Siri ya mastaa kuvaa sweta zenye kofia
Muktasari:
- Ili kuutafuta ukweli Mwanaspoti limefanya mahojiano na baadhi ya mastaa nchini kujua kuna siri gani ya wao au baadhi ya nyota wa burudani na muziki kuvaa masweta hasa wanapokuwa wanajitokeza kwenye macho ya watu wengi.
JE umewahi kujiuliza kuna uhusiano gani kati ya masweta yenye kofia na mastaa mbalimbali duniani? Na je unapokutana na picha zao ama kukutana nao laibu wamevaa hivyo ni picha gani inakujia kichwani?
Ili kuutafuta ukweli Mwanaspoti limefanya mahojiano na baadhi ya mastaa nchini kujua kuna siri gani ya wao au baadhi ya nyota wa burudani na muziki kuvaa masweta hasa wanapokuwa wanajitokeza kwenye macho ya watu wengi.
Kihistoria inaonyesha walikuwepo ndugu wawili Abraham (Abe) Feinbloom na William (Bill) Feinbloom kutoka Rochester, New York, Marekani, ambapo 1934 Abe baada ya kutembelea Michigan, alianzisha ushirikiano na duka la vifaa vya michezo la Moe’s Sport ili kuuza masweta yenye kofia maarufu Kimombo kama hoodies, masweta ya kawaida wanayoyaita sweatshirts na fulana zilizokuwa na nembo ya Chuo Kikuu cha Michigan.
Tangu miaka hiyo imekuwa ni mitindo ya kisasa kwa mastaa mbalimbali duniani kuvaa masweta ya kofia wanapokuwa stejini wakati mwingine viwanja vya ndege, na baadhi yao ni msanii Chris Brown kutoka Tappahannock, Virginia, Marekani na A$AP Rocky ambaye licha ya kufanya muziki pia anafahamika kama mwanamitindo.
Na Kibongobongo ni kawaida kumuona Diamond Platnumz, Tundaman hao ni baadhi kwa wanamuziki kwa wanasoka, kipa wa Yanga, Djigui Diarra, beki Hussein Kazi (Singida Black Stars) na wengine wengi.
Mwanaspoti limefanya mahojiano na baadhi ya mastaa wa soka na muziki, ambao wamefichua sababu za kuvaa masweta ya kofia pindi wanapoonekana viwanja vya ndege na wanapotokea kwenye umati wa watu.
Nahodha wa Yanga, Dickson Job kwa upande wake anasema, anapovaa sweta lenye kofia anajisikia kuwa huru, kuna wakati anakuwa anafunika kichwa hasa anapokuwa anafika kwenye macho ya watu wengi.
“Lakini mbele ya watu wengi inasaidia kujificha na macho yao, wakati mwingine wanakuwa wameshitukia umeishafika mbali, ndiyo maana ukiwa na sweta lenye kofia ni rahisi kutoa kofia na kuivaa,” anasema Job anayependa mitindo na anasisitiza anajisanifu mwenyewe.
Msanii mkongwe wa Bongofleva, maarufu kama Ferooz anasema kuna sababu nyingi za wao kuvaa sweta za kofia, mojawapo ikitaja hali ya hewa, fasheni namna ya kutokea kwenye macho ya jamii.
“Wakati mwingine tunakwenda mikoa yenye baridi kali,kwenye ndege au basi baridi inakuwepo, tunafanya shoo usiku ambao hali ya hewa inakuwa ya baridi, jambo lingine ukijitokeza mbele ya watu wengi, unapofunika kichwa kwa kepu au sweta lenye kofia au mwingine akivaa mawani anaona anajisikia vizuri, lakini wengine wanapenda kuonekana zaidi Kihip Hop,” anasema Ferooz.
Aliyewahi kuwa mshambuliaji wa Azam FC na Yanga, Prince Dube ambaye anachezea Hardrock ya nchini kwao Zimbabwe, kabla ya kuondoka nchini anasema :”Nikivaa sweta lenye kofia au kepu, mimi uso wangu una aibu hivyo ninapokuwa mbele ya watu wengi, inakuwa inanisaidia kuniweka huru.”
Naye msanii wa Bongofleva, Omary Waziri Shaban ‘Kidampa’ anasema kwa upande wake anapovaa mbele ya watu wengi, anakuwa anahitaji utulivu wa kutoonekana kwa wakati huo:”Kwangu inakuwa kuondoa attention ya watu, waache kufanya kazi zao, waanze kukufuatilia wewe.
Anaongeza: “Binafsi nikienda sehemu, sipendi watu waache kufanya kazi zao, badala yake waanze kunizingatia mimi au kunishangaa, ndiyo maana natumia prova ili kuepusha hayo, ila ukiniona nimevaa stejini inakuwa nimetaka nitoke na muonekano huo.”
Kwa upande wake, msanii mwingine wa Bongofleva, Rashid Said ‘Bright’ anasema: “Nikivaa sweta hasa wakati nasafiri na ndege, inakuwa inategemea na hali ya hewa ya nchini ama mkoa ninayokwenda, wakati mwingine inakuwa najisikia nipo huru zaidi kutokeza vile mbele ya watu wengi.”
Hata hivyo, staa wa Bongofleva, Nedy Music anasema: “Kwa upande wangu napenda kuvaa hoodie, navaa sare juu na chini kwani sipendi mambo mengi, nikijua natumia muda mwingi kwenye ndege, hivyo nikivaa hivyo najisikia kuwa huru, nikilala najua aliyeko kushoto au kulia anakuwa hanioni kwa sababu nakuwa nimezibwa na sweta lenye kofia.
Anaongeza: “Ingawa wengine wanaiga baada ya kuona kwa watu fulani, hasa watu wenye majina makubwa duniani pia mtu anaweza akavaa hivyo anakuwa anatambulisha biashara yake.”
Na anachokisema msanii wa Bongofleva, Jay Melody kuhusiana na kuvaa masweta ya makofia ni kwamba,” kwanza nakuwa huru hasa safari za ndege ambapo nazingatia zaidi hali ya hewa, wakati mwingine inakuwa swaga tu, naangalia ni namna gani naweza nikatokea mbele ya macho ya jamii.” Akizungumzia hilo, mkongwe wa Bongofleva, Juma Nature: “Kuna masweta ambayo tunayauza, inakuwa moja ya kutangaza biashara mashabiki wakiyapenda wakiona tumevaa ni rahisi kununua.”