Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mastaa Bara wapata kiota kipya, wafuatana Libya!

LIBYA Pict

Muktasari:

  • Hapo kati Ligi Kuu England ilipoteza mastaa kibao wakienda Saudi Arabia ambako ilionekana kuna fedha nyingi za matajiri wa mafuta, na mastaa wakubwa walifurika Uarabuni kwenda kuzichota wakiweka nyuma suala la ushindani kule ambako walitoka.

MAISHA ya wachezaji wa soka hayana makazi ya kudumu kwani leo yupo pale, lakini kesho anaweza kuamkia kwingine na mambo yakaendelea. Yote hiyo inatokana na mahitaji na uamuzi wa kipato ambacho anaweza kukipata.

Hapo kati Ligi Kuu England ilipoteza mastaa kibao wakienda Saudi Arabia ambako ilionekana kuna fedha nyingi za matajiri wa mafuta, na mastaa wakubwa walifurika Uarabuni kwenda kuzichota wakiweka nyuma suala la ushindani kule ambako walitoka.

Hii imehamia hapa kwetu kwa sasa. Kumeanza kuchangamka baada ya kuonekana mastaa kadhaa waliowika hapa nchini wakianza kufurika kujazana Libya wakisajiliwa kwa fedha nyingi na klabu za huko, wakiamua kuutosa ushindani uliopo katika Ligi Kuu Bara.

Mchezaji wa karibuni kuingia katika orodha ya mastaa waliotimkia Libya ni mshambuliaji wa Simba na timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Kibu Denis, aliyetua Al Nasr Benghazi akiingia katika orodha ya mastaa waliotimkia huko. Hapa hapa ni baadhi ya mastaa waliotua huko na wengine wakiwa njiani.

LIBY 01

FABRICE NGOMA (AL NASR)

Kiungo wa zamani wa Simba, Fabrice Ngoma baada ya kumalizika kwa msimu uliopita mkataba wake ulifikia tamati na msimu huu ulipoanza alitua Al Nasr ya Libya anayoendelea kuitumikia mpaka sasa.

Ngoma ni kiungo mkongwe ambaye ana uzoefu wa kucheza ligi mbalimbali ikiwamo kwao DR Congo, Morocco, Sudan na Tanzania. Lakini, mapema tu alikwenda Libya kuongeza idadi ya mastaa kutoka hapa nchini wanaokipiga nchini humo.


LIBY 02

JEAN BALEKE (AL KHUMS)

Mshambuliaji Jean Baleke baada ya kuzitumikia Simba na Yanga kwa nyakati tofauti, hapo kati alisota kidogo bila kuwa na timu, lakini mwisho wa mwaka jana alitimkia nchini Libya alikojiunga na Al Khums.

Baleke, raia wa DR Congo hapa nchini alishindwa kumudu ushindani kuzichezea klabu kubwa, lakini alipohitajika na timu ndogo kujiunga nazo aligoma na sasa anaendelea kupambana kurudisha jina lake akiwa na timu hiyo inayoshiriki ligi daraja la kwanza.

Rekodi za Baleke ndani ya Simba mpaka sasa ndizo zinaongoza kwani alifunga mabao 16 ndani ya misimu miwili, huku akifunga matatu ndani ya Al Ittihad aliyoitumikia kwa miezi sita pekee na baada ya hapo alitua Yanga akiacha bao moja alikodumu nusu msimu.


LIBY 03

STEVE MUKWALA (AL NASR)

Mshambuliaji raia wa Uganda, Steven Mukwala amejisalimisha Libya na sasa kaungana na Ngoma ambaye waliwahi kufanya kazi pamoja Simba kwenye msimu ambao walitisha kiasi cha kwenda kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mukwala ameitumikia Simba kwa msimu mmoja na nusu ambapo uliopita alionyesha kiwango bora akifunga mabao 13, lakini msimu huu aliuanza taratibu kabla ya Simba kuamua kumuuza Al Nasr ya Libya.


LIBY 04

LUIS MIQUISSONE (AL AHLY BENGHAZI)

Winga Luis Miquissone naye amefuata fedha Libya. Aliwahi kutumika Simba kisha Wekundu wa Msimbazi walimuuza kwa Al Ahly ya Misri ambao baadaye ilimrudisha Simba kufuatia kutoridhishwa na uwezo wake.

Miquissone baada ya kurudi Simba hakukaa muda mrefu akatemwa na kurudi kwao Msumbiji ambako aliuwasha moto akiwa mmoja wa wafungaji bora na sasa amenunuliwa tena na Al Ahly ya Benghazi mwezi uliopita akienda kuanza maisha mapya, akionekana kuwa mchezaji ambaye atalipwa fedha nyingi.


LIBY 05

KIBU DENIS (AL NASR)

Kiungo mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis ameiona fursa na mamilioni ya fedha za Walibya siyo kitu cha kumpita kwa sasa. Amefungasha mabegi yake kwenda kujiunga na Al Nasr akiwa ni staa wa tatu kutoka kwa Wekundu wa Msimbazi kwenda kuvaa jezi za kijani nchini humo.

Kibu ameuzwa kwa fedha nyingi ambapo klabu yake imechukua kiasi kisichopungua Sh700 milioni huku mwenyewe akienda kuvuna zaidi ya Sh1.8 bilioni kwa mwaka mmoja na nusu ambao atakuwa akiwatumikia Waarabu.

Akiwa Simba, Kibu hakuwa na namba kubwa, lakini umuhimu wake ni mkubwa ndani ya kikosi hicho kutokana na nishati yake alipokuwa uwanjani, na sasa anakwenda kuungana na wenzake kina Ngoma, Mukwala ambao walishatangulia nchini humo tayari kuanza maisha mapya.


LIBY 06

STEPHANIE AZIZ KI (AL ITTIHAD)

Yanga inaye ‘mwakilishi’ nchini Libya ambaye ni kiungo wa zamani, Stephanie Aziz KI, ambaye aliondoka nchini majuzi akienda kujiunga na Al Ittihad ya huko akitokea Wydad Athletic ya Morocco.

Mambo yamebadilika kwa kasi upande wa Aziz KI ambapo baada ya kuwa na misimu mitatu ndani ya Yanga yenye mafanikio makubwa aliuzwa Wydad kwa pesa ndefu, lakini hakumaliza hata msimu mmoja na kumfanya auzwe hivi karibuni kwenda Libya.

Aziz KI tayari alishatambulishwa na sasa anasubiriwa kuanza kazi ndani ya klabu yake mpya akitajwa kuwa ni mmoja wa mastaa Al Ittihad ambao watakuwa wanalipwa pesa ndefu.


LIBY 07

FEI TOTO YUKO NJIANI

Kama kuna staa anazikataa ofa kutoka Libya, basi ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye klabu za huko zinapigana vikumbo kuwania saini yake, lakini tatizo ni utajiri na jeuri ya klabu anayoichezea ya Azam FC, ambayo imekuwa ikivimba kwa kumpandia dau na kumbakisha.

Hata hivyo, bado vita hiyo ni ngumu kwani Fei Toto anaonekana kushawishika kubaki Chamazi, ugumu ukiwa ni mkataba wake na Azam lakini siku mabayo matajiri hao wakikunjua nafsi basi kiungo huyo ataibukia huko haraka.

Kwa sasa Fei anahusishwa na kutakiwa na kikosi cha Al Ahly Tripoli ya Libya ambayo ndiyo kinara kwenye ligi ya nchini humo ikiwa na pointi 23 katika mechi 9 ilizocheza.