Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Namna mpira wa mikono unavyokua Zanzibar

MIKONO Pict

Muktasari:

  • Mafanikio hayo ni miongoni mwa ishara za kukua kwa mchezo huo visiwani hapa, ambao awali haukuwa na mwamko mkubwa kwa wananchi.

TIMU za mpira wa mikono Zanzibar zimeendelea kuonyesha ushindani mkubwa katika mashindano mbalimbali, kuanzia ngazi ya shule, klabu hadi mashindano ya kitaifa na kikanda.

Mafanikio hayo ni miongoni mwa ishara za kukua kwa mchezo huo visiwani hapa, ambao awali haukuwa na mwamko mkubwa kwa wananchi.

Kwa sasa, wadau na wafuasi wa mchezo huo wamekuwa wakishuhudia timu za Zanzibar zikionyesha kiwango kizuri, hasa katika mashindano ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Mabadiliko hayo yamechangiwa na juhudi za watu mbalimbali wanaojitolea kuukuza mchezo huo, wakiwemo makocha wanaokuza vipaji vya vijana.

Miongoni mwa watu waliochangia maendeleo hayo ni Kocha Kombo Ali Kombo, ambaye amekuwa akitumia muda na maarifa yake kufundisha mchezo huo katika makundi na madaraja mbalimbali.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kombo anasema mchango wake katika kuendeleza mpira wa mikono hauishii kwenye ukocha pekee, pia unatokana na uzoefu alioupata akiwa mchezaji na kushiriki mashindano mbalimbali, kuanzia ngazi ya shule, klabu hadi timu za taifa.

Anasema uzoefu huo umemjengea uelewa mpana kuhusu mchezo huo na kumhamasisha kuingia kwenye ukocha ili kutumia maarifa yake kukuza vipaji vya wengine.

“Mchango wangu hauishii katika ukocha pekee, kwani niliwahi pia kucheza mchezo huu katika mashindano mbalimbali, kuanzia ngazi ya shule, klabu hadi timu za taifa,” anasema.

Kwa sasa, Kombo ni miongoni mwa makocha wanaohudumu katika kambi ya timu ya taifa ya Tanzania, huku pia akiwa kocha wa timu ya JKU ya Zanzibar.


MIKO 01

MAPAMBANO YANAVYOZAA MATUNDA

Akizungumzia maendeleo ya mchezo huo, anasema juhudi ambazo amekuwa akizifanya kwa kushirikiana na wadau wengine zimeanza kuonyesha matokeo chanya, hasa kutokana na ongezeko la watoto na vijana wa rika mbalimbali wanaojitokeza kujifunza na kucheza mchezo huo.

Anasema awali haukuwa maarufu katika shule na maeneo ya mitaani, lakini kwa sasa mwamko umeongezeka na kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.

Anabainisha miongoni mwa mabadiliko makubwa aliyoyashuhudia ni kuvunjika kwa dhana iliyokuwepo, mpira wa mikono ni mchezo wa wanawake pekee.

Kwa sasa wanaume wengi wameanza kuupenda, kujifunza na kushiriki katika mashindano mbalimbali.


SAFARI YAKE ILIVYOANZA

Akielezea namna alivyoanza kuupenda mchezo huo, Kombo anasema walimu wa shule za msingi ndio waliokuwa chachu ya safari yake, akiwataja Mwalimu Sara, Juma na Mussa Abdul Rabi Fadhil wa Shule ya Msingi Mwanakwerekwe kuwa miongoni mwa watu waliomhamasisha.

Anasema alianza kucheza mchezo huo akiwa mwanafunzi wa darasa la tatu; “Mimi nimeanza kucheza mchezo huu nikiwa darasa la tatu Shule ya Msingi Mwanakwerekwe E. Baadaye niliendelea nao hadi sekondari katika Shule ya Mwanakwerekwe A,” anasema.

Akiwa katika ngazi ya shule, alishiriki mashindano mbalimbali yakiwemo Elimu Bila Malipo, UMISSETA na FEASSA (Michezo ya Shule za Sekondari Afrika Mashariki).

Baadaye aliendelea kucheza mchezo huo katika timu za Nyuki na JKU, huku safari yake ya timu za taifa Zanzibar ikipitia makundi ya umri wa miaka 15, 17 na 19 kabla ya kufikia timu za wakubwa za Zanzibar na Tanzania.

Katika kipindi chake cha uchezaji, Kombo anasema alipata nafasi ya kutwaa mataji mbalimbali katika mashindano ya Elimu Bila Malipo, UMISSETA, FEASSA, East Africa Clubs Championship (Youth), Ligi Kuu ya Zanzibar, Ligi ya Muungano na Klabu Bingwa Tanzania.

Mafanikio hayo, kwa mujibu wake, yamempa msingi mzuri wa kuelewa changamoto na mahitaji ya wachezaji, jambo linalomsaidia katika kazi yake ya ukocha.


MIKO 02

MIKAKATI YA KUENDELEZA MCHEZO

Akizungumzia mipango ya kuufikisha mpira wa mikono katika hatua nyingine, Kombo anasema kuna mikakati mbalimbali inayolenga kuimarisha maendeleo yake, hususan katika kukuza vipaji vya watoto na vijana.

Anataja vipaumbele kuwa ni kuendeleza programu za kukuza vipaji, kuongeza idadi ya mashindano katika ngazi mbalimbali na kuanzisha ligi maalumu zitakazowapa wachezaji nafasi ya kuonesha uwezo wao, kupata uzoefu na kuimarisha viwango vyao.

Anasema hatua hizo ni muhimu katika kujenga msingi imara wa mchezo huo, huku zikiwapa vijana fursa ya kuonesha vipaji vyao na kujiandaa kwa mashindano makubwa zaidi.


MABADILIKO YANAYOONEKANA

Kombo anasema mpira wa mikono Zanzibar umepiga hatua kutokana na kuongezeka kwa mwamko miongoni mwa vijana, uwepo wa vituo vya kufundishia na shule nyingi kuanza kuhamasisha wanafunzi kushiriki katika mchezo huo.

Anabainisha mabadiliko hayo yanaonyesha juhudi za wadau katika kuutangaza na kuuendeleza mchezo huo zimeanza kuzaa matunda, ingawa bado kuna mambo yanayohitaji kufanyiwa kazi ili kuufikisha katika kiwango cha juu zaidi.


MIKO 03

LIGI YA KUDUMU MUHIMU

Akizungumzia maeneo yanayohitaji maboresho, Kombo anasisitiza umuhimu wa kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa wadau, kuanzia ngazi ya shule hadi klabu.

Pia anataja umuhimu wa kuandaa mafunzo ya mara kwa mara kwa wachezaji na makocha ili kuongeza ujuzi na maarifa ya kiufundi, yatakayowawezesha kukabiliana na ushindani wa mashindano mbalimbali.

Hata hivyo, anasema changamoto kubwa inayohitaji kupatiwa ufumbuzi ni kukosekana kwa ligi maalumu ya mpira wa mikono Zanzibar, hali inayowafanya wachezaji kukosa jukwaa la kudumu la kuonyesha uwezo wao na kuendeleza vipaji.

Anatoa wito kwa wadau na mamlaka husika kuweka mikakati ya kuanzisha ligi ya kudumu, akiamini hatua hiyo itaimarisha ushindani, kuongeza uzoefu kwa wachezaji na kuvutia mashabiki wengi zaidi.


VIJANA WAPEWA WITO

Katika hatua nyingine, Kombo amewahimiza vijana kujitokeza kujifunza na kucheza mpira wa mikono na mchezo huo una fursa nyingi kwa wale wanaojituma na kuwa na nidhamu.

“Nawaomba vijana wajifunze kucheza mpira wa mikono kwa sababu ni mchezo kama michezo mingine na una fursa nyingi. Vijana wengi wamepata nafasi za kusajiliwa katika taasisi mbalimbali kupitia mchezo huu,” anasema.

Akizungumzia hatua zinazochukuliwa kuongeza ujuzi kwa wachezaji na makocha, Kombo anasema kwa sasa wameandaa programu ya Handball Clinic inayolenga kuwajengea uwezo wadau hao.

Anasema programu hiyo pia inanufaika na uwepo wa wataalamu kutoka nje ya Tanzania ambao hutoa mafunzo na msaada wa kitaalamu kwa wachezaji na makocha.

Kwa mujibu wake, programu hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha mchezo wa mpira wa mikono unaendelea kukua, huku vijana wakipata maarifa na ujuzi utakaowawezesha kushindana katika viwango vya juu zaidi.