Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Presha mpya yaibuka kimataifa

PRESHA Pict


SIMBA juzi usiku iliendeleza ubabe wa timu za Tanzania katika michuano ya CAF kwa msimu huu kwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Gaborone United ya Botswana.


Ushindi huo wa Simba iliyokuwa ugenini, ulikuwa ni muendelezo tu wa wawakilishi wa Tanzania, kwani Yanga iliuanzisha mwendo kwa ushindi wa 3-0 ugenini dhidi ya Wiliete Benguela ya Angola.


Azam FC ikiwa Juba, Sudan Kusini pia ilishinda mabao 2-0 dhidi ya El Merriekh Bentiu, huku Singida Black Stars ikitakata jijini Kigali, Rwanda kwa kuitambia Rayon Sports kwa bao 1-0, japo Mlandege ilichemsha kwa Insurance ya Ethiopia kwa kuchezea kichapo cha mabao 2-0.

Jana ilikuwa ni zamu ya KMKM iliyokuwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kuvaanana AS Port ya Djibouti waliokuwa wenyeji wa mechi hiyo ya raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika (bila shaka matokeo ya mechi hiyo tayari unayo).

Licha ya ya Yanga, Simba, Azam FC na Singida BS kushinda mechi zao za ugenini bado kuna presha mpya imeibuka kwa makocha kutokana na mashabiki na wapenzi wa klabu hizo kuonekana kutofurahishwa na vile timu hizo zilivyocheza. Presha kubwa ipo kwa makocha wa Yanga na Simba, Romain Folz na Fadlu Davids, kwani mashabiki wanaona timu hizo bado hazijacheza kwa ubora tangu msimu umeanza.

Simba na Yanga zote zipo katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kama wenzao wa Azam na Singida zilizopo Kombe la Shirikisho zimerudi na clean sheet kutoka ugenini, lakini bado namna timu hizo zilivyocheza wikiendi zimeongeza presha kwa makocha kwa mechi za marudiano wikiendi hii.

Presha ilizonazo Simba na Yanga sio katika mechi hizo za CAF, bali hata katika Ligi Kuu kwani tayari kengele ya hatari imeanza kulia tangu katika mechi za matamasha ya klabu hizo yaliyofanyika wiki iliyopita na timu hizo kushinda mechi za kirafiki za kimataifa dhidi ya klabu za Kenya.

Simba ilianza kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Gor Mahia, wakati Yanga ilishinda 1-0 mbele ya Bandari kabla ya kuvaana zenyewe katika Ngao ya Jamii na Simba kulala 1-0 ikiwa ni mara ya nne mfululizo kwa kocha Fadlu Davids kupoteza na kuongezewa presha wakati zikienda katika mechi za CAF.

PRE 05

WILIETE 0-3 YANGA

Ikiwa Angola ambako hii ni mara ya tatu kwenda huko, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 0-3 dhidi ya Wiliete Benguela huku rekodi mbili zikiwekwa.

Mechi hiyo ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2025-2026 iliyochezwa Septemba 19, 2025 kwenye Uwanja wa Novemba 11 uliopo Luanda, Angola, Aziz Andabwile alikuwa wa kwanza kufunga bao katika dakika ya 32 akiachia shuti kali la kutokea nje ya boksi lililomshinda kipa na mpira kujaa wavuni.

Dakika ya 71, Yanga ilipata bao la pili lililofungwa na Edmund John akimalizia pasi ya Maxi Nzengeli.

Prince Dube, alihitimisha ushindi huo akifunga bao la tatu dakika ya 83 baada ya kupewa pasi na Celestine Ecua.

Ushindi huo umeifanya Yanga kuweka rekodi mbili, kushinda kwa mara ya kwanza ugenini Angola baada ya mara mbili zilizopita kupoteza. Pili ni mara ya kwanza kwa kikosi hicho kufunga bao nchini Angola dhidi ya wapinzani katika mashindano ya CAF.

Hata hivyo, Yanga imekuwa na rekodi nzuri ya kuziondosha timu za Angola ilipokutana nazo katika mashindano ya CAF.

Rekodi zinaonyesha mwaka 2007, ilicheza dhidi ya Petro De Luanda katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kushinda kwa jumla ya mabao 3-2. Mchezo wa kwanza ugenini ilipoteza kwa mabao 2-0, nyumbani ikashinda 3-0.

Pia mwaka 2016, ilicheza dhidi ya Sagrada Esperansa na kuitoa kwa jumla ya mabao 2-1 kwenye Kombe la Shirikisho Afrika. Mechi ya nyumbani ilishinda mabao 2-0, ugenini ikapoteza kwa bao 1-0.

Katika mchezo uliopita wa ugenini, mabadiliko ya kikosi yaliyofanywa na kocha wa Yanga, Romain Folz kutoka kile kilichoifunga Simba bao 1-0 kwenye Ngao ya Jamii, yalimlipa na kuondoka na ushindi wenye rekodi. Mabadiliko hayo yalikuwa matatu, Bakari Mwamnyeto, Mohamed Doumbia na Clement Mzize walianza badala ya Dickson Job, Mudathir Yahya na Maxi Nzengeli. Job na Mudathir hawakucheza kabisa, lakini Maxi aliingia kipindi cha pili na kutoa pasi ya bao.

Jinsi timu ilivyocheza ikipoteza nafasi nyingi za wazi na kubanwa muda mrefu na Wiliete imefanya mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo kutofurahia, hata kama timu imejiweka pazuri kusonga mbele kwa hisia kwamba kama itaendelea kucheza hivyo ni ngumu kuhimili vishindo vya michuano hiyo.

Prince Dube alionekana kushangilia sana alipofunga bao la tatu, jambo ambalo wengine walilitafsiri kama alikuwa akifidia nafasi nyingi za wazi alizopoteza katika kipindi cha kwanza na hata alipoingia Celestin Ecua naye alionyesha kiwango cha kawaida na kuwa mchoyo wa pasi kwa wenzake, kitu kinachomuongezea presha Folz ambaye ni kocha mpya Yanga.

Jambo hilo la timu kucheza sivyo ndivyo, hata Folz amelishtukia na kukiri kwamba ana kazi kwa mechi zijazo ikiwamo za Ligi Kuu ili timu ifike mbali zaidi na kutimiza malengo waliyonayo.

“Matokeo ni mazuri, ingawa sio kama tulivyostahili, tunataka kufanya vizuri zaidi, wakati tunakwenda mapumziko tukiongoza 1-0, niliona haitoshi, lakini nashukuru kwa matokeo haya. Bado tupo katika kujenga timu lakini hatupo sehemu mbaya,” anasema Folz.

Hata hivyo, Yanga bado ina kazi ya kumalizia ili kwenda hatua inayofuata kwani baada ya mechi hiyo zitarudiana Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mshindi wa jumla anaenda raundi ya pili kucheza na mshindi kati ya Elgeco Plus ya Madagascar au Silver Striker ya Malawi. Folz na mastaa wa Yanga wana kibarua kwanza cha kucheza mechi ya Ligi keshokutwa Jumatano dhidi ya Pamba Jiji kabla ya kurudiana na Wiliete.

PRE 04

GABORONE UNITED 0-1 SIMBA

Bao pekee la Elie Mpanzu Kibisawala alilofunga kwa kichwa katika dakika ya 16 akiunganisha krosi ya nahodha, Shomari Kapombe limeipa Simba mwanzo mzuri wa 0-1 ikiwa ugenini, Botswana.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Obed Itani Chilume uliopo Francistown, Simba imekuwa na mwanzo mzuri katika hatua ya awali ya michuano hiyo, huku ikilenga kufika mbali zaidi baada ya msimu uliopita kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kabla ya kuingia kwa bao hilo, Simba ilionekana kupanga mashambulizi ambayo yalitibuliwa na Gaborone United, lakini mbinu za kocha Fadlu Davids kwa wachezaji wakiwamo nyota wapya kama Anthony Mligo na Naby Camara, uliifanya kuwa imara.

Simba iliingia katika mchezo huo bila ya kiungo wake mkabaji, Yusuph Kagoma anayeitumikia kadi nyekundu aliyoonyeshwa msimu uliopita katika fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, ndio maana Fadlu akaanza na Naby Camara kuchukua nafasi yake, huku Mligo akiwa beki wa kushoto. Kumbuka nyota hao wote ni wapya, huku Camara akiwa na uwezo wa kucheza pia beki wa kushoto mbali na eneo la kiungo.

Ushindi huo ni mwendelezo wa rekodi bora kwa Simba inapokuwa Botswana, kwani mara nne zote ilipocheza hapo katika michuano ya CAF haijapoteza, ikishinda tatu na sare moja.

Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2003, ilipokutana na BDF XI katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikashinda 1-3, kisha ikafuzu hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 4-1.

Mwaka 2021, Simba ilipambana na Jwaneng Galaxy katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ugenini ilishinda 2-0, lakini nyumbani ikafungwa 1-3, ikatolewa mashindanoni kwa bao la ugenini wakati matokeo yakiwa 3-3.

Baada ya hapo, mwaka 2024, Simba ilipokutana tena na Jwaneng Galaxy katika hatua ya makundi, ugenini zilitoka 0-0, ikaja kushinda nyumbani kwa mabao 6-0.

Simba na Gaborone United zinatarajiwa kurudiana Septemba 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar ambako mshindi wa jumla atafuzu hatua inayofuata kucheza na mshindi kati ya Simba Bhora ya Zimbabwe na Nsingizini Hotspurs kutoka Eswatini.

Kwa hapa, Simba ina mambo mawili ya kuingia nayo katika mechi ya marudiano, kwani licha ya kuwa na rekodi bora ya kutopoteza kwenye mechi 11 mfululizo za CAF ikiwa nyumbani kufuatia kushinda tisa na sare mbili tangu mara ya mwisho ifungwe 0-3 na Raja Casablanca Februari 18, 2023, ikumbukwe mwaka 2021 ilishinda ugenini nchini Botswana, ikaja kufungwa nyumbani na kutolewa.

Licha ya ushindi huo, Simba haikucheza ilivyotarajiwa na baadhi ya mashabiki walishindwa kujizuia na kutumia mitandao ya kijamii kuweka hisia zao, japo wengine wanafurahia kwa kuamini Kwa Mkapa Jumapili, Gaborone watazichezea nyingi.

PRE 03

AL MERREIKH 0-2 AZAM

Kocha Florent Ibenge ameanza vizuri kibarua katika Kombe la Shirikisho Afrika akiiongoza Azam kupata ushindi wa mabao 0-2 dhidi ya Al Merreikh Bentiu ugenini Sudan Kusini kwenye Uwanja wa Juba.

Mabao ya Feisal Salum  ‘Fei Toto’ katika dakika ya 45 na Jephte Kitambala dk68, yameipa mwanga Azam katika kuisaka rekodi mpya ya kucheza makundi ya michuano ya CAF mwa mara ya kwanza tangu kuasisiwa kwa klabu hiyo iliyopo Ligi Kuu Bara kuanzia msimu wa 2008-2009.

Rekodi zinaonyesha mara zote Azam iliposhiriki mashindano ya CAF, haijawahi kucheza hatua ya makundi ambapo sasa Ibenge ana kazi ya kufanya na kikosi hicho.

Kucheza ugenini na kushinda bila ya kuruhusu bao, huku timu ikicheza vizuri ikiwa na nyota kadhaa wapya sambamba na kipa chipukizi Zuber Foba, ni ishara kwamba Azam inaweza kushangaza msimu huu kwani hata ukiangalia wapinzani inaokwenda kukabiliana nao ikipenya hapa, inawamudu.

Timu hizo zinatarajiwa kurudiana Septemba 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar ambako mshindi wa jumla atakwenda kucheza hatua inayofuata dhidi ya mshindi kati ya AS Port ya Djibouti na KMKM kutoka Zanzibar.

“Ni jambo zuri kwetu kuanza vizuri, nadhani dakika 30 za kwanza tulikuwa na mchezo mzuri, baada ya hapo tukawaacha Al Merreikh waje na walijitahidi dakika 15 za mwisho kipindi cha kwanza.

“Tukiwa tunaongoza 1-0, nikafanya mabadiliko kidogo ya sehemu ambazo hazikuwa vizuri, tukarejea kipindi cha pili na kufunga bao jingine. Kwa leo nadhani tumepata ushindi wa kawaida kwani tumetengeneza nafasi nyingi.

“Jambo gumu katika mpira wa miguu ni kufunga lakini kuzuia ni rahisi, kwa hiyo tunapaswa kuimarisha hilo kwa sababu hii ni mara ya kwanza tunacheza mechi ya kimashindano na ilikuwa ngumu kufunga japo tulikuwa na uwezo wa kufunga zaidi. Tutaenda Chamazi kulifanyia kazi,” anasema Ibenge.

PRE 02

RAYON SPORTS 0-1 SINGIDA BLACK STARS

Kwa mara ya kwanza, Singida Black Stars ikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika, imepata ushindi wa bao 0-1 dhidi ya Rayon Sports kwenye Uwanja wa Kigali Pele nchini Rwanda.

Marouf Tchakei ndiye aliyewapa tabasamu mabingwa hao wa Kombe ka Kagame 2025 baada ya kufunga bao pekee dakika ya 22 akiunganisha kwa kichwa mpira wa frii-kiki uliopigwa na Clatous Chama.

Singida Black Stars inayofundishwa na Miguel Gamondi, kazi bado haijaisha, kwani kuna mchezo wa marudiano utakaofanyika Septemba 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar. Mshindi wa jumla anacheza dhidi ya mshindi kati ya Flambeau du Centre ya Burundi na Al Akhdar ya Libya.

Uwepo wa kikosi chenye wachezaji wenye uzoefu wa michuano ya kimataifa kama Chama na Khalid Aucho, pengine unaweza kuifanya Singida Black Stars kufuata njia za Namungo ambayo ilishiriki mara ya kwanza na ya pekee michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2021 ikacheza makundi licha ya kutofanya vizuri hatua hiyo.

Mtibwa Sugar, Biashara United na Coastal Union ambazo nazo zimewahi kushiriki michuano hiyo mara moja pekee kwa miaka ya hivi karibuni, ziliishia hatua za mwanzoni.

PRE 01

INSURANCE 2-0 MLANDEGE

Wakati wawakilishi wa Tanzania Bara wakianza vyema kwa kushinda mechi zao za ugenini, upande wa Mlandege ya Zanzibar, imekubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Ethiopian Insurance.

Mchezo huu uliofanyika Septemba 20, 2025 kwenye Uwanja wa Abebe Bikila, Adis Ababa, wenyeji walifunga mabao hayo kila kipindi na kuwapa nafasi ya kutoka kifua mbele kuelekea mchezo wa marudiano utakaofanyika Septemba 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar ambapo mshindi wa jumla atakwenda kukabiliana na mshindi kati ya APR ya Rwanda na Pyramids kutoka Misri.


Mlandege inarejea Zanzibar kwenye Uwanja wa New Amaan kujiuliza mbele ya wapinzani wao, huku ikiwa n amlima mrefu wa kuupanda kuvuka hatua inayofuata, kwani inahitaji ushindi wa zaidi ya mabao 2-0 iwapo inataka isonge mbele na hapo presha inapanda kwa benchi la ufundi chini ya Abdallah Mohammed ‘Baresi’ na mastaa wa timu hiyo wakiwamo wapya.