania.
“Amapiano ni muziki wa kitamaduni Afrika Kusini ukichanganyika na House Music, sisi hapa pia tunaweza kufanya japokuwa si muziki wetu kwa maana ya Tanzania, lakini Kiafrika kama nina maarifa ya muziki kwanini nisifanye?,” amesema.
Mnamo Juni 2023 waandaji wa tuzo za Grammy Marekani, Recording Academy walianzisha kipengele cha ‘Best African Music Perfomance’ ambacho ni maalum kwa ajili ya aina mbalimbali za muziki kutokea Afrika ikiwemo Bongo Fleva na Amapiano.
Mwimbaji kutokea Afrika Kusini, Tyla akaweka rekodi kama msanii wa kwanza kushinda kipengele hicho 2024 kupitia wimbo wake wa Amapiano, Water (2023) akiwabwaga wakali kibao akiwemo Davido ambaye aliwania pia na wimbo wa Amapiano, Unavailable (2023).