Serengeti Boys na safari ya kwanza Kombe la Dunia
Muktasari:
- Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 17 lilianza mwaka 1985 nchini China, wakati huo likiitwa Mashindano ya Dunia ya Soka kwa Vijana chini ya Miaka 16 (FIFA U-16 World Championship).
TIMU ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys inajiandaa kuandika historia mpya katika Fainali za Kombe la Dunia za vijana zitakazofanyika Qatar kuanzia Novemba 19 hadi Desemba 13, 2026.
Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 17 lilianza mwaka 1985 nchini China, wakati huo likiitwa Mashindano ya Dunia ya Soka kwa Vijana chini ya Miaka 16 (FIFA U-16 World Championship).
Ni mafanikio yanayobeba uzito mkubwa kwa soka la Tanzania, hasa ikizingatiwa kuwa kwa miaka mingi nchi imekuwa ikitafuta nafasi ya kupeleka timu ya taifa ya wanaume katika mashindano hayo makubwa ya vijana lakini ikawa inashindikana.
Safari hiyo haijaja kwa bahati mbaya. Imechangiwa na hatua ambazo vijana hao wamekuwa wakizipiga katika mashindano ya kikanda na yale ya Afrika, huku mafanikio yao makubwa yakionekana katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON) zilizofanyika Morocco mwaka huu.
Tanzania ilifika kwenye hatua hiyo baada ya kufanya vizuri katika mechi za makundi za AFCON, ikiwafunga Msumbiji mabao 3-0 kabla ya kuichapa Angola kwa matokeo kama hayo.
Ushindi dhidi ya Angola Mei 17, 2026 uliifanya Serengeti Boys kufikisha pointi sita na kufuzu robo fainali, huku tiketi ya Kombe la Dunia ikiwa tayari mikononi mwao. Mabao hayo yalifungwa na Razak Juma, Hassan Kizinga na Sadam Hussein.
Lakini vijana hao hawakuishia kwenye kufuzu Kombe la Dunia. Waliendelea kupambana na kufanikiwa kufika fainali ya AFCON kwa mara ya kwanza katika historia yao.
Katika robo fainali waliitoa Algeria kwa penalti 4-3 baada ya sare ya mabao 3-3, kabla ya kuiondoa Misri kwa penalti 4-3 pia baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu.
Fainali dhidi ya Senegal ilimalizika kwa sare ya bao 1-1, Hamis Chenga akiifungia Tanzania dakika ya saba, lakini Serengeti Boys ikapoteza kwa penalti 4-2 na kumaliza mashi ndano ikiwa mshindi wa pili Afrika.
HISTORIA TANZANIA U-17 AFCON
Kabla ya mafanikio ya mwaka 2026, Tanzania ilikuwa imeshiriki mara tatu katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17.
Mwaka 2017 ilikuwa miongoni mwa washiriki wa mashindano hayo, kisha ikashiriki tena 2019 ilipokuwa mwenyeji.
Baada ya hapo ilirejea tena 2025 na kushiriki tena 2026, ikiwa ni mara yake ya nne. Tofauti na miaka iliyopita, mwaka huu imefanikiwa kuvuka hatua ya makundi, kufika fainali na kukata tiketi ya kihistoria ya Kombe la Dunia.
Hivyo, mafanikio ya Morocco ni ishara ya hatua mpya kwa soka la vijana nchini, hasa kwa kuonyesha kuwa Serengeti Boys inaweza kushindana na mataifa yenye uzoefu mkubwa katika soka la Afrika.
MTIHANI WA KUNDI
Baada ya kufanikisha safari ya kufuzu, Serengeti Boys sasa inakabiliwa na mtihani mwingine mkubwa katika Kundi I, ambako imepangwa pamoja na Brazil, Jamhuri ya Ireland na Costa Rica. Hili ni kundi ambalo linahitaji maandalizi makubwa kutokana na tofauti za uzoefu wa washiriki wake katika mashindano ya kimataifa.
Brazil ndiyo timu yenye historia kubwa zaidi katika kundi hilo. Imewahi kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia U-17 mara nne, ikiwa ni mwaka 1997, 1999, 2003 na 2019. Hivyo, mchezo dhidi yake utakuwa kipimo kikubwa cha uwezo wa vijana wa Tanzania kukabiliana na moja ya mataifa yenye mafanikio makubwa katika soka la vijana.
Jamhuri ya Ireland nayo si timu ya kuichukulia kawaida. Ilishiriki Kombe la Dunia la mwaka 2025 na kufika hatua ya 16 bora kabla ya kutolewa na Uswisi. Pia ilifuzu mashi ndano ya mwaka huu baada ya kuifunga Slovakia mabao 7-0 katika hatua ya kufuzu.
Costa Rica ina uzoefu mkubwa zaidi wa mashindano hayo kuliko Tanzania, ikiwa imeshiriki mara 11 kabla ya mwaka huu.
Mafanikio yake makubwa yalikuwa kufika robo fainali katika matoleo ya 2001, 2003, 2005 na 2015. Hii inaifanya kuwa moja ya timu ambazo Serengeti Boys italazimika kujiandaa nazo kwa umakini mkubwa.
KUVUKA MAKUNDI
Tofauti na mfumo wa zamani wa mashindano hayo, toleo la 2026 litashirikisha timu 48 zilizogawanywa katika makundi 12 yenye timu nne kila moja.
Timu mbili za juu kutoka kila kundi zitafuzu hatua ya 32 bora, huku zikifuatana na timu nane zitakazomaliza nafasi ya tatu zikiwa na matokeo bora zaidi.
Hii ina maana kuwa Serengeti Boys haitahitaji tu kupambana kwa ajili ya nafasi mbili za juu, bali pia inaweza kutumia nafasi ya kuwa miongoni mwa timu nane bora zilizomaliza nafasi ya tatu.
Kwa hiyo, kila pointi na kila bao vitakuwa na umuhimu katika safari ya Tanzania nchini Qatar.