Rekodi zilivyotawala Ligi Kuu Bara 2025-2026
Muktasari:
- Wakati ushindani huo ukizidi kuongezeka zikibakia raundi saba kuhitimisha msimu, zipo rekodi mbalimbali za timu, makocha na wachezaji zilizowekwa kama zinavyoelezewa.
LIGI Kuu Bara msimu wa 2025-2026, unaendelea kushika kasi, tunashuhudia upinzani makali katika mbio za kusaka ubingwa pia, kuna wale waonapamba kukwepa janga la kushuka daraja jambo linalofanya kila mechi sasa kuwa kama fainali.
Wakati ushindani huo ukizidi kuongezeka zikibakia raundi saba kuhitimisha msimu, zipo rekodi mbalimbali za timu, makocha na wachezaji zilizowekwa kama zinavyoelezewa.
MABAO 382
Hadi sasa yamefungwa mabao 382, kati ya hayo wachezaji wazawa 99 wamefunga 211, wageni 51 wakifunga 156, huku mabao 12 ni ya kujifunga, wakati matatu yakiwa ni ya ushindi wa mezani ilioupata Pamba Jiji, Oktoba 27, 2025.
Pamba ilipewa ushindi huo wa mabao 3-0 na pointi tatu, baada ya mechi yao dhidi ya Dodoma Jiji iliyopigwa Oktoba 25, 2025, kusimama dakika ya sita, kufuatia kutokea hitilafu ya umeme kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.
Wakati mechi hiyo inasimama, wenyeji Dodoma Jiji walikuwa wanaongoza bao 1-0, lililofungwa na Benno Ngassa. Hata hivyo, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi Kuu Bara katika kikao chake cha Oktoba 27, 2025, kilitoa uamuzi wa kuipa Pamba Jiji ushindi wa mabao 3-0 na pointi tatu, kwa kosa la Dodoma Jiji kushindwa kuiandaa mechi hiyo kikamilifu.
Sababu ya Dodoma Jiji kupokwa ushindi huo ni kutokana na kutofanya juhudi zozote za kurejesha mwanga kwenye Uwanja wa Jamhuri, hivyo kusababisha mechi hiyo kuvurugika, huku adhabu ikitolewa kwa kuzingatia kanuni ya 32:3 ya Ligi Kuu Bara.
Kutokana na adhabu hiyo kwa mujibu wa kanuni ya 32:3 ya Ligi Kuu Bara kuhusu kuvuruga mechi, bao la Ngassa lilifutwa katika orodha ya mabao yake na ya timu anayoichezea.
Jambo linalosubiriwa kwa hamu ni kuona kama idadi hiyo ya mabao 382, yaliyofungwa hadi sasa itaifikia ya msimu wa 2024-2025 yalipofungwa 572, ambapo wazawa 118 walifunga mabao 306 na wageni 65 wakifunga 247, huku ya kujifunga 19.
BAO LA MAPEMA ZAIDI
Mabao mawili aliyofunga mchezaji wa Coastal Union, Bakari Msimu katika ushindi wa timu hiyo wa 4-1 dhidi ya Tanzania Prisons, Februari 10, 2026, yamemfanya nyota huyo kuandika rekodi ya kufunga bao la mapema zaidi.
Nyota huyo alifunga mabao hayo kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya na mengine yakifungwa na Shiza Kichuya na Cleophace Mkandala, huku bao pekee la Prisons likifungwa na George Mpole.
Rekodi tamu alizoandika Msimu ni ya kufunga bao la mapema zaidi msimu huu katika Ligi Kuu ambalo lilichukua sekunde ya 58, ya pili ni ya kufunga mabao yake ya kwanza, huku ya tatu ni ya kuifungia timu hiyo bao la kwanza ugenini msimu huu.
REKODI YA YANGA, AZAM YAVUNJWA
Ushindani msimu huu umeanza kuonekana baada ya kushuhudia Yanga na Azam FC zikivunjiwa rekodi zao za kucheza kwa muda mrefu bila ya kupoteza mechi ya Ligi Kuu Bara, baada ya miamba hiyo kutengeneza ufalme wake kimya kimya.
Kichapo cha mabao 4-1 ilichokipata Azam kutoka kwa TRA United, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, Mei 8, 2026, ilikifanya kikosi hicho kupoteza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara tangu Aprili 10, 2025.
Kabla ya hapo, mara ya mwisho kwa Azam kupoteza ilikuwa ni kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Yanga, Aprili 10, 2025, ikiwa ni rekodi bora iliyodumu hadi Mei 8, 2026, baada ya timu hiyo kucheza mechi 26, ikishinda 15, sare 10 na kupoteza moja.
Kwa upande wa Yanga, baada ya kucheza kwa siku 552 , sawa na mwaka mmoja, miezi sita na siku sita bila ya kupoteza, hatimaye rekodi hiyo bora ilivunjwa rasmi Mei 13, 2026, ilipochapwa mabao 3-2 dhidi ya Dodoma Jiji.
Dodoma Jiji ilivunja rasmi rekodi hiyo ya Yanga ya kucheza mechi 42 bila kupoteza tangu ilipochapwa na Tabora United sasa TRA United mabao 3-1, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Novemba 7, 2024.
REKODI TISHIO AZAM
Licha ya Azam FC kutibuliwa rekodi ya kucheza muda mrefu bila kwa kupoteza dhidi ya TRA United, ila kikosi hicho kimekuwa na mwenendo mzuri kinapocheza wa nyumbani.
Azam FC inashikilia rekodi bora hadi ya kucheza mechi za nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, huku ikiwa haijaruhusu kufungwa bao.
Msimu huu hadi sasa timu hiyo imecheza mechi 11 nyumbani, imeshinda saba na kutoka sare nne, ikifunga mabao 16, bila kuruhusu, ikiwa ni rekodi bora kwa Kocha Mkuu, Florent Ibenge.
JOSIAH NA REKODI TATU
Suluhu iliyoipata Dodoma Jiji dhidi ya Simba, Februari 25, 2026, imemfanya Amani Josiah kuandika rekodi mpya ya kocha wa kwanza kwa kikosi hicho kupata sare mbele ya Wekundu wa Msimbazi.
Tangu msimu wa 2020-21, Dodoma Jiji imecheza mechi 11 dhidi ya Simba kati ya hizo imepoteza 10 na kutoa sare moja, huku wakifunga mabao mawili na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 22.
Josiah aliyejiunga na timu hiyo Oktoba 16, 2025, akichukua nafasi ya Mnyrwanda, Vincent Mashami anakuwa ni kocha wa kwanza wa Dodoma Jiji kuandika rekodi ya kupata sare katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba.
Rekodi ya pili kwa Josiah aliyoiweka ni ya Dodoma Jiji kupata ushindi wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga tangu imepanda daraja msimu wa 2020-2021, baada ya kushinda 3-2, Mei 13, 2026, kwani kabla ya hapo ilichapwa mechi 10 na sare moja tu.
VITA IKO HUKU!
Ukiachana na vita ya ubingwa ambapo Yanga inaongoza na pointi 54, ikifuatiwa na Simba pointi 52 na Azam ya tatu (pointi 46), ila uhondo zaidi uko kwa timu zinazopambana kushuka daraja na zile za ‘Play-Off’.
Hadi sasa KMC ipo mkiani mwa msimamo ikiwa nafasi ya 16 na pointi tisa baada ya kucheza mechi 23, ikihitaji zaidi miujiza ya kujinasua na janga la kushuka daraja, ikifuatiwa na Tanzania Prisons inayoshikka nafasi ya 15 na pointi 17.
Kwa upande wa timu zilizo katika mstari wa kucheza mechi za ‘Play-Off’, ni Mbeya City iliyo nafasi ya 14 na pointi 21 na Namungo inayoandamwa na ukame wa ushindi, inayoshika nafasi ya 13 na pointi 24.
Timu nyingine ni Mashujaa iliyo nafasi ya tisa na pointi 26, ambazo ni sawa na Mtibwa Sugar inayoshika nafasi ya 10 na Coastal Union iliyo nafasi ya 11 na pointi 25, sawa na kikosi cha Fountain Gate kinachoshika nafasi yake ya 12, haziko salama ikiwa hazitachanga karata zao vizuri.
Vita nyingine ni kuwania nafasi ya nne ya kupata tiketi ya kuwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika, ipo kwa Singida Black Stars iliyo nafasi nne na pointi 38, JKT Tanzania ya tano na pointi 36, TRA United ya sita na pointi 34, Dodoma Jiji ya saba na pointi 32, Pamba Jiji ya nane na pointi 30, kila moja akichanga karata zake vizuri anaweza kupata nafasi hiyo.