Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Madhara ya kurudia nguo za ndani

Muktasari:

  • Wapo wanaume na wanawake wanaodhani kuwa boxer inaweza kuvaliwa mara mbili au zaidi ikiwa haijachafuka kwa kuonekana au haina harufu kali. Wengine huona hakuna sababu ya kufua chupi kila siku kwa sababu wanavaa kwa muda mfupi tu, hasa wanapokuwa hawajatoka nyumbani. 

UNAWEZA kutumia fedha nyingi kununua marashi, mafuta ya kujipaka na bidhaa mbalimbali za kujisitiri ili kuhakikisha mwili wako unanukia vizuri, lakini kuna jambo moja dogo unaloweza kuwa unalipuuza kila siku nalo ni kurudia kuvaa boxer ambayo tayari umeivua bila kuifua. Wakati ukijitahidi kuonekana msafi kwa nje, je, unajua kinachoendelea kwenye nguo yako ya ndani baada ya kuitumia kwa siku nzima?

Wapo wanaume na wanawake wanaodhani kuwa boxer inaweza kuvaliwa mara mbili au zaidi ikiwa haijachafuka kwa kuonekana au haina harufu kali. Wengine huona hakuna sababu ya kufua chupi kila siku kwa sababu wanavaa kwa muda mfupi tu, hasa wanapokuwa hawajatoka nyumbani.

Lakini, ukweli ni kwamba, kutoona uchafu kwa macho hakumaanishi boxer ni safi. Jasho, mafuta ya ngozi, bakteria na majimaji ya mwilini yanaweza kubaki kwenye kitambaa na kujenga mazingira yasiyofaa kwa afya ya ngozi na sehemu za siri.

JASHO NA BAKTERIA

Mtaalamu wa afya Dorcas Natse anasema kuwa: “Sehemu za siri ni miongoni mwa maeneo ya mwili yanayoweza kuwa na joto na unyevunyevu kutokana na kufunikwa na nguo kwa muda mrefu. Hali hiyo inapokutana na boxer iliyotumika, hasa yenye jasho, inaweza kuongeza uwezekano wa bakteria na fangasi kuzaliana.

“Kwa hiyo, mtu anaporudia boxer bila kuifua, anaweza kuendelea kuvalia mabaki ya jasho na uchafu uliokusanyika tangu matumizi ya awali. Hali hiyo inaweza kuchangia matatizo ya ngozi, hasa kwa watu wanaotokwa na jasho jingi au wanaovaa nguo zinazobana.”


MUWASO

Anasema kuwa: “Kwa wanawake, kurudia chupi kunaweza kuongeza hatari ya muwasho kwenye ngozi ya nje ya sehemu za siri, hasa pale kitambaa kinapokuwa na unyevunyevu na kusababisha msuguano.

“Mazingira yenye joto na unyevunyevu yanaweza kuchochea ukuaji wa fangasi kwenye maeneo ya kinena na kusababisha muwasho, wekundu na vipele. Maambukizi ya fangasi ukeni yana sababu mbalimbali na si lazima yatokane na kurudia chupi.”

WANAUME WAPO KWENYE HATARI

Anasema kuwa: “Kwa wanaume, kurudia boxer kunaweza kusababisha mazingira ya joto na unyevunyevu kwenye eneo la korodani na mapaja ya ndani. Hali hii inaweza kuongeza uwezekano wa muwasho, michubuko na fangasi kwenye kinena.

“Tatizo linaweza kuwa kubwa zaidi kwa wanaume wanaofanya kazi zinazowafanya watokwe na jasho jingi, wanaofanya mazoezi au wanaovaa boxer zinazobana kwa muda mrefu.

“Mbali na matatizo ya ngozi, jasho na bakteria vinapokusanyika kwenye kitambaa vinaweza kusababisha harufu mbaya. Hivyo, hata kama mtu anatumia marashi na kujipulizia manukato, kufanya hivyo hakuondoi uchafu uliopo kwenye boxer.”


USAFI UNAANZA NA BOXER SAFI

Ili kujikinga na matatizo hayo, jambo la kwanza ni kubadilisha boxer kila siku na kuvaa iliyofuliwa na kukaushwa vizuri. Mtu akifanya mazoezi au kutokwa na jasho jingi anashauriwa kubadilisha nguo ya ndani mara moja baada ya shughuli hizo.

Pia, ni vizuri kuchagua boxer za pamba zinazopitisha hewa, kuepuka kuvaa nguo za ndani zenye unyevunyevu na kuhakikisha zinafuliwa kwa sabuni na kukaushwa vizuri kabla ya matumizi mengine.

Ni muhimu pia kutoficha harufu kwa kutumia marashi badala ya kutafuta chanzo chake. Ikiwa muwasho, vipele, maumivu au harufu isiyo ya kawaida vinaendelea, ni vyema kumuona daktari kwa uchunguzi.

USHAURI

Usafi wa mwili hauishii kwenye kuoga, kupaka mafuta na kutumia manukato. Unaanzia pia kwenye nguo unazovaa moja kwa moja kwenye mwili wako. Boxer na chupi siyo nguo za kuzoea kuzivaa kwa sababu tu hazionekani chafu ila ni nguo zinazohitaji kubadilishwa na kufuliwa kama nyingine yoyote.