Prime
Kwa Prince Dube, Yanga hawajui kama walie au wacheke
MTOTO wa Mfalme aliyezamia ughaibuni amerudi kwao. Imekuja ghafla. Sikutazamia lakini sikushtuka sana. Prince Dube amerudi kwao kama ambavyo wahamiaji wa Zimbabwe wanavyorudi kwao kutoka Afrika Kusini wakati huu Wasauz wakiwakataa wahamiaji.
Tofauti ni Dube ametokea Tanzania ambako aliishi kihalali na alipendwa na watu wengi. Alipendwa na wazawa. Awali alipendwa na mashabiki wa timu yake ya kwanza nchini Azam ambayo alihamia akitokea Highlanders ya kwao Zimbabwe. Baadae akapendwa na mashabiki wa Yanga ambayo alihamia kutoka Azam na ameondokea huko kurudi nyumbani.
Labda mashabiki pekee ambao hawakumpenda Dube, ingawa ni kweli hawakumchukia pia, walikuwa ni mashabiki wa timu ya Simba. Aliwanyanyasa kwa kuwafunga mabao muhimu kuanzia alipohamia nchini hadi alipoondoka.
Simba hawakumchukia kwa sababu hakuwa mchezaji mkorofi ndani na nje ya uwanja. Alicheza huku akitabasamu. Ilikuwa ngumu kumchukia .Hata hivyo, anaondoka nchini akiwa ameacha hisia mkanganyiko kwa mashabiki wake wa timu yake ya mwisho, Yanga.
Kwanza kabisa walimpenda Dube kwa sababu mbili. Waliufurahia uhamisho wake kutoka Azam kwa sababu alikuwa mmoja kati ya washambuliaji tishio nchini ingawa rekodi zake hazikuonyesha kuwa tishio aliyepitiliza.
Dube hakuwahi kufunga zaidi ya mabao 20 ya ligi kwa msimu. Sawa, alikuwa mshambuliaji mzuri lakini hakuwahi kuacha alama kama ambavyo kina Amiss Tambwe, John Bocco na Meddie Kagere waliacha katika miaka ya karibu. Hata hivyo, alikuwa mfungaji mzuri.
La pili, Yanga walifurahia namna ambavyo Dube alikwenda kwao kwa uhamisho ambao ulionekana kama vile wa kisasi dhidi ya Azam. Azam walikuwa wametoka kumchukua Fei Toto kutoka Yanga kwa ubabe wa ajabu ajabu na hapo hapo Injinia Hersi Said na genge lake wakapata bahati ya kulazimisha uhamisho wa Dube atoke Azam kwenda kwao.
Na bahati nzuri kwao licha ya utata mwingi ambao ulifunika uhamisho wake lakini Dube alikuwa tayari kushinikiza dili hilo litokee. Akaingia mgomo ule ule ambao Fei aliingia kwa Yanga kulazimisha uhamisho wa kuondoka na akafanya hivyo hivyo.
Jambo hili liliwafurahisha Wanayanga. Moja kwa moja wakamhifadhi moyoni.
Yanga huwa wana tabia ya kumfanya mchezaji ajihisi kuwa shabiki zaidi pengine kuliko kuwa mchezaji. Baada ya hapo Dube aliishi katika maisha yenye utata Yanga kiasi kwamba hadi juzi alipoonekana anasaini klabu ya Hardrock ya kwao Zimbabwe walikuwa hawajui kama walie au wacheke.
Dube ameishi katika maisha ya milima na mabonde pale Jangwani. Asilimia 45 alikuwa amefikia matarajio, asilimia 55 alikuwa hajafikia matarajio. Ndiyo maana maamuzi yake ya kurudi nyumbani Harare yamepokelewa kwa mikono miwili na mashabiki.
Kuwasili kwa Dube kulionekana kama vile Yanga walikuwa wamempata mrithi sahihi wa Fiston Mayele ambaye alikuwa ametimkia Pyramids ya Misri. Yanga walihisi wangeimarika zaidi kwa kuwa na Dube kwa sababu walikuwa na timu nzuri ba viungo bora. Dube angecheza mbele ya viungo mahiri kama Pacome Zouzoua, Clatous Chotta Chama, Maxi Nzingeli na Aziz Ki.
Hata hivyo, Dube alikumbwa na tatizo la kukosa mabao ya wazi. Uwiano wake wa kufunga na kukosa ulikuwa asilimia hamsini kwa hamsini. Mwanzoni wakati anaingia Yanga alikosa mabao ya wazi zaidi mpaka baadhi ya mashabiki wa Yanga waliamini Dube alikuwa amefanyiwa mambo ya kishirikina na wachezaji wenzako. Alikosa mabao ambayo usingeweza kuamini angekosa.
Siku moja aliondolewa uwanjani baada ya kukosa mabao lukuki akaenda zake katika benchi na kuanza kulia. Siku chache zilizofuata Yanga wakaanzisha kampeni ya kumuongezea mapenzi zaidi kwa ajili ya kumuongezea uwezo wa kujiamini. Wakaanza kuimba jina lake kila anapocheza pale katika uwanja wa KMC. Alijaribu kurudisha kiwango chake lakini hakuwahi kuikamata Yanga kama ambavyo ilipaswa.
Hakuwahi kuimakamata Yanga kama ambavyo kina Mayelle waliwahi kufanya huko nyuma. Na kabla ya kina Mayele, basi kina Edibily Lunyamila waliwahi kuikamata Yanga huko nyuma. Sawa ni mfungaji mzuri, pia ni mkosaji mzuri wa mabao.
Na sasa kuna mambo mawili ya kuyaweka katika katika akiba. Jambo la kwanza ni deni kwa kina Injinia Hersi na genge lake. Wanapaswa kuziba nafasi ya Dube kwa mshambuliaji ambaye mashabiki wa Yanga hawatamkumbuka Dube.
Mara nyingi mashabiki wetu huwa wanaulaumu zaidi uongozi wao kwa sababu ya kuchemsha kuziba pengo la mchezaji mahiri aliyepita. Kama ameondoka mchezaji hodari basi pengo lake inabidi lizibwe na mchezaji hodari zaidi.
Nafasi ya Clement Mzize ilikuwepo Yanga. Yeye ni mzawa. Lakini pale mbele kulikuwa na nafasi mbili za washambuliaji wageni. Alikuwepo Dube mwenyewe na alikuwepo Dilson Maria Aurello Depu. Inamaanisha Yanga wana nafasi ya mshambuliaji wa kigeni pale mbele kama wakijisikia.
Na kama wakijisikia kuwa na mshambuliaji wa kigeni basi lazima wawe na mtu kama Prince Dube au ambaye anazidi ubora wake. Hili ni deni ambalo Hersi na wenzake linawakabili kwa sasa. Kama wakiweza basi litakuwa jambo zuri. Kama wasipoweza basi mashabiki wataugeukia uongozi wa Yanga kwanini hawakubaki na Dube.
Jambo jingine ambalo ni muhimu kukumbuka ni ukweli kuna uwezekano mkubwa tukamkaribisha tena Dube nchini baada ya miezi 24 kuanzia sasa. Imekuwa ni kitu cha kawaida kwa wachezaji mahiri wa kigeni waliowahi kutamba nchini kwetu kuondoka na kurudi tena.
Tanzania ina maisha matamu. Huwa wanarudi kwa sababu nyingi tofauti. Siwezi kuzitaja sana hizo sababu kwa sababu watu wengi wanazijua lakini kwa ufupi nimkaribishe tena Dube nchini muda wowote ambao atajisikia. Hata akirudi kucheza Namungo namkaribisha tena kwa niaba ya watanzania wote kwa sababu imekuwa mazoea kwa wao kuondoka na kisha kurudi tena.