Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makocha wa kigeni wataibeba Afrika mashariki!

AFCON Pict

Muktasari:

  • Nchi hizo tatu zinashiriki mechi za kufuzu mashindano ambayo tayari zina uhakika wa kucheza, kutokana na kuwa wenyeji wa fainali hizo zitakazofanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027.

KUNA jambo la kipekee katika safari ya Uganda, Kenya na Tanzania kuelekea fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (PAMOJA AFCON) 2027.

Nchi hizo tatu zinashiriki mechi za kufuzu mashindano ambayo tayari zina uhakika wa kucheza, kutokana na kuwa wenyeji wa fainali hizo zitakazofanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027.

Kwa wenyeji hao, mechi hizi si vita ya kutafuta tiketi, bali ni sehemu ya kuzijenga timu, kuwapa nafasi wachezaji, kujaribu mifumo na, kwa makocha, kuendelea kupima uwezo wao kabla ya mtihani mkubwa wa fainali za nyumbani.

Lakini jambo jingine linalovutia ni kwamba nchi zote tatu zimewaamini makocha wa kigeni kuongoza safari hiyo.

Uganda inaongozwa na Mbelgiji Paul Put, Kenya iko chini ya raia wa Afrika Kusini, Benni McCarthy, huku Tanzania ikinolewa na Muargentina Miguel Gamondi.

Hata hivyo, hakuna kocha yeyote kati yao aliyeanza mradi huo jana. Put aliteuliwa kuwa kocha wa Uganda mwaka 2023 na mkataba wake ukaongezwa hadi 2028.

AFC 01

Katika kampeni ya CHAN 2024 iliyochezwa mwaka huu kutokana na kuahirishwa, Morley Byekwaso na Fred Muhumuza ndio waliokuwa wakisimamia timu rasmi, lakini Put aliendelea kushiriki katika maandalizi na uangalizi wa kikosi. Uganda ilifikia hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza katika historia yake ya CHAN.

McCarthy alijiunga na Kenya Machi 2025 na mara moja akakutana na majukumu ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026 pamoja na CHAN. Chini yake, Harambee Stars ilifikia robo fainali ya CHAN kwa mara ya kwanza, ikiwa imepata ushindi dhidi ya DR Congo na Morocco.

Kwa Gamondi, safari yake imekuwa tofauti kidogo. Alianza kuiongoza Tanzania kama kocha wa muda Novemba 2025, muda mfupi kabla ya fainali za AFCON nchini Morocco.

Aliiongoza Taifa Stars kufika hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza kabla ya kuthibitishwa kuwa kocha wa kudumu kwa mkataba wa miaka miwili Februari mwaka huu.

Kwa hiyo, matokeo ya mechi za mwanzo za kufuzu AFCON 2027 si usaili kwa makocha wapya. Ni mwendelezo wa miradi ambayo tayari imeanza.

Put alianza kwa kuiongoza Uganda kutoka sare ya bao 1-1 na Tunisia ugenini, huku Rogers Mato akisawazisha baada ya Alaa Arous kuipa Tunisia bao la mapema. Nathan Asiimwe alitoa pasi ya bao hilo. Uganda sasa inakutana na Libya kwenye Uwanja wa Hoima City.

Kenya nayo ilianza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Eritrea mjini Nairobi, huku Ryan Ogam akiokoa pointi kwa bao la kusawazisha dakika za mwisho.

Tanzania ilikuwa na mwanzo mgumu zaidi baada ya kufungwa mabao 2-0 na Guinea-Bissau Zanzibar, licha ya kumiliki mpira kwa muda mrefu. Taifa Stars ikalazimisha sare 1-1 na  Madagascar katika mchezo wa pili.

AFC 02

Matokeo hayo yana umuhimu, lakini si kwa maana ya kawaida ya kufuzu, kwa sababu wenyeji hao tayari wana tiketi ya AFCON 2027.

Kinachovutia zaidi ni historia ya uamuzi wao kwa benchi la ufundi.

Uganda imeifanya falsafa ya makocha wa kigeni kuwa karibu na utamaduni wake wa timu ya taifa. Mike Mutebi ni Mganda.

Mutebi alikuwa Mganda wa mwisho kuiongoza timu hiyo ya taifa kwa kudumu mwaka 2004. Tangu hapo, kazi hiyo imepitia mikononi mwa makocha wa kigeni kama Pedro Pasculli, Mohammed Abbas, Csaba Laszlo, Bobby Williamson, Milutin ‘Micho’ Sredojevic, Sebastien Desabre, Johnathan McKinstry na sasa Put.

Moses Basena na Abdallah Mubiru waliwahi kupewa majukumu ya muda, lakini hakuna aliyepata nafasi ya kudumu katika kipindi hicho.

Hivyo, Uganda imekuwa na pengo la zaidi ya miongo miwili katika kumpa kocha wake mzawa jukumu la kudumu la timu ya taifa.

Shirikisho la Soka Uganda (Fufa) limekuwa na hoja yake kuhusu uamuzi huo.

Mwaka 2018, rais wa Fufa, Moses Magogo, alisema Uganda ilihitaji kocha mwenye uzoefu wa kutosha katika soka la Afrika.

“Tunahitaji kocha mwenye utaalamu na uzoefu kwenye bara la Afrika. Hatukuwa na Mganda aliyefikia kiwango hicho,” alisema Magogo wakati akieleza sababu za kumteua Desabre sambamba na mipango ya kuwaendeleza makocha wazawa.

Mwaka mmoja baadaye, baada ya kuondoka kwa Desabre, Mubiru alipewa jukumu la muda huku Fufa ikitafuta kocha wa kudumu.

Mubiru hakutaka kuiona nafasi hiyo kama suluhisho la muda tu.

“Wageni hawatoki mwezini. Tunapitia mafunzo yanayofanana na wao, na sisi tuna faida ya kuijua mazingira yetu. Mawazo hayapimwi kwa rangi ya mtu,” alisema.

AFC 03

Kwa Kenya, simulizi ni tofauti. Harambee Stars imekuwa ikibadilisha kati ya makocha wazawa na wageni.

Francis Kimanzi, Jacob ‘Ghost’ Mulee na Stanley Okumbi ni miongoni mwa Wakenya waliowahi kuiongoza timu hiyo katika miaka ya karibuni, huku wageni kama Sebastien Migne, Bobby Williamson na Engin Firat nao wakipata nafasi.

Kimanzi aliwahi kusisitiza umuhimu wa uelewa wa mazingira ya ndani baada ya kumrithi Migne mwaka 2019.

“Makocha wazawa wako karibu zaidi na watu wao na wanaweza kupata kilicho bora kutoka kwao kwa sababu wanawaelewa zaidi,” alisema.

Hata hivyo, uamuzi wa Kenya kumchagua McCarthy unaonyesha kwa nini makocha wa kigeni bado wanavutia.

Shirikisho la Soka Kenya (FKF) lilieleza uzoefu, maono na dhamira yake ya kuendeleza soka la Kenya kuwa miongoni mwa sababu zilizomfanya McCarthy achaguliwe baada ya mchakato uliowahusisha waombaji wengi.

Tanzania nayo imekuwa ikibadilisha kati ya makocha wazawa na wageni. Salum Mayanga, Hemed Seleman ‘Morocco’ na Dk.Mshindo Msolla ni miongoni mwa wazawa waliowahi kuiongoza Taifa Stars, huku wageni kama Emmanuel Amuneke, Mart Nooij, Marcio Maximo na Adel Amrouche nao wakipewa nafasi.

AFC 03

Hivyo, uteuzi wa Gamondi si jambo jipya. Kinachoufanya kuwa wa kipekee ni uzoefu wake wa zaidi ya miaka 25 katika soka la Afrika na namna anavyosema bara hili limekuwa sehemu muhimu ya safari yake ya ukocha.

Ukweli ni kwamba kocha wa kigeni haimaanishi moja kwa moja kuwa bora kuliko mzawa. Vivyo hivyo, kuwa mzawa hakumaanishi moja kwa moja kuwa kocha bora zaidi.

Kinachobeba uzito ni uzoefu, mazingira ya kazi, ubora wa wachezaji, msaada wa shirikisho na muda anaopata kocha kujenga timu.

Na mjadala huo unakuwa mpana zaidi Uganda kwa sababu Fufa haijaishia kutafuta kocha nje ya nchi. Sasa pia inapanua wigo wa wachezaji wa Cranes kwa kuwapa nafasi wenye asili ya Uganda waliokulia katika mifumo ya soka ya mataifa mengine.

Hakuna ubaya katika hilo. Soka limekuwa likivuka mipaka kwa muda mrefu na wachezaji hao wanaweza kuleta uzoefu wa mifumo tofauti ya mafunzo na ushindani wa kiwango cha juu.

Lakini swali linabaki: Uganda ikiendelea kumtafuta kocha nje na pia wachezaji nje, hilo linasema nini kuhusu mfumo wa soka wa ndani?

Labda swali muhimu zaidi ni hili: nini kitabaki baada ya wageni hao kuondoka?

Mpango wa muda mrefu haupaswi kuwa tu kujenga kikosi imara cha Cranes kwa ajili ya AFCON 2027. Unapaswa pia kuhakikisha kuna kitu kinachobaki nyuma ya makocha wanaoendelea, akademi zenye nguvu, mashindano bora na mfumo unaoweza kuzalisha vipaji bila kutegemea msaada wa nje kila wakati.

Put, McCarthy na Gamondi tayari wamepata muda wa kuifahamu ardhi wanayoiongoza.

Lakini AFCON 2027 itakuwa mtihani tofauti kabisa.

Itakuwa nyumbani, mbele ya mashabiki wao, presha kubwa na matarajio ambayo hakuna mchezo wa kufuzu unaoweza kuyalinganisha.

Na hapo ndipo tutakapojua kama uamuzi wa Afrika Mashariki kutazama nje ulikuwa sehemu ya kujenga mafanikio ya muda mrefu au ulikuwa suluhisho la kufika kwenye mashindano ya nyumbani.