Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NJIA NYEUPE : Tanzania imeamua kujinyima fursa ya kuibua vipaji

Muktasari:

Wakati nchi nyingine duniani zimejikita katika kuendeleza na kuvumbua vipaji vya vijana, Tanzania inafanya mambo ambayo yanakwenda kinyume na azma hiyo.

        TANZANIA bado ina safari ndefu ya kupata mafanikio ya kufanya vizuri katika michezo kimataifa kutokana na hatua ambazo zinachukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Wakati nchi nyingine duniani zimejikita katika kuendeleza na kuvumbua vipaji vya vijana, Tanzania inafanya mambo ambayo yanakwenda kinyume na azma hiyo.

Hivi karibuni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Anayeshuhulkia Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene alitangaza kuahirisha fainali za michezo ya Shule ya Msingi na Taaluma maarufu Umitashumta na ile ya Shule za Sekondari Tanzania yaani Umisseta.

Akitoa sababu za kuhairisha michuano hiyo iliyokuwa ifanyike jijini Mwanza, waziri huyo alisema hatua hiyo imechukuliwa ili wadau wafanikishe utengezaji wa madawati kwa shule za Tanzania.

Rais John Magufuli alitoa maagizo kwa wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa kuhakikisha kuwa shule za maeneo yao zinakuwa na madawati na hakuna mtoto anayekaa chini ifikapo Juni 30 mwaka huu.

Pamoja na kwamba suala la kuwa na madawati kwa wanafunzi wote ni jambo la msingi na muhimu katika nchi lakini ni vigumu kuahirishwa michezo ya shule za msingi na sekondari.

Ukizingatia hali halisi ni vigumu kuona uwiano juu ya wanafunzi waliokua washiriki michuano hiyo na walimu wachache waliokuwa wanawasimamia na utengenezaji wa madawati ya shule.

Katika hali halisi shughuli za utengenezaji wa madawati zingeachwa ziendelee zilivyo na huku michezo hiyo ya vijana wa shule ambayo matayarisho yake yalikuwa yameshakamilika ingeachwa ifanyike kama ilivyopangwa ili vijana wenye vipaji waweze kuibuliwa.

Hakuna njia ya mkato kwa taifa lolote kupata maendeleo katika michezo bila kuwekeza katika medani hiyo ambayo imezisaidia nchi nyingi kupata mafanikio ya watu binafsi na taifa kwa jumla.

Katika maisha ya sasa ya dunia, michezo si tu kwa ajili ya kujenga afya tu, bali pia ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa jumla kwa hiyo si jambo la kubeza.

Wanamichezo katika nchi wanazofanya vizuri wanalitangaza taifa lao duniani na kwa hiyo inasaidia katika kukuza uchumi wa nchi na kukuza utalii.

Lakini Tanzania inaonekana bado haijazinduka na inaichukulia michezo kama jambo ambalo halina maana yoyote wala uzito wowote na wanalichukulia kwa maana halisi ya neno hilo na wakiufuata msemo wa Kiswahili usemao “Kazi mbaya si mchezo mwema.”

Katika dunia ya sasa msemo huo wa Kiswahili wa kazi mbaya si mchezo mwema umepitwa na wakati kwani imedhihirika kuwa wanamichezo kwa nyakati hizi ndio watarajiwa wakubwa duniani kuliko watu walioajiriwa kwenye kazi ambazo zinaonekana ni kubwa duniani.

Mfano mzuri kuna baadhi ya wanasoka duniani ambao wanalipwa zaidi ya Pauni 200,000 kwa wiki ambao ni sawa na mshahara wa mwaka mzima wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la fedha la Kimataifa (IMF) ambalo ni shirika kubwa zaidi la kifedha duniani.

Kwa kuzingatia mfano huo utagundua kwamba michezo kwa wakati huu inalipa na nchi ikiwa na wanamichezo wanaofanya vizuri duniani inakuwa katika nafasi ya kuwa na kundi kubwa la matajiri.

Fikiria mfano kama Tanzania ingekuwa na hata wanasoka 100 tu wanaocheza soko la kulipwa Ulaya na kulipwa kati ya Dola 30,000 na 50,000 basi ingekuwa na kada nzuri ya watu ambao wangekuwa na vitega uchumi na kutoa ajira kwa watu kadhaa.

Lakini kufikia mambo kama hayo inaonekana ni ndoto kwa Tanzania na kwa utaratibu huu wa kufuta michezo ya shule ndoto hiyo itakuwa ya kudumu na hapana shaka yoyote nchi kupiga hatua kwenye sekta ya michezo ni jambo lisilotarajiwa.

Kuna haja ya Tanzania kuzinduka na kuipa michezo kipaumbele kwani hakuna taifa lililopata maendeleo katika sekta hiyo kwa njia ya mkato bila kupitia kwa kuendeleza vijana wake.

Hatua kama hizi zinazochukuliwa na Waziri Simbachawene ndizo kwa kiasi kikubwa zimetufikisha hapa kwa taifa letu kuweza kusonga mbele katika michezo ya kimataifa.

Hivi viongozi wetu hawaoni wivu kwa kile kinachofanywa na majirani zetu Kenya, Uganda kwa wanamichezo wao wanaposhinda tuzo mbalimbali?

Masoud Sanani ni mwandishi wa habari mwandamizi amewahi kufanya kazi Televisheni Zanzibar, Uhuru na Mzalendo, Business Times ( Mhariri mwanzilishi wa Spoti Starehe ) na Mwananchi. Alikua Mkurugenzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania ( TEF). Anapatikana email [email protected] simu 0712-020020.     

Kwa taarifa zaidi nunua gazeti lako la Mwanaspoti au soma mtandaoni kupitia www.epaper.mcl.co.tz