Ni vita ya vibopa dhidi ya makapuku Simba
Mwina Kaduguda
Muktasari:
Uongozi wa Hassan Mohamed Dalali ulioingia madarakani baada ya uchaguzi uliofanyika Desemba 3, 2006 ulichukua nafasi ya uongozi kipindi kifupi baada ya kuondolewa Kamati ya Muda iliyokuwa chini ya Michael Richard Wambura na Makamu wake akiwa Evance Aveva.
MGOGORO wa uchaguzi unaoendelea ndani ya Klabu ya Simba hivi sasa si tu kwamba unawahusu wagombea wa nafasi ya urais, bali pia ni wa makundi mawili yaliyojibainisha waziwazi.
Ni baina ya wanaodaiwa kuwa ni wenye nacho (vibopa) dhidi ya wale wanaoonekana kuwa hawana kitu (makapuku) ndani ya klabu hiyo.
Ninathubutu kutoa kauli hii kufuatia malolongo wa matamko mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa ama na wagombea wa nafasi hiyo au wanachama wa Simba kwa nyakati tofauti kupitia vyombo vya habari, kwa upande mmoja na Kamati ya Uchaguzi wa klabu hiyo, kwa upande wa pili.
Aidha, matamko hayo ambayo yamekuwa yakiwachanganya wanachama na mashabiki “kindakindaki” wa klabu hiyo waliotapakaa kila kona ya nchi yetu, yamekuwa yakiandamana na matukio ambayo yanadhihirisha kuwa ni vita ya mafahari wawili ambao wameigawa Simba katika makundi ya matajiri na masikini.
Ama kwa hakika, haihitaji kuwa Profesa wa Chuo Kikuu kugundua kwamba ugomvi huu unaoendelea katika klabu hiyo yenye makao yake Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam haukuanzia kwenye uchaguzi bali ni visasi vilivyokuwa vimefichika ndani ya mioyo ya wahusika ambao awali walikuwa kitu kimoja.
Uongozi wa Hassan Mohamed Dalali ulioingia madarakani baada ya uchaguzi uliofanyika Desemba 3, 2006 ulichukua nafasi ya uongozi kipindi kifupi baada ya kuondolewa Kamati ya Muda iliyokuwa chini ya Michael Richard Wambura na Makamu wake akiwa Evance Aveva.
Kamati hiyo iliachia ngazi baada ya kutokea mtafaruku miongoni mwa vinara wa kundi la Friends of Simba uliowahusisha Wambura kwa upande mmoja dhidi ya wanachama wengine wa kundi hilo lenye ushawishi mkubwa ndani ya klabu kwa upande wa pili. Ndipo Baraza la Wazee likashika hatamu za uongozi mpaka uchaguzi ulipofanyika.
Busara inaelekeza kwamba haipaswi kuyabebea bango mabaya yaliyowafarakanisha katika mchakato wa kuiongoza klabu katika kipindi au vipindi vilivyopita, kwa sababu kuwekeana visasi, nongwa na kuendeleza chuki, kutaiangamiza Simba. Hivyo basi tunapaswa kuheshimu na kuenzi mchango wa kila mmoja na kurekebisha upungufu ili kuhifadhi na kudumisha miiko ya Simba.
Moja ya kaulimbiu za Simba ambayo imekuwa mithili ya kiapo cha wakuu wa nchi “wateule” ni kauli isemayo “NGUVU MOJA”. Lakini kwa hali ilivyo hivi sasa, Simba hakuna nguvu moja bali kuna makundi yanayopingana, kuumbuana na kudhalilishana hadharani hali ambayo ni kinyume na miiko na maadili yaliyowekwa na waasisi wa klabu.
Nasisitiza kuwa tatizo la Simba si kiongozi tajiri wala masikini au kundi fulani, bali ni kiongozi anayeweza kurejesha amani, upendo na mshikamano. Vibopa wamejenga hisia kwamba Simba haiwezi kwenda bila matajiri na kwa mantiki hiyo wao ndio wanaostahili kuongoza.
Wambura naye kupitia kundi la Taleban ameifanya agenda ya kuongoza Simba kuwa ni ya makapuku ambao hawatakuwa na chao endapo vibopa wataipora timu na kuificha magorofani. Ninamalizia kwa kuwakumbusha wanachama wa Simba kauli ya wahenga isemayo ‘Ni kituko na aibu kwa wanaojenga nyumba moja kugombea fito’.
Simba tukae pamoja matatizo yetu tusiyatoe hadharani. Vibopa na makapuku wote ni muhimu kwa maendeleo ya klabu. Mungu ibariki Simba, Amina.
*Mwandishi wa makala hii aliwahi kuwa Kocha Msaidizi wa Simba na kisha Katibu Mkuu.