NJIA NYEUPE : Kwa hawa Mazembe, Simba wagange yajayo
Muktasari:
Ikiwa uongozi umeonyesha udhaifu au chuki ya mioyo yao wa kusajiliwa Hassan Kessy na Yanga hata kufikia hatua ya kumwekea pingamizi asicheze. Je, watu hao wanaweza kuwaambia mashabiki wao waishangilie Yanga?
“KATIKA makala yako ya Mwanaspoti ya Juni 23, mwaka huu isemayo: “ Jangwani giza halafu mwanga tena”. Nimeguswa na kipengele cha uzalendo usiwashinde. Hivi katika klabu ya Simba ni nani awezaye kuwashawishi mashabiki kuishangilia Yanga?
Ikiwa uongozi umeonyesha udhaifu au chuki ya mioyo yao wa kusajiliwa Hassan Kessy na Yanga hata kufikia hatua ya kumwekea pingamizi asicheze. Je, watu hao wanaweza kuwaambia mashabiki wao waishangilie Yanga?
“Ni vigumu mimi kuishangilia Yanga bora hata nife kama mnaita uzalendo huo umenishinda”.
“Ni kweli tunashauriwa kuacha mambo ya U-Simba na U-Yanga na kwenye mechi ya Yanga na Mazembe kwani, inapeperusha bendera yetu ya taifa”.
“Magomeni Mpira Pesa na Upanga Mpira na Maendeleo Ukawa. Mbona Jerry Murro haongei? Hatuwezi kuwashangilia watalii wa Uturuki”.
“Njoo uchukue jezi ya Mazembe kuna kijana wetu pale (Thomas Ulimwengu) anahitaji kushangiliwa na wazalendo.”
“Hakuna kitu kama hicho Simba tuwashangilie Yanga? Tutaona wao si wakimataifa hofu yao nini? Wapigwe tu.“
”Nawatakia timu Mazembe ushindi mnono dhidi ya Yanga, Mungu awapofushe macho zaidi Yanga wasione lango la Mazembe. Kama ulivyoandika Jangwani giza na iwe hivo’’.
Hayo ni baadhi ya maneno yalioandikwa katika ujumbe wa simu kutoka kwa wasomaji wa Gazeti la Mwanaspoti wakizungumzia juu ya makala yaliyotoka Alhamisi iliyopita ambayo ilikuwa na kipengele kinachowataka mashabiki wote wa Tanzania watakaoingia Uwanja wa Taifa kuona mechi ya Yanga na TP Mazembe kuishangilia Yanga na kusahau tofauti ya U-simba na U-yanga.
Hata hivyo, kutokana na ujumbe mwingi uliotumwa inaonyesha kuwa mashabiki wa Simba hawako radhi kuishangilia Yanga na wanadai kwamba, hawawezi kufanya jambo hilo.
Hata hivyo, mashabiki wa Yanga walifurahia hatua hiyo ya kutaka watani wao wawashangilie kwa kuwa ni jambo zuri na lina faida.
Hatua hii imezua tafakuri mpya kwa kufikiria kwamba iwapo watu wawili wanagombana na ugomvi wao umeshika kasi kwa kutupiana mateke na ngumi na ghafla akatokea chui mbele yao je watafanya nini?
Watu hao wataendelea kupigana na kuendeleza ugomvi wao au wataacha kupigana na kuungana ili kupambana na chui katika harakati za kuokoa maisha yao?
Kwa akili za kawaida watu hawa wataungana pamoja na kwamba, walikuwa maadui watapata urafiki usio rasmi ili kugombana na chui ambaye ni adui yao wote.
Ukitilia maanani mfano huo utaona kwamba wakati Yanga inacheza na Mazembe huku ikiwakilisha Tanzania, timu hiyo kutoka Congo DR inapaswa kuwa adui wa Watanzania wote.
Kwa hiyo sote tunapaswa kushirikiana kwa kila njia ili kuhakikisha Mazembe haifui dafu kwa timu ya Tanzania na inarudi kwao ikiwa mikono kichwani.
Kwa hiyo ni muhimu watazamaji wengi wakijitokeza Uwanja wa Taifa na kujifunga kibwebwe kuipa nguvu Yanga ili ijiwekee mazingira mazuri ya kusonga mbele katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
Hata hivyo, huo msaada wa mashabiki ni wa ziada tu kazi ya msingi na jukumu la kuifunga Mazembe katika mechi hiyo iko chini ya makocha, Hans Pluijm, Juma Mwambusi na Juma Pondamali na wachezaji wao kwa jinsi watakavyoonyesha umahiri uwanjani.
Mashabiki wapige kelele hata vifua vikauke kama wachezaji hawatacheza kwa umakini wa hali ya juu na kujituma haitasaidia kwani, Mazembe watachanua na kutoka uwanjani kifua mbele.
Huu ni wakati wa timu ya Yanga kujijengea rekodi mpya wa kuweza kuingia nusu fainali ya michuano hiyo au hata kufika fainali na kuweza kuchukua kombe hilo kwa mara ya kwanza.
Kwa Yanga sasa ambayo imeonesha kiwango cha kuridhisha katika michuano mbalimbali iliyoshiriki msimu huu, ina uwezo mkubwa wa kufanya vizuri katika mechi hiyo.
Suala la mahali pakukaa kwa mashabiki wa Yanga katika Uwanja wa Taifa ambao, wametakiwa na klabu yao kukaa mahala popote huku Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likipinga hatua hiyo linafaa litatuliwe vyema na pande hizo mbili ili lisije likaleta vurugu.
Masoud Sanani ni mwandishi wa habari mwandamizi amewahi kufanya kazi Televisheni Zanzibar, Uhuru na Mzalendo, Business Times (Mhariri mwanzilishi wa Spoti Starehe ) na Mwananchi. Alikua Mkurugenzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania ( TEF). email [email protected] simu 0712-020020.
Kwa taarifa zaidi nunua gazeti lako la Mwanaspoti au soma mtandaoni kupitia www.epaper.mcl.co.tz