Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NJIA NYEUPE : Baada ya uchaguzi, Yanga wajipange kuepuka utegemezi

Muktasari:

  • Uchaguzi huo ulifanyika baada ya kuwepo sarakasi za hapa na pale kati ya Yanga, Baraza la Michezo la Taifa [BMT] na Shirikisho la Soka [TFF] ambao awali walipanga uchaguzi huo ufanyike Juni 25, mwaka huu ukisimamiwa na vyombo hivyo.

KLABU ya Yanga ya Dar es Salaam juzi Jumamosi ilifanya uchaguzi mkuu kuwapata viongozi wake watakaoiongoza kwa miaka minne.

Uchaguzi huo ulifanyika baada ya kuwepo sarakasi za hapa na pale kati ya Yanga, Baraza la Michezo la Taifa [BMT] na Shirikisho la Soka [TFF] ambao awali walipanga uchaguzi huo ufanyike Juni 25, mwaka huu ukisimamiwa na vyombo hivyo.

Lakini Yanga waligeuza kibao na kueleza utafanywa na kamati yake ya uchaguzi na hatimaye wakaufanya Juni 11, mwaka huu, yaani juzi.

Viongozi waliochaguliwa ni Yusuf Manji, ambaye ameshinda kiti ya uenyekiti wakati Clement Sanga ameshinda kiti cha umakamu mwenyekiti.

Wengine wameshinda nafasi za ujumbe ambao ni Siza Augustino, Omary Said, Tobias Lingalangala, Salim Mkemi, Ayoub Nyenzi, Samuel Lukumay, Hashim Abdallah na Hussein Nyika.

Hatua hiyo ya uchaguzi wa viongozi imeondoa ombwe la uongozi lililodaiwa kuwepo na BMT iliyodai uongozi wa Yanga chini ya Manji ulikuwa umemaliza muda wake na hautambuliki tena.

Baada ya kufanyika uchaguzi huo ni wakati wa wanachama wa Yanga kutulia na kushirikiana na viongozi wao waliowachagua katika kuijenga klabu ambayo ina jukumu kubwa la kushiriki hatua ya makundi la Kombe la Shirikisho Afrika linalotarajiwa kuanza Juni 19, mwaka huu.

Hicho ndio kitakuwa kipimio cha kwanza cha uongozi wa Yanga baada ya kufanya vizuri msimu huu kwa kutwaa Ngao ya Hisani, Ubingwa wa Ligi Kuu na Ubingwa wa Kombe la FA.

Sasa Yanga inatakiwa itupe macho na masikio yake kwenye michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho ambayo inashirikisha timu ngumu za Bara la Afrika.

Umoja na Mshikamano

Viongozi wa Yanga na wanachama wana wajibu wa kuimarisha umoja na mshikamano kwani, ni jambo linalohitajika zaidi kwa sasa kuliko wakati mwingine wowote ule.

Waswahili husema Umoja ni nguvu na utengano ni dhaifu, kwa hiyo ili Yanga ipate mafanikio ni lazima iwe na umoja na mshikamano na iepuke migogoro ya aina yoyote ile.

Migogoro siku zote ni adui wa maendeleo na mahali inapokuwepo hapawezi kuota ladha ya mafanikio kwani ni muhimu na lazima kwa wanachama kuiepuka.

Viongozi wa Yanga wanapaswa kuwa makini katika uongozi wao kwa kufuata katiba ya klabu hiyo ili wasitoe mianya kwa wanachama wachache wasiokuwa na nia njema kuitumia kuleta migogoro.

Ni muhimu kwa viongozi hao kwa kushirikiana na wanachama wao kuhakikisha kwamba, wanakuwa na mipango na mikakati mizuri ili kuhakikisha wanaendana na kauli mbio yao ya Yanga daima, mbele nyuma mwiko.

Klabu kuwa Kampuni

Ni ukweli usiofichika kwamba kwa sasa klabu ya Yanga inamtegemea Manji kama mfadhili wa kuendesha shughuli mbalimbali za klabu.

Manji akisaidiwa na baadhi ya wanachama wenye uwezo wamekuwa wakiiendesha Yanga katika masuala yote yayohusu fedha, lakini utaratibu huo unafaa kutafutiwa mbadala.

Pamoja na Yanga kutegemea fedha za michango ya wanachama wake, lakini haina budi kutafuta njia ya kutafuta vyanzo vya kupata mapato ya fedha ili klabu iweze kujitegemea.

Hii ndio njia ya ukombozi itakayosaidia Yanga kuwa na fedha za kutosha na kuweza kuzitumia kwa maendeleo ya soka katika kipindi cha sasa fedha ndio msingi wake.

Mpira pesa, katika hali ya sasa bila ya kuwa na fedha ni vigumu kupata maendeleo ya maana katika soka hivyo ni lazima ijengwe misingi imara ya kuingiza fedha katika klabu.

Kumtegemea mtu kuendesha klabu si jambo la busara kwani, siku akijiweka pembeni mambo yatakuwa magumu.

Lakini klabu ikiwa katika mfumo wa kampuni na kuamua kufanya biashara mbalimbali na kuwekeza katika hisa na kuingiza mapato itakuwa na uhakika wa kuendesha mambo yake bila ya wasiwasi wowote wala kutegemea mtu.

Kwa hiyo ni wakati wa muafaka kwa uongozi wa Yanga unaoingia madarakani kukaa na wanachama wao kutafuta staili mpya ya kuendesha klabu ili iwe na uhakika wa kuwa na fedha za kutosha. Yanga ya sasa inatakiwa kujiendesha yenyewe na si kutegemea misaada ya watu wachache.

Masoud Sanani ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi amewahi kufanya kazi Televisheni Zanzibar,Uhuru na Mzalendo,Bussiness Times[Mhariri mwanzilishi wa Spoti Starehe] na Mwananchi. Alikuwa mkurugenzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania [TEF]. Anapatikana kwa email [email protected] simu 0712-020020

Kwa taarifa zaidi nunua gazeti lako la Mwanaspoti au soma mtandaoni kupitia www.epaper.mcl.co.tz