Real Madrid mzigoni, Mourinho akirudi na mawili LaLiga
Muktasari:
- Katika kipindi cha mapumziko ya mechi za kimataifa, benchi la ufundi la Real Madrid lilitumia muda huo mrefu kushughulikia maeneo mawili katika kikosi hicho yanayoisumbua timu hiyo.
MADRID, HISPANIA: REAL Madrid itakuwa mzigoni leo, Jumamosi, Oktoba 10, 2026, dhidi ya Villarreal katika mchezo wa nane wa Ligi Kuu Hispania (LaLiga), unaotarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu kuanzia saa 4:00 usiku.
Katika kipindi cha mapumziko ya mechi za kimataifa, benchi la ufundi la Real Madrid lilitumia muda huo mrefu kushughulikia maeneo mawili katika kikosi hicho yanayoisumbua timu hiyo.
Kocha Jose Mourinho na benchi lake la ufundi wameutumia muda huo kuboresha upya mfumo wa uchezaji wa Real Madrid; vipaumbele viwili vikizingatiwa ikiwa kwanza ni kuweka mikakati itakayomwezesha Vinicius Junior ambaye alikuwa katika majukumu ya timu ya taifa ya Brazil kurejea katika kiwango chake bora.
Pili, benchi hilo limefanya marekebisho katika safu ya kiungo ili kuipa timu udhibiti mkubwa zaidi katika vipindi fulani vya mechi, huku pia likiimarisha mshikamano wa wachezaji na uimara wa ulinzi.
Malalamiko ya Mourinho kuhusu uamuzi wa waamuzi baada ya Real Madrid kufungwa katika mchezo wa dabiy, ambayo yanaeleweka kutokana na ushahidi wa wazi ulioonekana kwenye video hayajatumiwa ndani ya timu kama kisingizio cha matokeo dhidi ya Atletico Madrid wala upungufu wa timu katika kumiliki mpira. Badala yake, timu imefanya tathmini ya kina kuhusu uwajibikaji wa wachezaji.
SUALA LA VINICIUS
Vinicius bado ni sehemu muhimu ya mipango ya Real Madrid. Badala ya kuhoji nafasi yake katika kikosi cha kwanza, mkazo umewekwa katika kubaini marekebisho ya kiufundi yatakayomsaidia Mbrazili huyo kurejea katika kiwango chake bora.
Nyota huyo anapitia mwanzo wa msimu wenye kiwango cha chini zaidi tangu kipindi cha janga la corona, akiwa amefunga bao moja tu na kutoa asisti tatu katika mechi nane za kwanza. Hata hivyo, imani ya Mourinho kwake ni kwamba atarejea kwenye ubora.
Vinicius anashika nafasi ya nne katika kikosi hicho kwa idadi ya dakika alizocheza akiwa nazo 652 akitanguliwa na Fede Valverde mwenye 654, pamoja na wachezaji wawili ambao hawajakosa hata dakika moja ya mchezo, Thibaut Courtois na Kylian Mbappe waliocheza kila mmoja 720.
Katika Uwanja wa Estadio Metropolitano unaomilikiwa na Atletico Madrid, Vinicius alionyesha kiwango cha chini akiwa mchezaji wa Real Madrid aliyeshiriki kwa kiwango kidogo zaidi katika kucheza na mpira, akizidiwa hata na wachezaji walioingia wakitokea benchi. Katika mchezo huo aligusa mpira mara 22, ikilinganishwa na mara 24 za Eduardo Camavinga aliyeingia dakika ya 74, na mara 26 za Bernardo Silva aliyeingia dakika ya 81.
Vinicius alijaribu kukokota mpira akiwa akikabiliana na mpinzani mara moja tu na kufanikiwa. Hata hivyo, alimaliza mchezo akiwa amefanikiwa kupiga pasi nane pekee zilizowafikia wachezaji wenzake.
“Mchezaji akitoa kila alichonacho uwanjani, huwezi kumtaka afanye zaidi ya hapo,” Mourinho amekuwa akisema mara kwa mara akimtetea Vinicius, ambaye amekubali kikamilifu matakwa ya kocha huyo kuongeza mchango wake katika majukumu ya ulinzi.
Ingawa mabadiliko ya kiufundi bado hayajaonekana uwanjani, uwezekano ni kwamba Mbrazili huyo hatalazimika tena kurudi nyuma sana kusaidia kulinda upande wa kushoto, badala yake jukumu hilo linaweza kukabidhiwa kwa mmoja wa viungo.
MFUMO VIUNGO WAWILI WA KATI
Wakati huohuo, Real Madrid inatafuta namna ya kuwa na utulivu zaidi katika safu ya kiungo, ambalo ndilo eneo pekee la timu halijapata mfumo wa kudumu. Mourinho anaendelea kutumia mfumo wa 4-2-3-1 unaompa Jude Bellingham uhuru wa kucheza kama kiungo mshambuliaji wa kati, namba 10. Hadi sasa, mchezaji huyo wa kimataifa wa England amefanya vizuri.
Nyota huyo amefunga mabao katika mechi tatu tofauti dhidi ya Rayo Vallecano, Malaga na Espanyol, huku pia akitoa asisti dhidi ya Real Sociedad. Jambo muhimu ni kwamba amefanya hivyo bila kulazimika kubeba mzigo wa majukumu ya ulinzi wa upande wa kushoto, jukumu ambalo kwa sasa linatekelezwa na Vinicius.
Ikumbukwe kuwa katika msimu wake wa kwanza Real Madrid, Bellingham alikuwa mhimili mkuu wa mabadiliko ya kiufundi yaliyofanywa na kocha Carlo Ancelotti, ambapo hatimaye yaliisaidia timu hiyo kutwaa mataji ya LaLiga na Ligi ya Mabingwa Ulaya katika msimu mmoja.
Wakati Mbappe akiwa bado hajaingia katika mipango ya kikosi, Ancelotti alimtumia Bellingham kama kiungo mshambuliaji wa kati, namba 10, nyuma ya Vinicius na Rodrygo. Hata hivyo, timu ilipokuwa ikijilinda, ilibadilika na kutumia mfumo wa 4-4-2, huku Mwingereza huyo akishuka na kusimama upande wa kushoto wa safu ya kiungo.
Kuhusu mfumo wa viungo wawili wa kati, Valverde anaonekana kuwa mchezaji ambaye ni vigumu kuondolewa katika kikosi cha kwanza kutokana na kile kilichoonekana hadi sasa. Pembeni yake, Mourinho amewajaribu viungo wanne tofauti katika mechi nane za mwanzo za msimu (kuanzia Ngao ya Jamii). Ushirikiano wa Valverde na Silva umezaa ushindi katika kila mechi waliyoanza pamoja, dhidi ya Espanyol, Real Sociedad na Rayo Vallecano.
Lakini, ushirikiano wa Valverde na Camavinga uliisaidia timu hiyo kupata ushindi rahisi dhidi ya Malaga na pia ulihusika katika kipigo dhidi ya Real Betis. Kwa upande mwingine, kumtumia Valverde na Trent Alexander-Arnold llikuwa suluhisho la dharura dhidi ya Inter Milan katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ushirikiano unaoonekana kuwa chaguo la muda mrefu, kati ya Tchouameni na Valverde umetoa matokeo yasiyo na mwendelezo mzuri. Ushirikiano huo uliisaidia Real Madrid kupata ushindi wa tabu dhidi ya Elche katika mchezo wa kusisimua, lakini ulionyesha udhaifu mkubwa katika kipigo dhidi ya Atletico Madrid.