Miaka 125 ya kukumbukwa… Brighton ilivyokaribia kufa hadi kuichapa Arsenal
Muktasari:
- Miaka kadhaa iliyopita ilikuwa ikipigania kuendelea kuwepo, ikipoteza uwanja wake, ikicheza mbali na nyumbani na kukabiliwa na hatari ya kushuka kabisa kutoka kwenye Football League.
BRIGHTON, ENGLAND; KAMA kuna klabu ambayo inastahili kuadhimisha miaka 125 kwa mbwembwe, basi Brighton & Hove Albion ina sababu zote.
Miaka kadhaa iliyopita ilikuwa ikipigania kuendelea kuwepo, ikipoteza uwanja wake, ikicheza mbali na nyumbani na kukabiliwa na hatari ya kushuka kabisa kutoka kwenye Football League.
Jumamosi iliyopita iliingia Uwanja wa Amex ikiwa na jezi maalumu za kumbukumbu, mashabiki 31,944 wakishuhudia sherehe, kisha ikamaliza siku hiyo kwa kuichapa Arsenal, mabingwa watetezi wa England, mabao 3-0.
Huu si ushindi wa kawaida. Ni simulizi ya klabu iliyowahi kuwa ukingoni mwa kusahaulika, lakini sasa inacheza soka la kiwango cha juu, inashiriki mashindano ya Ulaya na ina uwezo wa kuangusha miamba ya England.
ARSENAL MGENI WA SHEREHE
Brighton haikuruhusu Arsenal kuharibu sherehe zake. Pascal Gross aliifungia bao la kwanza, Charalampos Kostoulas akaongeza la pili kabla ya mapumziko, huku Chema Andres akifunga la tatu kipindi cha pili.
Mashabiki waliofika kusherehekea miaka 125 ya klabu yao walipata zawadi waliyoitamani zaidi.
Ushindi wa mabao 3-0 ulikuwa mkubwa zaidi kwa sababu ulipatikana dhidi ya Arsenal, timu inayotetea taji lake la Ligi Kuu England.
Kocha Fabian Hurzeler alisema ilikuwa siku maalumu, si kwa sababu ya mpinzani pekee, bali kutokana na kiwango ambacho wachezaji wake walionyesha.
“Ni mchezo ambao wachezaji walianza kwa nguvu, walishinda mipambano yao binafsi, wakacheza vizuri walipokuwa na mpira na kutengeneza nafasi,” alisema.
ILIPOTOKEA
Lakini ili kuelewa ukubwa wa ushindi huo, lazima urudi nyuma. Brighton ilianzishwa mwaka 1901. Iliingia Football League baada ya takribani miongo miwili na mwaka 1979 ikafika Ligi Kuu kwa mara ya kwanza. Lakini haikujenga historia yake kwa njia rahisi.
Mwaka 1983 ilifika fainali ya Kombe la FA dhidi ya Manchester United na kupata nafasi ya kushinda taji kubwa la kwanza katika historia yake.
Katika dakika za mwisho za muda wa ziada, Gordon Smith alipata nafasi ambayo mashabiki wa Brighton waliamini ingeandika historia. Lakini Gary Bailey, kipa wa Manchester United, aliokoa. United ikashinda marudiano. Baada ya hapo, Brighton ikaingia kwenye kipindi kigumu.
GOLDSTONE IKAPOTEA
Mwaka 1995, Uwanja wa Goldstone Ground uliokuwa nyumbani kwa Brighton tangu mwaka 1902 uliuzwa kutokana na madeni yaliyokuwa yakiongezeka.
Mashabiki hawakushirikishwa katika uamuzi huo. Mbaya zaidi, hakukuwa na uwanja mbadala uliokuwa tayari.
Mwaka 1997 Brighton ikaondoka Goldstone. Mchezo wa mwisho wa msimu wa 1995-96 uliishia kwenye vurugu baada ya maelfu ya mashabiki kuingia uwanjani kupinga uongozi. Hata nguzo za magoli zilivunjwa.
Klabu ambayo leo inakusanya zaidi ya mashabiki 31,000 kwa mchezo ilikuwa ikitafuta mahali pa kuchezea.
GILLINGHAM, KISHA WITHDEAN
Baada ya kuondoka Goldstone, Brighton ililazimika kucheza takribani maili 70 kutoka nyumbani, Gillingham. Iliishi huko kwa misimu miwili. Mwaka 1999 ikarejea Brighton, lakini hali haikuwa ya kifahari.
Ilianza kutumia Uwanja wa Withdean uliokuwa maarufu zaidi kwa matumizi ya riadha. Uwezo wake ulikuwa unaweza kuchukua takribani mashabiki 6,000.
Leo, Brighton ina Uwanja wa Amex wa kisasa, ikiwa na wastani wa zaidi ya mashabiki 31,000 kwa mchezo. Hapo ndipo tofauti ya Brighton ya zamani na ya leo ilipo.
MASHABIKI WALIKATAA KUFA
Mmoja wa watu wanaokumbuka vizuri kipindi hicho ni Paul Samrah, shabiki wa muda mrefu wa Brighton.
Kwa mujibu wake, baada ya fainali ya Kombe la FA mwaka 1983, wachezaji waliuzwa, uwekezaji ukapungua, Goldstone ukaanza kuchakaa na idadi ya mashabiki ikaanza kushuka.
Uhusiano kati ya mashabiki na viongozi nao ukawa mbaya. Hakukuwa na mwendelezo wa uongozi wala mwelekeo wa wazi. Lakini mashabiki walikataa kuiacha klabu ife. Walifanya kampeni. Walifanya maandamano. Walichanga fedha. Walipigania uwanja.
Na mwaka 2007 wakapata ushindi mkubwa baada ya kupata kibali cha mipango ya kujenga uwanja mpya Falmer. Brighton ikaanza kuamka.
BLOOM AKAFUNGUA SURA MPYA
Mwaka 2009, Tony Bloom akawa mwenyekiti. Mzaliwa huyo wa Brighton na shabiki wa maisha wa klabu hiyo, alihusika katika mabadiliko makubwa ya klabu.
Chini ya uwekezaji wake, Brighton ikaanza kupanda kutoka League One, ikafika Championship, kisha Ligi Kuu England. Na hapo ndipo klabu ilipoanza kujenga mfumo wake maarufu wa usajili.
Brighton ilinunua wachezaji wenye vipaji, ikawakuza na baadaye kuwauza kwa fedha kubwa. Data na uchambuzi vikawa sehemu muhimu ya mfumo huo.
Klabu ambayo zamani ilikuwa ikipambana kutafuta uwanja sasa ilikuwa ikifanya biashara ya wachezaji kwa mamilioni ya fedha.
KISHA ULAYA IKAFUNGUKA
Mabadiliko hayo yakafikisha Brighton kwenye hatua ambayo zamani mashabiki wake wangeiona kama ndoto.
Mwaka 2023 ilicheza mashindano ya Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia yake. Haikuwa safari ya kawaida.
Brighton ilikwenda Amsterdam kukutana na Ajax, moja ya klabu kubwa kabisa katika historia ya soka la Ulaya.
Zaidi ya mashabiki 7,000 wa Brighton walikuwa Amsterdam. Brighton ikashinda 2-0.
Klabu iliyowahi kucheza mbele ya mashabiki 6,000 kwenye Withdean, kuona maelfu ya mashabiki wake wakivamia Amsterdam kwa mashindano ya Ulaya ilikuwa uthibitisho wa mabadiliko makubwa yaliyokuwa yametokea.
SASA WANAWASUMBUA VIGOGO
Brighton sasa ni timu ya Ligi Kuu yenye uwezo wa kuwakabili vigogo.
Iliifunga Manchester United kwenye Uwanja wa Old Trafford kwa mara ya tano katika ziara zake sita za mwisho.
Imecheza misimu 10 mfululizo ya Ligi Kuu. Na sasa imeanza kampeni yake nyingine ya Ulaya, ikitafuta taji ambalo halijawahi kuwepo kwenye kabati lake.
Siku ambayo Brighton ilikuwa ikiadhimisha miaka 125 ya kuzaliwa kwake, iliwakaribisha mabingwa watetezi wa England, Arsenal. Wenyeji wakashinda 3-0.
BILA MASHABIKI ISINGEKUWEPO
Tony Bloom, katika ujumbe wake wa maadhimisho hayo, alikumbusha safari yote. Alitaja kupotea kwa Goldstone, safari za Gillingham na changamoto za kipindi cha Withdean. Lakini jambo kubwa alilosisitiza ni mchango wa mashabiki.
Kwa miaka mingi, mashabiki walikataa kuamini kwamba Brighton inapaswa kutoweka. Walipigana hadi klabu ikapata uwanja mpya na kuanza safari ya kurejea kileleni.
Leo, vizazi tofauti vya mashabiki vinakutana Amex. Babu anampeleka mwanawe. Mwana anampeleka mjukuu. Na wote wanashuhudia Brighton ambayo ni tofauti kabisa na ile iliyokuwa ikihangaika miaka ya 1990.