Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mitihani minne inayomsubiri Senaf Simba Queens

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo raia wa Ethiopia ameanza ligi kwa kasi, akifunga bao muhimu kwenye nusu fainali ya Ngao ya Jamii na kuonyesha dalili kwamba anaweza kuwa mmoja wa wachezaji watakaobeba matarajio ya Wekundu hao wa Msimbazi msimu huu kulitetea taji la ligi.

KAMA kuna mchezaji mpya ambaye ameanza kuonyesha ubora wake mapema ndani ya kikosi cha Simba Queens, miongoni mwao yupo Senaf Demise.

Mshambuliaji huyo raia wa Ethiopia ameanza ligi kwa kasi, akifunga bao muhimu kwenye nusu fainali ya Ngao ya Jamii na kuonyesha dalili kwamba anaweza kuwa mmoja wa wachezaji watakaobeba matarajio ya Wekundu hao wa Msimbazi msimu huu kulitetea taji la ligi.

Senaf alifunga bao la pili katika ushindi wa Simba Queens wa mabao 3-0 dhidi ya Yanga Princess kwenye nusu fainali ya Ngao ya Jamii, matokeo yaliyoipeleka timu hiyo fainali ambapo ilikutana na JKT Queens.

Bao hilo lilikuwa muhimu kwake binafsi kwa sababu lilikuja baada ya kocha Mussa Hassan ‘Mgosi’ kumpa mazoezi maalum kwa siku nne mfululizo, yakilenga kumuongezea kujiamini mbele ya wapinzani kama Yanga.


ALIPOANZIA

Kabla ya kutua Simba, alikuwa sehemu ya kikosi cha CBE ya Ethiopia ambako aliacha rekodi iliyomfanya avutie macho ya klabu mbalimbali ikiwemo Simba ambayo ilipambana kumpata kwa miaka mingi.

Msimu wa 2022/23 akiwa Mechal, alifunga mabao 16 katika Ligi Kuu ya Wanawake Ethiopia, akimaliza nyuma ya Loza Abera na Aregash Kalsa aliyewahi kukipiga Yanga Princess msimu uliopita waliomaliza kileleni kwa mabao 23 kila mmoja.

Mwaka 2024 akiwa CBE, alimaliza mfungaji bora wa mashindano ya CECAFA ya kuwania Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake akiweka kambani mabao sita.

Katika mashindano hayo, Senaf alianza kwa kufunga bao katika ushindi wa CBE wa mabao 3-2 dhidi ya Rayon Sports, kisha akafunga mawili kwenye ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Yei Joint Stars.

Alimalizia kwa kufunga bao la ushindi dakika ya 79 dhidi ya Kenya Police Bullets kwenye fainali, bao lililoipa CBE ubingwa na tiketi ya kwanza ya kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika katika historia ya klabu hiyo.

REKODI ZA SHIKANGWA

Hapo ndipo mtihani wake wa kwanza unapoanzia. Mshambuliaji huyo alisajiliwa kuziba nafasi ya aliyewahi kuwa straika wa Simba, Jentrix Shikangwa ambaye kwa sasa anakipiga FC Masar ya Misri.

Mtihani wa kwanza ni kuziba pengo la Shikangwa. Kwa misimu minne aliyoitumikia Simba, Shikangwa alitengeneza jina kubwa. Msimu wake wa kwanza 2022/23 aliibuka mfungaji bora wa ligi kwa mabao 17, msimu uliofuata akafunga 12 katika mechi 10 za mashindano yote, kabla ya 2024/25 kupachika mabao 24 na msimu wa 2025/26 alifunga 16, akisaidia Simba kurejea kwenye mashindano ya kimataifa baada ya kutwaa ubingwa wa ligi.

Kuondoka kwa Shikangwa kunaacha nafasi kubwa kwenye safu ya ushambuliaji, lakini pia kunampa Senaf nafasi ya kujenga jina lake.

Hata hivyo ubora wa Shikangwa kwa kushirikiana na washambuliaji wengine kama Aisha Mnunka, Shelda Boniface, Elizabeth Wambui walitengeneza safu bora ya ushambuliaji ya timu hiyo.


PRESHA YA USAJILI

Mtihani wa pili ni kubeba presha ya usajili mkubwa.Simba haikumsajili kwa bahati. Klabu hiyo ilimfuatilia kwa zaidi ya mwaka mmoja na awali dili lilishindikana kutokana na Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kutokamilika kwa wakati.

Baada ya hapo alirejea Ethiopia na kujiunga na Mechal kwa mkataba wa miezi sita lakini msimu wake ukaathiriwa na majeraha na baadae Simba ikarudi mezani na kufanikisha usajili wake wa mwaka mmoja. Hivyo kitendo cha viongozi wa Simba kupambana naye kumpata hivyo kila bao atakalofunga litakuwa na maana kubwa kwa mashabiki wa timu hiyo.

Lakini pia tayari mechi mbili tu za Ngao ya Jamii alizocheza ameonyesha kiwango kilichowafanya mashabiki waondoke na jina lake midomoni mwao hivyo matarajio yao makubwa ni kuona nyota huyo anaweza kuwa suluhisho la muda mrefu kwenye safu ya mbele, hasa kwenye michezo mikubwa ambayo Simba Queens italazimika kushinda ili kurejesha utawala wake ndani ya soka la wanawake Tanzania.


REKODI ZA WAGENI

Ni baadhi ya wachezaji wachache wa kigeni waliosajiliwa na timu hiyo wakafanya vizuri kikosini hapo wengi walishindwa kuonyesha ubora wao kutokana na presha ya Ligi.

Asha Djafar aliwahi kuwa miongoni mwa wageni waliofanya vizuri zaidi, akitwaa Kiatu cha Dhahabu msimu wa 2021/22 akifunga mabao 27.

Msimu uliofuata Shikangwa alifunga mabao 17 na kuwa na muendelezo wa kufunga kwa misimu minne mfululizo.

Kwa miaka ya hivi karibuni mshambuliaji raia wa Kenya, Cynthia Musungu alishindwa kuonyesha kiwango bora Simba kutokana na changamoto za majeraha yaliyomuweka nje karibu msimu mzima. Wengine walioshindwa kuonyesha makali yao kwenye safu ya ushambuliaji kwa miaka ya hivi karibuni ni Precious Christopher aliyefunga bao moja katika mechi 12 akiwa Simba msimu wa 2024/25 kabla ya kurejea Yanga.

Zawadi Usananse ambaye alisajiliwa msimu uliopita akitokea AS Kigali ya kwao Rwanda kwa mkataba wa mwaka mmoja, lakini alishindwa kupata nafasi mbele ya Shikangwa akianzia benchi.Msimu mzima mshambuliaji huyo alifunga mabao sita.

Hii ndiyo changamoto nyingine inayomsubiri Senaf kuvunja rekodi za washambuliaji wa kigeni kwa miaka ya hivi karibuni.


MSIKIE MGOSI

Kocha wa Simba Queens, Mussa Hassan 'Mgosi' anasema Senaf ni mshambuliaji mzuri ambaye kama ataendelea kuonyesha ubora wake kwa kushirikiana na wenzake anaweza kuisaidia kwa kiasi kikubwa timu hiyo.

"Tuna safu bora ya ushambuliaji ambayo kama itaonyesha makali yake kwa muendelezo inaweza kuwa tishio, Senaf ni mchezaji mzuri ambaye kwa kushirikiana na wenzake wanaweza kutengeneza makali kule mbele."