Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Real Madrid ilitunga sheria ya Mbappe, Dar itunge ya Fei

FEI Pict

Muktasari:

  • Kodi yake kwa mwaka ni Sh360 milioni sawa na asilimia 37.5 ya mshahara wake.

FEISAL Salum ‘Fei Toto’ amesaini mkataba wa kuendelea kuitumikia Azam FC hadi 2027. Awali mkataba wake ulitakiwa kumalizika 2026. Katika mkataba mpya, mshahara wake wa mwaka utakuwa Sh960 milioni kabla ya kodi.

Kodi yake kwa mwaka ni Sh360 milioni sawa na asilimia 37.5 ya mshahara wake.

Hiki ni kiwango kilichochangamka sana na kuzidi hata baadhi ya nchi zilizoendelea kuliko Tanzania.

Kupitia kodi hii ya Feisal Salum nimekumbuka kilichotokea kwa Kylian Mbappe alipojiunga na Real Madrid mwaka 2024.

Ni nyota raia wa Ufaransa anayepokea mshahara wa mwaka wa Euro 31,250,000. Kodi yake ni Euro milioni 15...sawa na asilimia 48!

Hii ni kodi kubwa sana na Hispania ni nchi yenye sheria ngumu za kodi kwa wanamichezo na wawekezaji wengine kiasi, wengi wao huamua kuhamisha mitaji yao au kusajilia vipato vyao nje ya nchi hiyo.

Hapo ndipo hujikuta kwenye matatizo na sheria za nchi hiyo kuishia kukabiliana na kesi mahakamani.

PUM 03

Kutokana na hilo, mji wa Madrid ukaamua kutengeneza sheria ndogo ndogo za kuwalinda watu wa aina hii dhidi ya kodi kama hizi.

Hata hivyo, mji huu unafaidika na muundo wa serikali ya Hispania ambao unatoa mamlaka kwa serikali za majimbo kuwa na sheria zake za ndani.

Kwa hiyo serikali ya jimbo la Madrid ikatunga sheria maakumu iliyoitwa ‘Mbappe Law’ au sheria ya Mbappe, katika jitihada za kuwashawishi wageni wenye mitaji na vipaji kuwekeza mjini humo na kupata unafuu wa kodi.

Serikali ya jimbo la Madrid iliichapisha sheria hii mpya namba 4 ya mwaka 2024 katika gazeti lake rasmi la Novemba 28 mwaka 2024.

PUM 01 (1)

Lengo la msingi la sheria hii ni kuwavutia  watu wenye pesa, familia na nyota wa michezo kuja Madrid kutoka nje kwa kuwapa punguzo kubwa la kodi kwa vipato vyao binafsi kwenye rasilimali fulani zao.

Mbappe Law au Sheria ya Mbappe au sheria namba 4/2024 inarejesha Sheria ya Beckham, miaka zaidi ya 20 iliyopita ambayo bado inatumika hadi sasa.

Sheria ya Beckham ilitungwa pale David Beckham alipojiunga na Real Madrid mwaka 2003 akitokea Manchester United.

Chini ya sheria hii, wageni wote ambao wanaanza kufanya kazi Hispania, walitozwa kodi ya asilimia 24 badala ha 45....pia sheria hii ilikuwa na nafuu nyingine nyingi kwa wageni.


SHERIA MBAPPE INAFANYAJE KAZI

Kuanzia Januari Mosi 2024 mgeni yeyote Hispania ambaye amesajiliwa kodi zake Madrid, anaweza kufaidika na punguzo la kodi la asilimia 20 ya kipato chake.

Kwa mfano kama kipato chako ni Euro milioni 10 kwa mwaka na ukaamua kuwekeza Euro milioni mbili kwenye kampuni yoyote ya ndani ya Madrid, basi utapata punguzo la kodi la asilimia 20.

Utakuwa umeokoa Euro laki nne kupitia sheria hii...na ukiwekeza zaidi, ndiyo utaokoa zaidi.

PUM 02

DAR ES SALAAM IIGE

Mtoto wa Dar es Salaam, Chiddy Benz aliwahi kuimba Dar es Salaam Stand Up, akiutaka Mji wa Dar es Salaam kusimama.

Na mimi nautaka mji huu siyo tu kusimama bali kuamka kabisa kutoka usingizi mzito.

Feisal Salum ni mmoja tu kati ya wachezaji wengi wa kigeni wanaokuja jijini.

Halmashauri ya jiji inaweza kujipanga kuangalia namna ya kuwavutia watu hawa kuwekeza kwa kuwatengenezea mazingira fulani rafiki kupitia sheria maalumu kama Mbappe Law....ambayo mimi ningependa iitwe Fei Toto Law.

Wachezaji wa Kitanzania hawalipwi mabilioni kama Ulaya, lakini wanapata mamilioni mashallah.

Hizi milioni 100 na kuendelea ni kawaida....ambazo kimsingi zinafaa kuanzisha biashara fulani ndogo ndogo kulingana na uchumi wetu na mazingira yetu.

Kutokana na Fei Toto Law, Dar es Salaam inaweza kuwasaidia wachezaji hawa kutambua fursa na kuwekeza huku wakipata unafuu wa kodi.

Hii utawavutia hata wachezaji wa nje ya Dar es Salaam kuja kufaidika na sheria hii.

Hapo uchumi wa Dar es Salaam utazidi kuimarika na kuboresha maisha ya watu wake.

Hii siyo Dar es Salaam pekee. Miji kama Arusha, Dodoma na Mwanza inaweza kufanya hivi pia...lakini hata Zanzibar.

Kupitia fursa kama za utalii, inawezekana kabisa ukatengenezwa mpango utaambatana na elimu kwa wachezaji hawa kujua hizi fursa na wao kupeleka pesa zao kama sehemu ya mtaji kupitia hisa. Pesa watapata...na miji hii itakuza uchumi.

Madrid imeona fursa, na miji yetu iamke kuziona fursa hizi katika mazingira yetu.