KWA miaka inayokaribia saba ndani ya Yanga, Bakari Mwamnyeto amepitia nyakati tofauti katika maisha yake ya soka, kutoka furaha ya kubeba mataji hadi vipindi vigumu vilivyomlazimu kutulia, kutafakari na kujitafuta upya.
Lakini, pamoja na yote hayo, kuna jambo moja ambalo beki huyo wa kati na nahodha wa Yanga anasema halijawahi kubadilika ndani yake; uaminifu kwa klabu iliyompa nafasi, imani na kumfanya kuwa mmoja wa viongozi muhimu katika kikosi hicho.
Mwamnyeto anasema tangu aliposajiliwa Yanga 2020 amekuwa akiichukulia klabu hiyo kama familia yake jambo linalomfanya asiwe tayari kufanya chochote ambacho kinaweza kuichafua au kuihujumu timu hiyo.
“Katika maisha yangu ya mpira sijawahi kufanya kitu kama hicho. Napenda haki na napenda kitu ninachofanya, kwa hiyo siwezi hata siku moja kujaribu kufanya kitu kama hicho. Yanga wameniamini tangu miaka yote mpaka sasa hivi,” anasema Mwamnyeto.
Anaongeza: “Hawa ndio mabosi zangu, ndio watu walionisajili mpaka sasa hivi, kwa hiyo hii ndiyo familia yangu.”
Huo ndio msimamo wa nahodha huyo ambaye anasema hata anapokutana na lawama kutoka kwa mashabiki, huwa hazichukulii kwa namna mbaya bali sehemu ya jukumu alilobeba kutokana na nafasi yake ya uongozi. “Napenda sana nisemwe mimi kuliko mtu mwingine kwa sababu mimi ndiye kapteni wa timu na kiongozi wao. Hata ningepewa alama, napenda nipewe mimi kuliko mtu wote mwingine. Kwangu mimi naona hicho ni kitu kinachoniinua zaidi kwa asilimia 100,” anasema.
Msimu huu Yanga imeongeza nguvu katika maeneo mbalimbali ya kikosi, ikiwamo safu ya ulinzi ambako uwepo umeongeza ushindani wa nafasi za kucheza. Hata hivyo, Mwamnyeto anasema hajawahi kuutazama ushindani wa nafasi kama vita binafsi, bali anauona kama sehemu ya safari ya timu kuelekea malengo yake.
Anasema kinachompa furaha ni kuona wachezaji wapya wakifika na kuzoea mazingira ya timu kwa haraka, kwa sababu hilo huongeza nguvu ya kikosi kizima. “Katika timu nikiwepo, huwa siangalii ushindani, naangalia malengo ya timu. Naweza nikacheza mimi hapa timu ikachukua ubingwa, anaweza akacheza Job timu ikachukua ubingwa,”€ anasema na kuongeza:
“Yeyote ambaye ameitwa au amesajiliwa hapa, kikubwa ni kuweza kumpokea vizuri na kila mechi kushinda au kushindana. Masuala ya kucheza anaachiwa kocha.”
Kama nahodha, Mwamnyeto anajua presha inayokuja pamoja na michezo mikubwa, hasa pale Yanga inapokuwa ikielekea katika mechi ambayo inaweza kuamua hatua inayofuata katika mashindano.
Anasema kabla ya michezo migumu, wachezaji hukutana, kujadili na kuweka wazi kile wanachotaka kukifikia. “Jambo la kwanza huwa naongea na wenzangu na kujua malengo ya mechi ambayo tunakwenda kuifuata. Kama ni mechi kama hii (Dabi ya Kariakoo), muda mwingi tunafanya sana vikao na kukaa wenyewe kwa wenyewe,” anasema.
“Tunajua hapa ni nyumbani na mechi hii ndiyo mechi yetu ambayo inaweza kutufanya sisi tukaelekea hatua nyingine. Kwa hiyo ni lazima nawaambia wenzangu tupate matokeo, tuweze kwenda hatua nyingine.”
Mwamnyeto anasema jukumu la nahodha si kuvaa kitambaa tu mkononi, bali kuhakikisha wachezaji wanakuwa na picha moja kabla ya kuingia uwanjani.
Mwamnyeto pia anafunguka kuhusu namna anavyokabiliana na vipindi vigumu katika soka, akisema hakuna mchezaji anayepitia maisha yote ya soka bila kukutana na changamoto.
Anasema siri yake imekuwa kutokufanya maamuzi kwa hasira au presha, bali kujipa muda wa kutulia na kutafuta sehemu ambayo anapaswa kurekebisha.
“Jambo la kwanza ni utulivu wa akili wa kimwili na wa kifikra. Sitaki kufanya maamuzi ambayo baadaye yanaweza kunigharimu mimi au kumgharimu mtu mwingine,” anasema na kuongeza:
“Natulia, nafikiria nimekosea wapi, sehemu gani nirekebishe na sehemu gani niweze kuwa bora zaidi. Hicho ndicho kitu ninacho fikiria kwa dakika nyingi sana.”
Mwamnyeto anasema falsafa hiyo haimhusu mpira pekee, bali hata maisha yake kwa ujumla.
“Katika mpira au katika maisha kuna kupanda na kushuka. Ukishuka usijilaumu, jipe moyo, nadhani utaweza kuinuka kama sasa hivi nimeinuka, namshukuru Mwenyezi Mungu,” anasema beki huyo wa zamani wa Coastal Union.
Miongoni mwa kumbukumbu zinazomfurahisha zaidi Mwamnyeto katika maisha yake ya soka akiwa na timu hiyo ya Wananchi ni bao alilofunga msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba katika sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbeni, jijini Dar es Salaam.
Kwa beki huyo, bao hilo lilikuwa na uzito wa kipekee kwa sababu lilikuwa la kwanza kwake katika dabi dhidi ya wapinzani wao wakubwa.
“Nilijisikia vizuri. Katika dabi zangu zote zilizopita, nadhani sasa nimefikisha dabi 10 au nimepitisha, lile ndilo lilikuwa goli langu la kwanza kucheza na kuwafunga Simba,” anasema.
Anaongeza kuwa furaha hiyo haikuishia kwake pekee, bali iliifikia hata familia yake akisema: “Nilijisikia vizuri zaidi na si mimi tu, hata familia yangu ilijisikia vizuri.”€
Mbali na mambo ya uongozi na maisha ya soka uwanjani, Mwamnyeto ana upande mwingine unaoonyesha namna anavyolichukulia suala la vifaa vya michezo kwa umakini.
Beki huyo anasema anatumia viatu vya Nike, ukubwa namba 10 na kwa msimu mzima anaweza kutumia hadi jozi 10 kulingana na mahitaji ya mashindano na aina ya uwanja.
Anasema mara nyingi hununua viatu hivyo nje ya Tanzania kwa sababu ya kutafuta ubora unaoendana na mahitaji yake.
Anafafanua kuwa si lazima kila mechi atumie kiatu kilekile kwa sababu aina ya uwanja, mashindano na mazingira ya mchezo vinaweza kumlazimu kubadilisha.
Kuna sehemu nyingine inaweza kuwa timu ya taifa nina kiatu kingine, ligi hapa najua naweza kuchezea Chamazi kiatu kingine, nikachezea Zanzibar kiatu kingine. Inategemea na uwanja na jinsi ya mechi ninayojiandaa nayo, anasema.
Licha ya kuwa mchezaji anayejulikana, Mwamnyeto anasema kama asingekuwa mwa nasoka huenda angejikita katika biashara.
Lakini anapozungumzia mtu aliyemjenga zaidi nje ya uwanja, anamtaja baba yake, ambaye anamuelezea kama mtu mpole na mkarimu aliyekuwa na mchango mkubwa katika kumfundisha misingi ya maisha.
Anasema wakati wa mapumziko hutumia muda mwingi akiwa na familia yake, mara nyingi akielekea Tanga kukaa na wazazi na ndugu zake.
“Naumia sana kwa ajili ya familia yangu,” anasema.
Mwamnyeto anakumbuka ushauri wa baba yake ambao mpaka leo bado anauishi, hasa kuhusu namna ya kuishi na watu.
“Ananiambia vitu vingi sana mpaka leo navishika katika misemo yake la kwanza, usigombane na mtu yeyote. Mtu akitaka kukukera usiweze kugombana naye, jambo lingine ni wachezaji wote unaokuwa nao uwaone sawa, usibague huyu wala huyu kingine ni kuheshimu kila mtu,” anasema.
Uhusiano wake na wachezaji wenzake pia ni sehemu ya nguvu ya Mwamnyeto ndani ya Yanga huku akimtaja mlinda mlango Djigui Diarra kama mmoja wa watu ambao amekuwa na mawasiliano mazuri nao licha ya kuwa mara nyingi wanakutana katika mazingira tofauti ya uwanjani.
Anasema mawasiliano yao hayaishii uwanjani, kwani hata nje ya uwanja hupigiana simu na kujadili mambo mbalimbali yanayohusu timu.
“Ni jambo zuri sana. Djigui ni mtu ambaye muda mwingi tunaasiliana. Ingawa huwa tunagongana, muda mwingi tunapigiana simu,” anasema na kuongeza:
“Uwanjani namwambia usiongee kwa sauti ndogo, wewe kipa upo nyuma, sisi tunaiangalia mpira tu kwa hiyo akiongea kwa sauti ni rahisi kujua anataka anataka kitu gani.”€
Msimu huu Mwamnyeto anaamini malengo ya Yanga yanaweza kutimia endapo kikosi kitaendelea kushikamana na kuelewana.
Nahodha huyo anasisitiza kuwa msingi wa safari yao ni umoja, nidhamu na kila mchezaji kuweka maslahi ya timu mbele ya maslahi binafsi.
“Bila wasiwasi, tukiwa pamoja na kuweza kuelewana, kila kitu kinaweza kutimia,” anasema.
Mwamnyeto anasema safari yake ya karibu miaka saba Yanga haijatawaliwa na soka pekee, bali pia imekuwa shule ya uongozi, uvumilivu, uaminifu na namna ya kubeba majukumu wakati wa furaha na wakati wa changamoto.
Na sasa, akiwa nahodha, jukumu lake ni kuliongoza jahazi la Yanga huku akisisitiza kuwa ubingwa na mafanikio ya timu ndiyo yanayopaswa kuwa mbele kuliko mafanikio ya mchezaji mmoja mmoja.