Huyu ndiye Hersi Said, Arafat Haji
Muktasari:
- Kuna makundi mawili kwenye kampeni hizo, wapo wagombea wa nafasi za Rais na makamu wake, pia kuna wagombea wa ujumbe wa kamati ya utendaji wakitafutwa watu watano kati ya 16 wanaogombea.
KAMPENI cha Uchaguzi mkuu wa Yanga zinaendelea, baada ya kufunguliwa juzi kila mgombea akipambana kuuza sera zake kuwania nafasi ya kuingia kwenye uongozi wa juu wa klabu hiyo.
Kuna makundi mawili kwenye kampeni hizo, wapo wagombea wa nafasi za Rais na makamu wake, pia kuna wagombea wa ujumbe wa kamati ya utendaji wakitafutwa watu watano kati ya 16 wanaogombea.
Hata hivyo nafasi mbili za juu za Rais na makamu wake hazitakuwa na shida kwani Rais anayetetea kiti chake na makamu wake Arafat Haji wao wataingia wakiwa wagombea pekee baada ya kukosekana watu wa kushindana nao.
HERSI SAID
Hersi anatetea kiti chake baada ya kuongoza muhula wa kwanza wa uongozi kwa miaka minne ya kwa mafanikio makubwa, kuanzia mwaka 2022 akiweka rekodi mbalimbali ndani na nje ya klabu hiyo.
Kitaaluma Hersi ni injinia wa mambo ya ujenzi pia anajihusisha na mambo ya biashara mbalimbali akianzia kwenye makampuni ya GSM ambayo kiuhalisia ndio yaliyomuibua na kuwa kiongozi wa klabu hiyo.
Hersi katika safari yake ya kuongoza Yanga metawaliwa na mapenzi kwea klabu hiyo, akianzia kuwa shabiki na baadaye mwanachama kisha kuingia katika uongozi baada ya makampuni ya GSM yalipoingia kuwekeza ndani ya klabu ambayo anaipenda.
Katika kipindi ambacho Hersi ameiongoza Yanga imekuwa ni klabu yenye mafanikio, ikiinuka kutoka kudorora kwa kiwango na kuja kuwa klabu shindani zaidi ndani ya Tanzania lakini pia Afrika Kiujumla.
Mbali na kuwa kiongozi wa Yanga, Hersi amefanikiwa kuitangaza Yanga kimataifa akiwa pia Mwenyekiti wa Umoja wa klabu Afrika (ACA), nafasi ambayo imempa mwanya wa kuingia kwenye kamati ya utendaji wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF)
Katika kipindi chake cha kwanza Yanga imechukua mataji matano ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara, mataji mawili ya Kombe la Shirikisho, ubingwa wa Muungano, Yanga pia ikichukua ngao mara nne. Kimataifa ikicheza fainalia ya Kombe la Shirikisho na ikicheza hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara moja.
Uwepo wa Hersi ndani ya Yanga ni kama uhakika wa ufadhili wa GSM ndani ya klabu hiyo ambapo, kigogo huyo amekuwa ni sehemu ya msukumo wa tajiri Ghalib Said Mohammed kuendelea kufanya makubwa ndani ya mabingwa hao.
Hersi ambaye ameonyesha uimara wa kuwa kiongozi mwenye msimamo pia ameisimamia Yanga kupita salama kwenye mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uongozi baada ya kuwa sehemu ya njia sahihi ya klabu hiyo kwenda kuongozwa kisasa, baada ya GSM kuileta kampuni ya La Liga kutoka Hispania kushauri njia salama ya kuibadilisha Yanga.
Hersi hatakuwa na mpinzani kwenye uchaguzi wa Yanga, kutakuwa na kura za ndio au hapana kutoka kwa wanachama ambao watapiga kura Agoti 2, 2026 katika mkutano mkuu wa uchaguzi wa klabu hiyo kuamua muhula wake wa pili wa kuiongoza klabu hiyo.
ARAFAT HAJI
Nafasi ya makamu wa Rais nayo ina mgombea mmoja kigogo mwingine mzito Arafat Haji, hakuna ambaye amejitokeza kuwania naye nafasi hiyo, hapa nako kutakuwa na kura ya ndio au hapana mchezo umekwisha.
Arafat kitaaluma ni mtaalamu wa fedha, akiwa na uzoefu wa kuongoza taasisi mbalimbali nchini, zikiwemo benki na zile za bima, akifanya kazi huko kwa takribani miaka 20, akiwahi pia kuwa mteule wa Rais kule Zanzibar pia na uzoefu wa biashara mbalimbali.
Kigogo huyu naye anagombea kutafuyta muhula wa pili wa uongozi ambapo katika kipichi cha awali anasifika kwa kuwa na misimamo thabiti kuongoza kuitetea klabu hiyo, anyeamini kwenye uwajibikaji, ushirikishwaji na kuongoza kwa matokeo yanayopimika, akiwa muumini wa kuongoza kwa uwazi.
Akiwa na elimu kiwango cha shahada ya uzamili ya MBA kwenye teknolojia ya habari na mawasiliano aliyoipata nchini England na shahada ya benki na fedha akiiapata Chuo cha IFM hapa nchini.
Arafat ni mwanachama na mwanamichezo mwenye mapenzi ya dhati na Yanga ambapo uwepo wake ndani ya klabu hiyo umekuwa ukinogesha kuwa sehemu ya Muungano kutokana na kuzaliwa na kukulia visiwani Zanzibar.
Kabla ya kuwa makamu wa Rais , Arafat aliwahi kushika nafasi ya mjumbe wa kamati ya utendaji katika utawala wa aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo Dk Mshindo Msolla, akiwahi pia kushiriki vyema juu ya mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshwaji wa klabu hiyo, aliwahi pia kupata nafasi ya kujengewa uwezo wa kuongoza klabu kupitia mafunzo yaliyoendeshwa na Shrikisho la Soka Kimataifa (FIFA) yaliyofanyika nchini Marekani.
Arafat amekuwa sio mtu kuongea sana lakini anasifika kwa kuwa mtu wa vitendo ndani ya klabu hiyo kwenye kupanga mambo mengi ya kimkakati ndani ya klabu hiyo akishirikiana vizuri na viongozi wake wa juu pamoja na sekretarieti ya klabu hiyo.
Wakati anaingia kwenye muhula wa kwanza Arafat alijitiwisha mzigo wa kuisimamia timu ya wasichana Yanga Princess, ambayo kwasasa imeendelea kupitia mabadiliko makubwa ya ubora, kutoka kuwa timi dhaifu mpaka kuwa ndani ya tatu bora ambapo sasa imebakiza kuanza kupata mataji pekee.
Dira ya Arafat ndani ya klabu hiyo ni kuona Yanga ikiendelea kuwa klabu kubwa ya kisasa inayojitegemea na yenye ushindani wa kudumu barani Afrika, pia kuhakikisha haitetereki katika usimamizi wa kifedha.
Arafat amekuwa akimalisha combo nzuri ya kiuongozi na Hersi ambapo kwenye eneo ambalo rais wake hayupo, klabu hiyo imeendelea kuwa kwenye usimamizi salama kutokana na ujuzi wa kiutawala kutoka kuziongoza taasisi mbalimbali.
Ni kiongozi anayejitoa katika matukio mengine nje ya klabu hiyo, ambapo hivi karibuni alionekana kwenye misiba tofauti ya klabu zingine zikiwemo Simba na Azam, licha ya tofauti za kiushindani.