Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi ya Ndemla yenye mengi matamu, machache ya kuumiza

Muktasari:

  • Na kwa uzoefu wawili hao pia wana uzoefu mkubwa kuliko Fei. Hata hivyo, katika upande wa kupiga mashuti ya nje ya 18 na kutikisa nyavu wanaweza kuwa sawa au mdogo akawazidi wakubwa zake.

UNAWEZA kusema umfananishe Said Ndemla na Feisal Salum 'Fei Toto' au Hassan Nassor Maulid 'Machezo', lakini itakuwa si sahihi. Kwa upande wa umri Ndemla na Machezo ni wakubwa kuliko Fei Toto.

Na kwa uzoefu wawili hao pia wana uzoefu mkubwa kuliko Fei. Hata hivyo, katika upande wa kupiga mashuti ya nje ya 18 na kutikisa nyavu wanaweza kuwa sawa au mdogo akawazidi wakubwa zake.

Nyota hao watatu wamekuwa bora zaidi kupiga mashuti ya mbali. Mwanaspoti limefanya mahojiano na kiungo mshambuliaji wa JKT Tanzania, Ndemla ambaye kamtaja Fei Toto kuwa ni nyota ambaye ana uwezo mkubwa na kwamba anapita katika nyayo zake kwa ubora wa kupiga mashuti ya mbali.


FEI TOTO NJE 18 HAKUACHI

Licha ya kuwa na ubora wa kufanya vizuri kwenye eneo la kupiga mashuti nje ya 18, Ndemla hajasita kumtaja Fei Toto kuwa ana uwezo mzuri pia katika kufanya hivyo.

"Ni wengi wanafanya hivyo, lakini kwangu Fei Toto ni bora na amekuwa akifanya uamuzi mzuri ambao umekuwa na faida kwake hata kwa klabu," anasema Ndemla.

"Kupiga mashuti nje ya 18 ni uamuzi wala siyo mazoezi, unaweza ukafanya mazoezi kwa ajili ya kufanya hivyo na ukiingia kwenye mchezo ukashindwa kutokana na kukosa uamuzi wa kufanya hivyo."

Ndemla anasema huwa hafanyii mazoezi zoezi hilo, lakini huwa uamuzi ndiyo unampa akili ya kupiga na kujikuta anafanya kile ambacho kinakuwa hakijatarajiwa na wengi kwa wakati husika.


KICHUYA KONA, NYONI PENALTI

Katika kikosi cha nyota 11 kuna uamuzi wa kocha kwenye mambo fulani ya uwanjani kutokana na mazoezi yanavyofanyika siku moja kabla ya mchezo husika, na kuna mastaa ambao hupewa majukumu ya kupiga kona, faulo na penalti.

Kwa upande wa Ndemla anasema kwenye Ligi Kuu Bara kuna mafundi wawili ambao anaamini likitokea pigo la kona au penalti wana uhakika wa kufanya kwa usahihi.

"Mambo ya kona kwangu ni Shiza Kichuya. Ni mtu sahihi timu yangu haiwezi kuchongwa kona na mchezaji yeyote kama kuna Kichuya kutokana na ubora wake eneo hilo. Ana ufundi, anaweza akafunga moja kwa moja au akatoa krosi nzuri ikazaa bao," anasema Ndemla.

"Lakini, kwa upande wa penalti naweza kuacha zikapigwa na wengine wote ya mwisho ambayo inaweza kuamua matokeo hakuna mwingine zaidi ya Erasto Nyoni. Huyu hata ingewezekana kupigwa na mmoja, basi ningemuachia apige zote. Yupo vizuri eneo hilo."

Ndemla anasema ukiondoa mafundi hao wawili anaowataja kwenye maeneo hayo, lakini anamuongeza na Mohammed Hussein 'Tshabalala' kuwa mmoja wa mafundi wazuri wanaotumia mguu wa kushoto.

"Kwa asilimia kubwa nyota wengi wanaotumia mguu wa kushoto ni mafundi, lakini kwangu Tshabalala ni bora zaidi kwani anajua kumwaga maji na ana matumizi mazuri na mguu huo."


JEZI NAMBA 8 MAFUNDI

Namba 8 ni jezi ambayo ina sifa ya kuvaliwa na mastaa wa maana wenye ufundi wa kipekee kama Khalid Aucho, Bruno Fernandes (Man United), Andre Iniesta (zamani Barcelona), Toni Kroos (zamani Real Madrid0, Steven Gerrard (zama zile Liverpool), Frank Lampard (zamani Chelsea) na wengine wengi, na Ndemla anaungana na kauli hiyo huku akidai kuwa mara nyingi pia inavaliwa na viungo.

"Jezi namba 8 haivaliwi na wachezaji wabovu. Ni jezi ya heshima, inavaliwa na nyota wengi wanaojua mpira sawa na jezi namba 10 inavaliwa na mastaa ambao ndiyo wanaozibeba timu zao," anasema mchezaji huyo.

"Kama ni mfuatiliaji wa mpira utaungana na mimi kwenye hilo. Mastaa wakubwa ndiyo wanaivaa. Mimi nimeivaa nikiwa hapa JKT Tanzania baada ya jezi yangu namba 13 kukuta ina mtu, na sikutaka kumuomba, lakini naamini na mimi nastahili kuivaa kwani ni mpambanaji pia."

Ndemla anasema alianza kuvaa jezi namba 13 kutokana na mapenzi yake kutoka kwa mchezaji wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya Ujerumani, Michael Ballack.

"Jezi namba 13 nilikuta inavaliwa na mtu, hivyo sikutaka kumuomba nikatafuta namba nyingine. Sasa navaa namba 8 ambayo naikubali pia na nilikuta haina mtu."


TAJIRI WA NJUMU, AMTAJA TSHABALALA

Unaweza kushangaa, lakini huo ndiyo ukweli. Wakati mastaa wengi wakitajwa kwa unadhifu wa muonekano hasa wakiwa kwenye mavazi ya nyumbani nje na jezi, Ndemla anaipenda kazi yake buana, hivyo ndivyo unaweza kusema kutokana na kuwa na jozi nyingi za viatu kama anavyosema.

"Kazi yangu ni mpira, naipenda kazi hii. Kuzingatia hilo, kitu napenda ni kuwa na vifaa vingi ambavyo haviwezi kunifanya nikashindwa kufanya kazi yangu kwa usahihi. Mimi nina viatu vingi sana zaidi ya (jozi) kumi," anasema.

"Kutaja idadi nitajichanganya, ila ni zaidi ya kumi. Mimi kila kikitoka kiatu kizuri nanunua, lakini pia nimekuwa nikipokea zawadi kutoka kwa wachezaji wenzangu."

Ndemla anasema amewahi kupewa viatu na Mwinyi Kazimoto, Ibrahim Ajibu, Tshabalala na David Kameta 'Duchu'.

Lakini, je amewahi kununuliwa na mpenzi? Ndemla anasema haijawahi kutokea.


AMTAJA GORAN SIMBA

Ndemla ni zao la Simba na amepita Singida Black Stars huku sasa anakipiga JKT Tanzania, na kote Amekutana na makocha wengi, lakini anamtaja Goran Kopunovic kuwa ndiye aliyempa neema Simba na kumfanya atambulishe kipaji chake.

"Nimepita chini ya makocha wengi nikiwa Simba, Singida na sasa JKT Tanzania, lakini kwangu bora ni Kopunovic. Huyu aliniamini sana. Ndani ya msimu mmoja alioifundisha Simba alinipa nafasi ya kucheza na alikuwa ananikubali.

"Nilipata nafasi ya kucheza chini yake msimu mzima alioifundisha Simba hadi hapo makubaliano ya pande zote mbili yalipofikiwa. Nilikuwa bora sana chini yake," anasema Ndemla ambaye anadai kuwa kipaji chake ni cha kuzaliwa nacho na kucheza eneo la kiungo amerithi kutoka kwa baba yake na pia alicheza kiungo mshambuliaji.


CHAMA, ZAYD VIUNGO BORA

Ligi Kuu Bara imepokea viungo wengi bora ambao wamecheza kwa mafanikio, lakini Ndemla anamtaja Clatous Chama, kwa nyota wa kigeni kuwa ndiye mchezaji bora kuwahi kumshuhudia masihani mwake.

"Ni kweli Ligi Kuu wamepita mastaa wengi na wengine wapo wanaendelea kufanya vizuri, lakini mimi huniambii kitu kuhusu Chama. Ni kiungo wangu bora kuwahi kushuhudia kutokana na aina yake ya uchezaji. Ni mtulivu, anacheza kwa maarifa, ni darasa tosha kwetu," anasema na kuongeza:

"Sina maana mbaya kwamba wengine ni wabovu, ila kwa kuwa umenipa nafasi ya kuchagua ndiyo maana nimefanya chaguo hilo. Chama ni habari nyingine. Ni mchezaji ambaye anatumia sana akili na siyo nguvu. Anaufanya mpira kitu rahisi na ana uwezo wa kuamua mechi."

Kwa upande wa nyota wa ndani, Ndemla anamtaja kiungo wa Azam FC, Yahya Zayd kuwa licha ya kutozungumzwa sana na mashabiki lakini anaona ubora mkubwa na ana uwezo wa kumpa kocha machaguo mengi amtumie eneo gani.

"Mpira wa Tanzania kuna wachezaji wana bahati ya kuimbwa sana na mashabiki, lakini kuna wengine wana uwezo mkubwa, lakini hawazungumzwi. Basi Zayd ni miongoni mwao. Ni mchezaji mzuri na ana uwezo mkubwa."


MTENJE, NASHONI WACHEZAJI WA KADI

Licha ya soka kuwa burudani na ajira, kuna matukio hufanyika iwe kwa makusudi au bahati mbaya na kusababisha waamuzi kutoa adhabu, na katika hilo Ndemla anamtaja Kelvin Nashon wa Pamba Jiji na Mtenje Albano kuwa hawezi kuwawekea dhamana kutopata kadi kwenye mechi.

"Ukiondoa ubora walionao wachezaji hao siwezi kuwawekea dhamana kwenye suala la kutoonyeshwa kadi kwenye mechi mbili mfululizo," anasema Ndemla.

"Ni wachezaji wazuri, wana uwezo mkubwa uwanjani. Ukitaka kufanya nao bato huwezi kutoboa utatolewa nje. Wao wanatumia nguvu, ni rahisi kwao kuonyeshwa kadi za njano."


NIDHAMU KWANZA

Ndemla amecheza timu nne kwenye soka la ushindani akianzia Simba, Singida Black Stars, Mtibwa Sugar na sasa JKT Tanzania ambayo anaitaja kuwa tofauti na timu alizopita kwani kuna nidhamu kutokana na kumilikiwa na jeshi, lakini mambo mengine hayatofautiani.

"Kwenye mpira hakuna tofauti sana zaidi ya majina tu. Kuhusu nidhamu hapa ndiyo kila kitu, vitu vingine vinafuata. Si unafahamu hii ni timu ya jeshi? Huwezi kufananisha na timu nyingine za wanachama na watu binafsi," anasema Ndemla ambaye anawataja wadogo zake wawili ambao pia anaamini watakuja kufanya vizuri kwenye soka kutokana na kufuata nyayo zake.

"Nina wadogo zangu wawili ukiondoa baba yangu ambaye pia alikuwa mchezaji na wao wanakuja njia yangu. Mmoja ni winga anatumia mguu wa kushoto na mwingine ni kiungo mshambuliaji kama mimi. Lakini pia baba ambaye alikuwa mtangulizi wetu," anasema mchezaji huyo na kufafanua kuwa wadogo zake hao hivi sasa wanasoma na hawajaanza kucheza soka la ushindani kutokana na kujikita katika masomo.


ANDAMBWILE, YASSIN WATU POA

Katika soka kwa mchezaji akipata nafasi ya kupita kwenye timu zaidi ya mbili hawezi kuacha kukumbuka mazuri na mabaya alikopita, na Ndemla anasema mazuri ni mengi kuliko mabaya.

"Ni mengi mazuri nikisema niyazungumze hapa sitamaliza leo, lakini kwa timu yangu ya mwisho Singida kabla sijaja JKT Tanzania nakumbuka vituko na urafiki wa karibu kutoka kwa wachezaji ambao nilikuwa nafanya nao kazi pamoja," anasema.

"Singida maisha yalikuwa mazuri, nimekutana na wachezaji wakarimu sana na wana utu. Mfano nakumbuka maisha ya urafiki nilikuwa na ukaribu na Yassin Mustafa, Aziz Andambwile na Paul Godfrey 'Boxer'. Tuliishi kama familia na wote tumetengana kwa kila mmoja kujaribu maisha mengine nje ya timu hiyo."

Ndemla anasema kuna maisha nje ya soka na ameishi vizuri na wachezaji hao na ndiyo maana anakumbuka mambo waliyokuwa wanayafanya kipindi hicho wakiwa pamoja akiwakumbuka pia kwa vituko na ucheshi waliokuwa nao.