Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jinsi Kombe la Dunia 2026 lilivyoacha ramani ya AFCON 2027

ZENGWE Pict


Fainali za Kombe la Dunia zimeisha Jumapili iliyopita wakati Hispania ilipotwaa kombe kwa kuifunga Argentina katika mechi ya kusisimua ya mwisho iliyofanyika New Jersey, Marekani.


Fainali hizo zilizoshirikisha mataifa 48 ziliandaliwa kwa pamoja na Marekani, Canada na Mexico zilizo Amerika ya Kaskazini, ambako ukiondoa Mexico, mchezo wa mpira wa miguu bado haujaweza kuteka mioyo ya wananchi wengi.


Pamoja na yote fainali hizo zimekuwa na mafanikio makubwa ndani na nje ya uwanja, kiuchumo, kijamii na mambo mengine ukilinganisha na fainali za Qatar.

Watu milioni 6.8 wanakadiriwa kuingia viwanjani kuangalia mechi 104 zilizochezwa katika miji 16, hiyo ikiwa ni rekodi mpya iliyovunja rekodi ya awali ya watu milioni 3.5 iliyowekwa mwaka 1994 wakati fainali hizo zilipofanyika Marekani zikishirikisha mataifa 32 na mechi 52, huku baadhi ya mashabiki wakisafiri kutoka nchi moja hadi mwingine na timu kama Iran ikilazimika kuishi kwenye mji wa mpakani nchini Mexico lakini ikicheza mechi Marekani kutokana na matatizo ya kisiasa.

ZENG 01

Walioteseka licha ya kupata burudani safi walikuwa ni mashabiki ambao walikutana na viingilio vya juu vilivyofikia hadi dola 33,000 (takriban sh. milioni 70 za Kitanzania) kwa mechi ya fainali, huku usafiri wa ndani kwenda viwanjani ukifikia hadi dola 150,000 (zaidi ya Sh.300,000 za Kitanzania) kwa waliokuwa wanakwenda uwanja kama Metlife.

Bei za bidhaa kama jezi na vyakula nazo zilikuwa juu kutokana na kipindi hicho kugeuka kama msimu mzuri wa utalii kutokana na maelfu ya watu kuingia kwenye nchi hizo tatu kutoka kila pembe ya dunia.

Makadirio ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) yalikuwa kwamba fainali hizo zingeingiza zaidi ya dola bilioni 41 za Kimarekani, huku bilioni 17 zikibakia nchini Marekani ambako mechi nyingi za fainali hizo zilichezwa.

ZENG 02

Ndani ya uwanja nako kulikuwa na ushindani uliotoa burudani bora kwa watu waliokuwa ndani ya nchi hizo tatu na sisi huku tuliokuwa tukishuhudia kupitia runinga na mitandao.

Sherehe za ufunguzi na za kufunga zilishereheshwa vizuri na wasanii mbalimbali, zikichanganya utamaduni mbalimbali na hivyo kuwa za aina yake kuwahi kutokea.

Ni fainali ambazo hazikuwa na Kamati za Maandalizi za nchi (LOC) kama ulivyo utamaduni wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) na badala yake shirikisho hilo lilifanya kazi na taasisi za nchi wenyeji kama Kikosi Maalum cha Ikulu (White House Task Force) na kama za nchi za Marekani, Canada na Mexico.

Kamati hizo za nchi zilikuwa na majukumu ya uendeshaji, kuhamasisha mashabiki na miradi ya ukumbusho wa fainali hizo, yaani miradi ya kunufaisha nchi, mpira a miguu au uchumi ambayo itawafanya watu waone umuhimu wa fainali hizo hata miaka mingi ijayo.

ZENG 03

Bila shaka, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) litachukua mfumo huo wa maandalizi kuelekea fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika nchini Tanzania, Kenya na Uganda. Kwa majaribio kwamba tunaweza kumudu fainali hizo, CAF ilitupa uenyeji wa fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zilizofanyika mwaka jana.

Kwa upande wa hamasa, Kenya ilionekana kuongoza kutokana na mashabiki kufurika viwanjani hata pale timu yao ya taifa ilipoondolewa, huku Tanzania na Uganda zikisuasua.

Na jitihada za kujenga hamasa hiyo hazionekani, huku timu ya taifa ikiwa inaendelea kupoteza mvuto licha ya kuwa na mafanikio makubwa katika miaka ya karibuni baada ya kufuzu kucheza fainali hizo mara mbili ndani ya miaka michache.

ZENG 04

Kwa mfumo huo, kamati za maandalizi za nchi ndizo zinatakiwa zifanye kazi hiyo ya hamasa kwa mashabiki wa ndani, huku taasisi nyingine kama Bodi ya Utalii zikifanya jitihada za kuitangaza zaidi nchi kama kisiwa cha amani ili wananchi wa mataifa mengine waone ni salama kuja Tanzania kuangalia fainali hizo badala ya kutangaza mbuga pekee.

Ingawa kumekuwa na jitihada za kuboresha mtandao wa barabara kote nchini, bado usafiri wa ndani ya miji umekuwa tatizo, hasa usafiri wa umma ma badala yake huduma hiyo imetekwa na pikipiki za matairi mawili (bodaboda) na matatu (maarufu kama Bajaj) ambazo zimekuwa kero barabarani.

Majiji ya Dar ambalo lina uwanja wa Benjamin Mkapa unaotegemewa kutumiwa kwa mechi muhimu kama za ufunguzi au ufungaji, na Arusha, ambako kuna uwanja mpya wa kisasa, yanaongoza kwa kero za bodaboda na Bajaj, ingawa usafiri wa mwendokasi (DART) unaendelea kukamilishwa maeneo tofauti.

Nidhamu ya sheria za barabarani haipaswi kusubiri kukaribia kwa mashindano, bali inatakiwa ianze kujengwa sasa ili igeuka utamaduni na hivyo kusafisha mazingira ya AFCON 2027 mapema.

ZENG 05

Kauli ya m wenyekiti wa chama cha wamiliki wa hoteli kwamba hakuwa na taarifa za ujio wa AFCON pia inaonyesha ni kiasi gani hakuna utayari sahihi. Haya mambo yapaswa kuanza kushughulikiwa mapema.

Taarifa za idadi ya watu watakaofanya kazi za kujitolea (volunteers) wakati wa fainali hizo zinapaswa kuanza kutolewa mapema ili zichakatwe na hatimaye ipatikane njia nzuri ya kuwapata.

Ni kumbukumbu gani tunadhani AFCON 2027 itaacha. Wamarekani walianzisha Ligi Kuu ya Soka (MLS) mwaka 1999 baada ya kuandaa kwa mafanikio fainali za mwaka 1994. Kwa hiyo mafanikio ya fainali za mwaka huu yamejengwa juu ya mafanikio ya fainali za kwanza kwao.

Marekani, Canada na Mexico haikufanikiwa kwa maandalizi ya dakika za mwisho, bali kuanza mapema kushughulikia mambo ya msingi na hivyo kuwa na kazi nyepesi mwishoni.

Tunahitaji kujifunza kutoka kwa nchi hizo tatu ili tuwe na fainali bora za AFCON 2027 na zikiondoka tuone kuna kitu tumekipata ambacho kilitusukuma tuombe uenyeji wa fainali hizo.

Swali linakuja kwamba tumejifunza lolote kutoka Mexico, Canada na Marekani?