Kinapigwa upyaaa Ligi Kuu England!
Muktasari:
- Kwa upande mwingine wa msimamo wa ligi hiyo, Arsenal wanaongoza kwa tofauti ya pointi tano baada ya kushinda mechi tano zilizopita mfululizo, huku Brighton wanakamata nafasi ya pili ilhali Manchester City wakishuka hadi nafasi ya tatu baada ya kupoteza mechi tatu mfululizo.
MANCHESTER, ENGLAND: KATIKA kipindi cha mapumziko cha wiki mbili ya kalenda ya Shirikisho la Kandanda Duniani (Fifa), kumekuwapo na mabadiliko mawili ya makocha katika Ligi Kuu England; Mauricio Pochettino amechukua nafasi ya Michael Carrick katika kikosi cha Manchester United, ambayo ipo katika eneo la kushuka daraja, huku Thomas Frank akichukua mikoba ya Pierre Sage katika timu ya Crystal Palace, ambayo ipo mkiani mwa msimamo.
Kwa upande mwingine wa msimamo wa ligi hiyo, Arsenal wanaongoza kwa tofauti ya pointi tano baada ya kushinda mechi tano zilizopita mfululizo, huku Brighton wanakamata nafasi ya pili ilhali Manchester City wakishuka hadi nafasi ya tatu baada ya kupoteza mechi tatu mfululizo.
Raundi ya 11 itakuwa na mechi kuanzia leo Jumamosi, Jumapili na Jumatatu. Kabla ya kuanza kwa ratiba kipute hebu tuangalie utabiri wa Opta unaendaje.
LEO JUMAMOSI
MANC CITY VS FULHAM
Mwanzo mzuri wa Manchester City katika msimu huu ulivurugika kabla ya mapumziko ya michezo ya kimataifa na sasa wanatafuta kurejea katika ushindi watakapokuwa wenyeji wa Fulham, leo.
City wamepoteza mechi tatu mfululizo za ligi, idadi sawa na ile waliyopoteza katika mechi 36 zilizotangulia (ushindi 25, sare 8). Tangu kuanza kwa msimu wa 2007/08 wamepoteza mechi nne mfululizo mara mbili tu, mwezi Agosti 2008 na Desemba 2024.
Hata hivyo, City wameshinda mechi 17 za mwisho za ligi hiyo dhidi ya Fulham, na pia wameshinda 20 za mwisho dhidi ya timu hiyo katika mashindano yote. Katika mechi hiyo City ina nafasi kubwa ya kushinda kwa asilimia 66.1. Hakuna timu nyingine yenye uwezekano mkubwa zaidi wa ushindi katika mechi za wikendi hii, huku Fulham wakipewa asilimia 15.5 ya kushinda.
Itakumbukwa kwamba Fulham walikuwa na mwanzo mgumu wa msimu, lakini hawajapoteza katika mechi nne zilizopita za ligi (ushindi 2, sare 2), na wamepoteza mechi moja tu kati ya saba zilizopita (ushindi 2, sare 4).
ASTON VILLA VS SUNDERLAND
Katika mechi zitakazoanza saa 3:00 usiku, Aston Villa wanatafuta kurejea kwenye ushindi baada ya kupoteza uongozi wa bao katika dakika za mwisho na kutoka sare ya kusisimua ya mabao 4-4 dhidi ya Manchester United katika mchezo uliopita. Safari hii watakutana na Sunderland.
Lakini, Villa wamepoteza mechi moja kati ya 12 zilizopita za ligi hiyo dhidi ya Sunderland (ushindi 5, sare 6). Kipigo hicho kilikuwa cha mabao 3-1 mwezi Januari 2016.
Villa pia hawajapoteza katika mechi sita zilizopita za ligi (ushindi 3, sare 3), ingawa katika sare zote tatu walipoteza pointi licha ya kuwa mbele kwa mabao. Kwa upande mwingine, Sunderland wanatafuta kushinda mechi mbili mfululizo za ligi hiyo kwa mara ya kwanza msimu huu, baada ya kuifunga Chelsea bao 1-0 katika mchezo uliopita.
Hata hivyo, Aston Villa ndiyo inayopewa nafasi kubwa kushinda kwa asilimia 59.3 katika mchezo huo ambao utakuwa mechi ya 150 ya Unai Emery akiwa kocha wa klabu hiyo katika ligi hiyo, huku
Sunderland wakiwa na asilimia 19.4 ya kushinda.
BOURNEMOUTH VS NITTINGHAM
Bournemouth inapewa asilimia 55.3 kushinda na kuendeleza kupanda kwao katika msimamo wa ligi watakapokutana na Nottingham Forest wanaopewa asilimia 21.6, ambao walimaliza kipindi chao kibaya cha matokeo kwa kuifunga Manchester City kabla ya mapumziko.
Bournemouth wameshinda mechi nane zilizopita katika mashindano yote na hawajapoteza katika mechi zote nane za ligi hiyo dhidi ya Forest (ushindi 4, sare 4).
Baada ya kuanza msimu kwa kusuasua, Bournemouth wamefanikiwa kuingia katika nafasi saba za juu na wanataka kushinda mechi tano mfululizo za ligi hiyo kwa mara ya kwanza katika historia.
Forest kwa upande wao hawajashinda katika mechi sita za ugenini za ligi dhidi ya Bournemouth (sare 2, vipigo 4). Hata hivyo, wanatafuta kushinda mechi mbili mfululizo za ligi kwa mara ya pili katika mwaka huu wa kalenda. Mara ya kwanza ilikuwa ni mfululizo wa ushindi wa mechi tatu mwezi Aprili na Mei.
Ushindi utakuwa matokeo mazuri kwa kocha Oliver Glasner, ambaye anajiandaa kusimamia mechi yake ya 100 ya Ligi Kuu England (ushindi 33, sare 32, vipigo 34). Hata hivyo, bado hajawahi kuifunga Bournemouth katika mashindano hayo.
CHELSEA VS LEEDS UTD
Chelsea waliingia katika mapumziko ya michezo ya kimataifa wakiwa wametoka kupoteza mchezo wa kukatisha tamaa dhidi ya Sunderland, wakati Leeds United walimaliza mfululizo wa mechi tano bila ushindi kwa kuifunga Tottenham. Hata hivyo, Chelsea wanatarajiwa kushinda katika Uwanja wa Stamford Bridge, wakiwa na uwezekano wa ushindi wa asilimia 51.1.
Katika mechi tano za nyumbani za ligi msimu huu, Chelsea wamekusanya pointi 10 (ushindi 3, sare 1, kipigo 1). Pia wameshinda mechi nane kati ya kumi za mwisho za nyumbani dhidi ya Leeds katika mashindano yote (sare 2), tangu walipopoteza kwa mabao 2-0 mwezi Desemba 1999.
Chelsea tayari wameifunga Leeds nyumbani katika mashindano ya Carabao msimu huu, kwa mabao 6-3. Hata hivyo, Leeds, ambao wanapewa asilimia 24 kushinda hawajapoteza katika mechi mbili za ligi dhidi ya Chelsea msimu wa 2025/26 (ushindi wa 3-1 nyumbani na sare ya 2-2 ugenini).
Lakini, hawajafanikiwa kucheza mechi tatu mfululizo bila kufungwa na Chelsea tangu kipindi cha Novemba 2000 hadi Oktoba 2001.
COVENTRY CITY VS CRYSTAL PALACE
Kuna uwezekano mzuri wa mchezo huu kuisha kwa sare, ambao ni asilimia 26.8, wakati Thomas Frank atakuwa akianza kazi yake kama kocha wa Crystal Palace. Coventry inapewa asilimia 45.7 kushinda, huku Crystal Palace ikiwa na 27.5.
Huu utakuwa mchezo wa kwanza kati ya Coventry na Palace katika mashindano yoyote tangu Machi 2012, walipotoka sare ya 1-1 katika Championship. Palace walishawagi kushinda mechi nne za kwanza za ugenini dhidi ya Coventry kati ya 2005 na 2008.
Hata hivyo, hawajashinda katika mechi nne za mwisho katika mashindano yote kati ya 2009 na 2012 (sare 2, vipigo 2). Coventry wamepoteza mechi moja kati ya sita walizocheza dhidi ya Crystal Palace ligi hiyo (ushindi 2, sare 3).
SPURS VS IPSWICH
Klabu ya zamani ya Thomas Frank, Tottenham Hotspur itakuwa dimbani Jumamosi, ambapo itakuwa mwenyeji wa Ipswich Town. Mfululizo mzuri wa matokeo wa Spurs ulisitishwa walipofungwa bao 1-0 na Leeds kabla ya mapumziko ya michezo ya kimataifa. Hata hivyo, wanatarajiwa kurejea kwenye ushindi.
Spurs inapewa asilimia 55.2 kushinda, huku Ipswich ikiwa na 21.7 ilhali uwezekano wa sare ni asilimia 23.1. Rekodi zinaonyesha kwamba Spurs wamepoteza mechi nne kati ya tano za mwisho za ligi hiyo dhidi ya Ipswich. Isipokuwa ni ushindi wa mabao 4-1 katika mchezo wao wa mwisho mwezi Februari 2025.
Pia Spurs hawajashinda katika mechi nne za kwanza za ligi baada ya mapumziko ya michezo ya kimataifa (sare 1, vipigo 3). Katika mapumziko ya kwanza ya msimu huu, walitoka sare ya 1-1 dhidi ya Manchester United. Hata hivyo, Spurs wanatarajiwa kufunga mabao katika mchezo huu kwa sababu Ipswich wamefungwa katika kila moja ya mechi 29 zilizopita za ligi hiyo.
Ni timu nne tu katika historia ya mashindano hayo zilizowahi kucheza mechi 30 au zaidi mfululizo bila kuweka rekodi ya kutofungwa bao.
NEWCASTLE VS ARSENAL
Mechi za Jumamosi zitahitimishwa katika uwanja wa St James’ Park, ambapo Newcastle United watawakaribisha Arsenal. Kumbukumbu zinaonyesha kwamba Newcastle wameshinda mechi moja tu kati ya 29 za mwisho za ligi hiyo dhidi ya timu zilizokuwa zinaongoza msimamo wa ligi siku ya mchezo (sare 8, vipigo 20).
Pia hawajashinda katika mechi 18 za mwisho za aina hiyo (sare 4, vipigo 14), tangu walipoifunga Chelsea kwa mabao 2-1 mwezi Desemba 2014. Na inatarajiwa mfululizo huo wa matokeo mabaya kuendelea, huku Arsenal wakipewa asilimia 56.4 wakiwa na nafasi kubwa zaidi ya kushinda kama timu ya ugenini wikendi hii.
Hakuna hata mmoja kati ya michezo 13 ya mwisho ya nyumbani ya Newcastle dhidi ya Arsenal katika ligi hiyo iliyoisha kwa sare (ushindi 4, vipigo 9). Rekodi ziko wazi kwamba Newcastle wameshinda mechi tatu kati ya tano za mwisho dhidi ya Arsenal, lakini katika mchezo huu wanapewa nafasi ya ushindi ya asilimia 21.7.
Arsenal wameshinda mechi nyingi zaidi za ligi hiyo dhidi ya Everton (41) na West Ham (39) kuliko walizoshinda dhidi ya Newcastle (38). Aidha, Arsenal wameweka rekodi ya kutofungwa bao katika mechi 32 dhidi ya Newcastle, idadi kubwa zaidi ya mechi ambazo timu moja imewahi kuweka rekodi hiyo dhidi ya timu nyingine katika mashindano hayo.
KESHO, JUMAPILI
HULL CITY VS BRIGHTON
Hull City walishinda mechi mbili za kwanza za ligi hiyo, lakini tangu hapo hawajashinda katika mechi nane zilizofuata (sare 5, vipigo 3). Hii ni mara ya nne katika historia ya mashindano hayo kwa timu kushinda mechi zake mbili za kwanza na kisha kushindwa kutoshinda nane zinazofuata.
Timu nyingine zilizowahi kufanya hivyo ni Wolves 2011/12, Hull 2016/17 na West Brom 2017/18. Timu zote hizo zilishuka daraja mwishoni mwa misimu hiyo. Hata hivyo, kabla ya kukutana kwa mara ya kwanza na Brighton katika Ligi Kuu England, Hull bado hawajapoteza mchezo wowote wa nyumbani katika ligi hiyo msimu huu.
Brighton hawajashinda katika mechi zote sita walizocheza katika uwanja wa MKM katika mashindano yote (sare 2, vipigo 4). Ushindi wa mwisho wa ugenini dhidi ya Hull ulikuwa katika uwanja wa Boothferry Park, katika daraja la nne la soka la England, mwezi Oktoba 2000.
Hata hivyo, Brighton wanafanya vizuri sana msimu huu na wanapewa nafasi ya kushinda kwa asilimia 50.1. Uwezekano wa sare ni asilimia 23.6, huku Hull wakiwa na asilimia 26.3 ya ushindi.
LIVERPOOL VS MAN UTD
Mechi kubwa ya kesho Jumapili itawakutanisha Manchester United, chini ya kocha mpya Mauricio Pochettino, na wapinzani wao Liverpool katika uwanja wa Anfield. Pochettino ndiye kocha wa kwanza wa Man United ambaye mchezo wake wa kwanza wa ligi akiwa na klabu hiyo atakutana na Liverpool.
Kati ya makocha tisa wa mwisho wa Man United, wakiwemo wa muda ni mmoja tu aliyepoteza mchezo wake wa kwanza wa ligi hiyo akiwa na klabu hiyo (ushindi 4, sare 4). Kocha huyo ni Erik ten Hag, ambaye alipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Brighton mwezi Agosti 2022.
Man United walishinda mchezo huu kwa mabao 2-1 msimu uliopita, na kumaliza mfululizo wa mechi tisa bila ushindi katika uwanja wa Anfield kwenye ligi hiyo (sare 5, vipigo 4). Na Liverpool walipoteza mechi zote mbili za ligi hiyo dhidi ya Man United msimu uliopita. Idadi hiyo ni sawa na jumla ya vipigo walivyopata katika mechi 18 zilizotangulia dhidi ya United (ushindi 7, sare 9).
Mara ya mwisho Liverpool kupoteza mechi nyingi zaidi mfululizo dhidi ya United ilikuwa kati ya Desemba 2014 na Januari 2016, walipopoteza mechi nne mfululizo. Hata hivyo, Liverpool ina nafasi kubwa ya kushinda mchezo huu kwa asilimia 57.3 huku Man United wakiwa na 20.5 ilhali 22.2 ni sare.
Raundi ya 11 itafikia tamati keshokutwa Jumatatu, Brentford watakapokuwa wenyeji wa Everton ambao wako katika kiwango bora, watakaoingia mchezoni hawapewi nafasi kubwa ya kushinda wakipewa asilimia 28.8 kushinda huku Brentford wakiwa na 44.3 ilhali sare ni 26.9.