Mastaa wanaobeba hatari ya Kariakoo Dabi
KARIAKOO Dabi ya Oktoba 10 si pambano la dakika 90 pekee, bali pia ni vita ya kumbukumbu. Baadhi ya mastaa wa Simba na Yanga wanaingia uwanjani wakiwa na rekodi nzuri dhidi ya watani wao, lakini sasa wanapaswa kuzithibitisha tena kwenye dabi hii ambayo Mnyama ndio mwenyeji.
Ndani ya mechi hii, kuna mastaa wanne ambao tayari wameonyesha kwamba wanaweza kuwa na ushawishi mkubwa kwenye dabi hii kutokana na kile walichokifanya kwenye mechi zilizopita, Albert Kangwanda na Maxi Nzengeli kwa upande wa Yanga, huku Simba ikiwa na Clatous Chama na Libasse Gueye.
ALBERT KANGWANDA
Kangwanda anaingia kwenye Dabi akiwa na kumbukumbu tamu zaidi dhidi ya Simba baada ya kuamua mchezo wa mwisho wa Ngao ya Jamii uliochezwa Agosti 12, 2026, Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Alifunga bao pekee dakika ya 31 kwa kichwa akimalizia krosi ya Chadrack Boka na kuipa Yanga ushindi wa 1-0.
Hilo haikuwa bao la kawaida kwa Kangwanda kwa sababu lilikuja kwenye Dabi iliyokuwa na taji mezani. Yanga ilibeba Ngao ya Jamii kwa mara ya pili mfululizo mbele ya Simba, na Kangwanda ndiye aliyeandika historia yake akiwa amesajiliwa msimu huu na kwenye mechi yake ya kwanza kufunga bao tena dhidi ya watani zao.
Nyota huyo alisajiliwa na Yanga msimu huu akitokea Red Arrows ya Zambia. Mbali na hilo, msimu huu ameanza vizuri, akiwa amefunga mabao mawili katika michezo sita ya ligi kabla ya Dabi.
MAX NZENGELI
Kama kuna mchezaji mwenye rekodi inayoweza kumtesa zaidi Simba, basi ni Nzengeli.
Novemba 5, 2023, katika moja ya Dabi zilizozungumzwa zaidi, Yanga iliichapa Simba 5-1 Uwanja wa Benjamin Mkapa. Maxi alikuwa sehemu kubwa ya kipigo hicho baada ya kufunga mabao mawili, dakika ya 64 na 77.
Agosti 8, 2024, katika nusu fainali ya Ngao ya Jamii, alifunga bao pekee lililoipa Yanga ushindi wa 1-0 dhidi ya Simba. Bao hilo alifunga dakika ya 44 baada ya kumalizia pasi ya Pacome Zouzoua. Hiyo inaifanya rekodi yake kufikia mabao matatu dhidi ya Simba, mawili katika ushindi wa 5-1 na moja katika ushindi wa 1-0.
Msimu huu tayari amefunga mabao matatu katika michezo sita ya ligi, akiwa pia ametajwa kuwa mchezaji bora wa mechi mara tano katika michezo hiyo.
CLATOUS CHAMA
Kumbukumbu yake ya mwisho kwenye Dabi ya ligi ni Mei 3, 2026, pale Simba ilipotoka sare ya 2-2 na Yanga. Chama alifunga bao la pili la dakika ya 10 baada ya kupewa pasi na Elie Mpanzu lakini pia alitoa asisti ya bao la kwanza la Libasse Gueye huku pia akiwa mchezaji aliyefanya kazi kubwa katika mchezo huo na kutajwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
Chama pia anaingia kwenye Dabi hii akiwa mfungaji bora wa Simba kwenye ligi msimu huu. Baada ya michezo sita, tayari amefunga mabao manne, wakati Simba ikiwa imefunga mabao 11. Hiyo inamaanisha kuwa anaweza kuonyesha ubora wake kwenye mechi hii.
LIBASSE GUEYE
Kisha kuna Libasse Gueye, ambaye jina lake linaweza kuibua kumbukumbu ya haraka zaidi kwa mashabiki wa Yanga. Mei 3, 2026, kwenye sare ya 2-2, Gueye alifunga bao la kwanza la Simba mapema kabisa, dakika ya tatu tu.Bao hilo liliwapa nguvu Simba na kufunga la pili ndani ya dakika 10 tu.
Winga huyo msimu huu amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Simba, akiwa amefunga bao moja na kutoa asisti tano katika michezo sita ya ligi.
Zaidi ya rekodi binafsi, timu zote mbili zinaingia kwenye Dabi zikiwa zimeanza msimu kwa kasi. Baada ya michezo sita ya ligi, kila moja imekusanya pointi 18, huku Yanga ikiwa imefunga mabao 16 na Simba 11. Timu zote ziliruhusu mabao mawili.
Rekodi nzuri za nyuma zinaweza kuwa faraja kwa mchezaji, lakini kwenye Dabi zinaweza pia kuwa mzigo. Kwa sababu kila upande unajua kile ambacho mpinzani wake tayari amewahi kukifanya.