Simulizi ya Nyakanda iliyobeba misoto kibao
Muktasari:
- Kwa sasa hakuna shaka kwamba miongoni mwa makipa wanaofanya vizuri na kung’ara Ligi Kuu ni pamoja na nyota huyo kutokana na uimara wake langoni akiwa chaguo la benchi la ufundi la timu hiyo.
MSOTO. Ni neno unaloweza kutumia kuelezea maisha ya kipa wa Polisi Tanzania, Christopher Nyakanda aliyopitia hadi kuwa tegemeo kikosini huku akifanikiwa kuiweka pazuri timu hiyo kwenye Ligi Kuu Bara.
Kwa sasa hakuna shaka kwamba miongoni mwa makipa wanaofanya vizuri na kung’ara Ligi Kuu ni pamoja na nyota huyo kutokana na uimara wake langoni akiwa chaguo la benchi la ufundi la timu hiyo.
Pamoja na kung’ara kwake unaambiwa amesota sana huko nyuma akifanya shughuli mbalimbali ambazo ziligoma na kuamua kuzama moja kwa moja kwenye soka mbapo wazazi wake walikuwa sehemu ya safari yake.
Polisi Tanzania iliyowahi kushuka daraja misimu miwili nyuma akiwamo kikosini kipa huyo, ilirejea msimu huu na imekuwa na mwenendo mzuri unaoiweka katika ramani thabiti kwenye msimamo..
MANULA AMTOA UDENDA
Nyakanda anasema wakati akisota kusaka ndoto yake ya soka 2019 alitua Dar ambapo aliamua kuingia uwanjani kufuatia mchezo wa Simba dhidi ya Nkana, ambapo anasema alijifunza kitu.
Anasema mbali na Simba kutakata mabao 3-1, lakini alivutiwa na kiwango bora alichoonyesha kipa wa zamani wa timu hiyo, Aishi Manula (kwa sasa Azam FC) na kujisema kimoyo kuwa anatamani kufika hatua hiyo.
“Ilikuwa mechi ya klabu bingwa Afrika, ambapo Simba alishinda 3-1 lakini Manula alinihamasisha sana nikaamini muda wangu utafika na mimi nitafikia ndoto zangu na leo sijutii ninachokifanya,” anasema kipa huyo.
ALISOTA HAPA
Kama ambavyo kila binadamu kuwa na historia yake ya maisha kabla ya kutoboa, Nyakanda naye anayo machungu sana kwenye mishe zake hadi kufikia alipo kwa sasa, huku akiamini kesho yake ni kubwa zaidi.
Anaeleza kuwa kabla ya kuonekana staa kwa sasa, alipitia mambo mengi ikiwamo kuimba, kuigiza, kuvua samaki lakini kazi zote hizo hazikumlipa chochote na hakuwahi kuzikubali kama ilivyo soka.
Anasema baada ya kujaribu maeneo na shughuli nyingine za kijasiriamali, aliamini kuwa ndoto zake ni kucheza mpira na anaweza kutoboa kupitia kipaji chake mguuni na hatimaye ameweza.
“Nilijaribu vitu vingi, nilishawahi kuigiza, kuimba, uvuvi na kufanya shughuli nyingine lakini sikutoboa nikaamua kuvumilia kutimiza ndoto zangu za kucheza mpira na ninashukuru nimefanikiwa,” amesema.
ALIKOTOKA
Mchezaji huyo mkazi wa Mwanga mkoani Kilimanjaro anasema licha ya kucheza kuanzia shuleni katika michuano ya Umitashumta na Umisseta, alibahatika kucheza pia kituo cha michezo cha Moskisa ya mkoani humo.
Anae leza kuwa baadaye alienda kujaribu bahati yake kufanya majaribio kwenye kikosi cha vijana (U20) cha Polisi Tanzania ambapo alionyesha uwezo na juhudi hadi kupata nafasi ya kucheza ligi ya vijana.
Anasema msimu wa 2020/21 aliyekuwa Kocha wa timu hiyo, Malale Hamsini alimpandisha kikosi cha wakubwa ambapo alipewa mechi mbili kati ya 30 lakini hakukata tamaa akiitumia kama fursa ya kujifunza.
“Msimu wa 2021/22 nikaanza kupata namba japokuwa nilikuwa na upinzani wa makipa wazoefu akiwamo Metacha Mnata na Peter Manyika, japokuwa niliishi nao vizuri wakawa wananipa matumaini.
“Msimu wa 2022/23 nikaanza kuaminiwa kupewa nafasi lakini kwa bahati mbaya timu ilishuka daraja nikiwa nayo na nikabaki kikosini misimu mitatu Championship hadi sasa nikarejea nao tena,” anasema mchezaji huyo.
UHAKIKA WA NAMBA
Hadi sasa Polisi Tanzania imecheza mechi tisa na kuwa nafasi ya sita kwa pointi 12, ambapo kati ya hizo Nyakanda amecheza michezo minane akikosa mmoja dhidi ya Singida Black Stars ambayo alikuwa na tatizo la kifamilia.
Akielezea mwenendo wake kikosini hadi kuwaweka benchi makipa watatu akiwamo mkongwe Beno Kakolanya mwenye uwezo na uzoefu mkubwa, Nyakanda anasema kujituma ndio siri kubwa kwake.
Anabainisha kuwa anapokuwa kikosini mawazo na akili huwa katika kudaka na si vinginevyo akieleza kuwa kwa muda aliokaa kikosini amejifunza mengi hata kwa wenzake akiwamo Kakolanya humpa maufundi.
“Kikubwa zaidi ni kupambana na kujituma, nimeishi na makipa wengi wenye uwezo na uzoefu hivyo kwa muda ambao nimekuwa benchi nilipata darasa kwa wenzangu na hadi sasa naendelea kujifunza,” anasema.
“Nilionao kikosini kwenye sehemu ya kipa akiwamo Kakolanya ananipa maufundi mengi kwakuwa amenitangulia kimpira hivyo nafurahia namna tunavyoishi vizuri na mafanikio ya timu ni ya wote.”
ALAMBA AJIRA
Mpira umeendelea kufungua fursa nyingi kwa vijana, ambapo Nyakanda ni moja ya waliobahatika kuingia kwenye mfumo wa ajira za polisi na kwa sasa ana majukumu nje ya soka.
Akielezea nafasi hiyo, kipa huyo anasema haikuwa kazi nyepesi lakini kutokana na mipango ya Mungu alimjalia kumuonyesha njia na sasa anaendelea kutumikia ajira yake kulingana na majukumu anayopewa.
“Nashukuru Mungu mpira umenifungulia njia nyingi ikiwamo ajira ya polisi, haikuwa rahisi lakini ni mipango pale Mungu anapoamua, kwa sasa naendelea kutimiza wajibu wangu kulingana na maelekezo,” anasema Nyakanda.
SAPOTI YA WAZAZI
Kipa huyo anaeleza kuwa katika msoto wake kwa muda wote wazazi walikuwa sehemu ya safari yake ya maisha kwani hata alipomaliza kidato cha nne walimuuliza atakachofanya.
Anasema kutokana na hali ngumu ya uchumi wa familia muda mwingine walimkatia tamaa kuhusu mpira wakiamini hawezi kutoboa, japokuwa mwenyewe alibaki na msimamo wa ndoto zake kufanikiwa. “Waliogopa na kutoamini kwamba mpira unaweza kubadili maisha yangu na hii ilikuwa ni kwa sababu ya ugumu wa maisha ya familia, lakini niliwaaminisha kuwa nitafanikiwa na Mungu akanipa njia,” anasema mchezaji huyo.
Anabainisha kuwa kabla ya milango kufunguka aliamua kuondoka nyumbani kuelekea Dar es Salaam kwa lengo la kutafuta nafasi ya kucheza soka, ambapo takribani miaka miwili hakutoboa.
“Ndoto yangu ni kuwa kipa tegemeo haswa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, kipa bora wa Ligi Kuu na kipa bora wa Polisi Tanzania, kimsingi ni kuendelea kupambana na kumtanguliza Mungu,” anasema.