Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mashujaa FC yapania kupindua meza 2025/26

MASHUJAA Pict

Muktasari:

  • Ugeni wa Mwanaspoti ulipokewa na meneja wa timu hiyo, Athuman Amir aliyewezesha mahojiano kufanyika na wachezaji, kocha na uongozi lengo likiwa ni kueleza maandalizi ya kikosi hicho kwa msimu huu.

WAKATI maandalizi ya msimu yakifanyika, timu nyingi zilikuwa kambini zikisaka ufiti kwa ajili ya msimu mpya ambapo Mwanaspoti lilitembelea kambi ya kikosi cha Mashujaa kilichokuwa Kunduchi jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujiandaa na msimu wa Ligi Kuu Bara, hivyo linakuletea mahojiano yaliyofanyika kambini.

Ugeni wa Mwanaspoti ulipokewa na meneja wa timu hiyo, Athuman Amir aliyewezesha mahojiano kufanyika na wachezaji, kocha na uongozi lengo likiwa ni kueleza maandalizi ya kikosi hicho kwa msimu huu.

MASHU 05

TABIA ZA WACHEZAJI KAMBINI

Amir anasema kila mchezaji ana tabia yake, lakini jambo la msingi wanaishi kama familia kwa sababu kila mmoja yupo kwa ajili ya kufanikisha malengo ya klabu.

"Kiongozi ni kama mzazi anayetakiwa kujua tabia ya kila mchezaji kisha anaishi naye kulingana na alivyo wakati mwingine kuwashauri kukaa katika mstari wa kuzifikia ndoto zao," anasema Amir.

Kitu ambacho ni lazima mchezaji kukizingatia ni kufuata taratibu za kambini kutokana na timu hiyo kuwa ni ya taasisi akitoa mfano kuwa kama mtu anataka kutoka nje ya kambi inatakiwa aombwe ruhusa meneja ili ajue anakokwenda.

"Timu ya Mashujaa ikija jijini Dar es Salaam inakaa kambi ya jeshi na tukiwa Kigoma pia tunakaa kambi ya jeshi, ndiyo maana kila mchezaji anaposajiliwa lazima aambiwe taratibu zinazotakiwa kufuatwa," anasema Amir.

Meneja huyo anaeleza kwamba baadhi ya wachezaji wana tabia za kipekee zinazotoa mafunzo na kuchekesha, lakini kama kiongozi anahakikisha wanazingatia kuishi kwa umoja na upendo.

MASHU 01

MREFU NA MFUPI ZAIDI

Katika kikosi hicho mchezaji mrefu kuliko wote, kwa mujibu wa meneja wa timu hiyo ni beki Frank Magingi aliye na futi 6.7, huku mfupi kuliko wote ni kiungo mshambuliaji Balama Mapinduzi 'Kipenseli' mwenye futi tano.

Wakati meneja anawaelezea wachezaji hao, Balama anaonekana kutokubaliana naye akimtaja straika mpya Suleiman Bwenzi aliyefunga mabao matano ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita akiwa na KenGold kuwa ndiye mfupi zaidi katika timu hiyo.

Meneja huyo anamaliza ubishi kwa kuwasimamisha pamoja wachezaji hao, lakini bado Balama akaonekana ndiye mfupi.

MASHU 04

MAANDALIZI

Amir anasema timu imecheza mechi kadhaa za kujiandaa na msimu, jambo linaloashiriwa kuwa wamejipanga vizuri kwa lengo la kuleta ushindani.

"Tumecheza na Enjoy Soccer, Tabora United, Fountain Gate, Talent Academy, Ngome, Elite Pro Academy Tanzania, Al Hilal," anasema meneja huyo.

Kuhusu tamasha la Siku ya Mashujaa ambalo hutumika kama sehemu ya utambulisho wa wachezaji wapya, Amir anasema limefanyika na lilifana.

MASHU 02

WACHEZAJI

Nyota wa timu hiyo, Ismail Mgunda anasema baada ya kurejea tena kikosini akitokea AS Vita ya DR Congo ambako alishindwa  kucheza kutokana na kutolipwa mshahara, amekutana na ongezeko la wachezaji wapya hivyo anatarajia ushindani wa namba.

"Kuna wachezaji wengi wazuri wameongezeka kikosini kama Salum Kihimbwa, Mudathir Said ambao wote ni wazuri na wanafanya tupambane zaidi katika uwanja wa mazoezi ili kumshawishi kocha kupata namba ya kucheza," anasema Mgunda.

Kiungo mshambuliaji, Omary Omary aliyerejea kwa mkopo ndani ya kikosi hicho akitokea Simba anasema: "Wakati narejea kutoka Simba nakumbuka mchezaji aliyenipokea na kunitania ni Mgunda. Aliniambia tumerejea nyumbani tupambane, hivyo najipanga kuhakikisha mchango wangu unakuwa na manufaa katika timu."

MASHU 03

BENCHI LA UFUNDI

Akizungumzia malengo ya timu, kocha msaidizi wa kikosi hicho, Charles Fredie 'Demba' anasema kwa usajili uliofanyika anaamini wana uwezo wa kumaliza katika nafasi nne za juu msimu wa 2025-2026.

"Kiufundi kikosi kimeanza kuelewana kwa maana ya wachezaji waliokuwepo na wageni. Ushindani wa namba ni mkali, pia tumeona usajili wa watu wengine ambao unaonyesha Ligi Kuu msimu ujao itakuwa ni ngumu kutokana na mahitaji ya kila mmoja wetu," anasema Demba na kuongeza:

"Tumefanya usajili mkubwa na mzuri kwa sababu tumehakikisha kila nafasi ina wachezaji bora zaidi ya wawili. Utakuwa ni msimu mgumu kutokana na timu nyingine zilivyosajili, ingawa tumepania kuleta ushindani ili kutimiza malengo yetu."