Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Swaga nje, makonde mazito ndani ya ulingo

Muktasari:

  • Kwa miaka mingi, bondia amekuwa akihusishwa na misuli, mazoezi makali, makovu na sura ya mtu anayejua kupambana. Lakini taswira hiyo imebadilika. Siku hizi, unaweza kumwona bondia akishusha makonde mazito ulingoni, lakini akitoka hapo anakuwa mtu mwingine kabisa katika mavazi, mwonekano na namna anavyojiweka.

UKIACHANA na makonde mazito, mikanda ya ubingwa na ushindani unaotawala ndani ya ulingo, mchezo wa ngumi nchini Tanzania una sura nyingine inayozidi kuvutia macho ya mashabiki. Ni suala la muonekano wa mabondia wanapokuwa nje ya kazi yao.

Kwa miaka mingi, bondia amekuwa akihusishwa na misuli, mazoezi makali, makovu na sura ya mtu anayejua kupambana. Lakini taswira hiyo imebadilika. Siku hizi, unaweza kumwona bondia akishusha makonde mazito ulingoni, lakini akitoka hapo anakuwa mtu mwingine kabisa katika mavazi, mwonekano na namna anavyojiweka.

Jambo la kuvutia zaidi ni kwamba hata mabondia wa kike wameendelea kuonyesha kuwa kushiriki mchezo unaohitaji nguvu nyingi hakumaanishi kuachana na urembo, fasheni na kujitunza.

Hawa hapa mabondia watano wa kike na watano wa kiume wanaovutia macho ya mashabiki kwa muonekano wao, huku rekodi zao zikionyesha kuwa si sura na swaga pekee, bali pia wana kazi ya kufanya ndani ya kamba nne.


FADHILI MAJIHA

Huyu ni bondia mwenye uzoefu mkubwa katika masumbwi ya kulipwa, akiwa amewahi kushikilia mikanda mbalimbali ya kikanda na kimataifa, ikiwamo ubingwa wa dunia wa UBO katika uzani wa Bantamweight.

Kwa mujibu wa takwimu za Record Boxing zilizosasishwa mwaka 2026, Majiha ana mapambano 54, ushindi 36, vipigo 14 na sare nne. Kati ya ushindi wake, 17 amepata kwa KO.

Majiha ni mmoja wa mabondia ambao majina yao yamekuwa yakihusishwa na safari ndefu ya ngumi nchini, huku uzoefu wake wa kimataifa ukiendelea kumweka kwenye orodha ya mabondia wenye historia ya kuvutia.

DEBORA MWENDA

Huyu ni miongoni mwa mabondia wanaovunja dhana kwamba mwanamke anayepigana ngumi lazima apoteze haiba yake ya kike.

Debora George Mwenda amejijengea jina la Bondia Mrembo, jina ambalo amekuwa akilitumia kuelezea namna mashabiki wanavyomchukulia kutokana na muonekano wake.

Debora amewahi kueleza kuwa anapenda kupendeza na kuonekana tofauti kwa sababu maisha yake hayaishii kwenye ngumi pekee. Nje ya ulingo pia anajishughulisha na biashara ya mavazi ya michezo.

Hata hivyo, usimdharau kwa sababu ya muonekano wake. Kwa mujibu wa rekodi za BoxRec, Debora amepigana mapambano sita ya kulipwa, akishinda matatu, kupoteza mawili na kutoka sare moja tangu alipoanza safari yake mwaka 2022.

Hapo ndipo unapoweza kuona tofauti ya Debora wa ulingoni na Debora wa uraiani. Glovu zinabaki gym, lakini haiba yake ya kike inaendelea kuwa sehemu ya utambulisho wake.


HASSAN MWAKINYO

Huyu ni miongoni mwa mabondia wanaotambulika zaidi nchini na jina lake limekuwa likibeba uzito mkubwa katika masumbwi ya kulipwa.

Hassan Mwakinyo ana mwonekano unaomtofautisha na taswira ya bondia anayejulikana kwa mapambano pekee. Namna anavyojibeba, kujiamini na muonekano wake wa uraiani ni sehemu ya mvuto wake kwa mashabiki. Lakini rekodi yake nayo inajieleza. Kufikia baada ya pambano lake la Juni 10, 2026, Mwakinyo alikuwa na mapambano 29, akishinda 25 na kupoteza manne. Kati ya ushindi huo, 19 aliupata kwa KO/TKO. Hapo ndipo unapoweza kuona kwamba Mwakinyo si jina kubwa kwa muonekano pekee, bali pia kwa makali yake ndani ya ulingo.


SARA ALEX

Sara Alex ni jina jingine linalostahili nafasi katika orodha hii. Bondia huyo amekuwa kivutio kikubwa katika ndondi za wanawake nchini kutokana na namna anavyojiweka nje ya mapambano.

Anatambulika pia kwa jina la Miss GB wa Arusha, huku akijijengea nafasi kupitia mapambano mbalimbali ya ngumi za kulipwa.

Lakini usidanganywe na muonekano wake. Sara ni mpambanaji ambaye amekutana na wapinzani wenye uzoefu mkubwa, akiwamo Halima Vunjabei katika pambano la kuwania taji la UBO la dunia mwaka 2026, ambalo alilipoteza kwa uamuzi wa majaji baada ya raundi 10.

Kwa mujibu wa rekodi ya sasa ya WBA, Sara ana ushindi nane, vipigo viwili na sare moja. Hiyo ni rekodi inayomuweka katika kundi la mabondia wanawake wanaozidi kujitengenezea jina kwenye mchezo huo.


IBRAHIM CLASS

Class, ni mmoja wa mabondia ambao wameendelea kuipa Tanzania heshima katika masumbwi ya kimataifa.

Mwaka 2026 aliandika historia baada ya kushinda mikanda miwili ya WBC International katika pambano moja nchini Thailand dhidi ya Kritiphak Duangnut, aliyemshinda kwa TKO ya raundi ya tano Aprili 25.

Mbali na mafanikio hayo, Class ana taswira ya kijana anayejitambulisha kwa kujiamini na kujibeba kama mtu anayejua thamani ya jina lake katika mchezo huo.

Kwa mujibu wa Class alikuwa na rekodi ya mapambano 42, akishinda 34, kati yake 17 kwa KO, kupoteza sita na kutoka sare mbili.

Ushindi wake wa kimataifa umeongeza ukubwa wa jina lake na kumfanya kuwa miongoni mwa mabondia wanaofuatiliwa na mashabiki.

STUMAI MUKI

Muki ni mmoja wa mabondia wanawake wanaotambulika kwenye ngumi za kulipwa nchini. Asili yake ni Kigoma na alianza safari ya ndondi mwaka 2019.

Bondia huyo amekuwa akivutia macho ya mashabiki kwa namna anavyojiweka nje ya ulingo, huku akionyesha kuwa maisha ya mwanamichezo hayaishii kwenye mazoezi na mapambano pekee.

Kwa mujibu wa taarifa za Mwanaspoti za Agosti 2026, Stumai alikuwa ameshacheza mapambano 18 ya kulipwa, akishinda 12 na kupoteza sita bila sare. Mbali na rekodi hiyo, Stumai amewahi kueleza namna familia yake, hasa mama yake, ilivyomsaidia kuendelea na mchezo huo licha ya hofu ya awali kuhusu hatari za ngumi.

Ni mfano mwingine wa mwanamke anayechanganya mapambano makali na haiba yake nje ya ulingo.


TWAHA KIDUKU

Kiduku ni jina ambalo haliwezi kukosekana kwenye orodha ya mabondia wanaovutia macho ya mashabiki.

Mtoto huyo wa Morogoro amekuwa akijijengea utambulisho kupitia ngumi za kulipwa, huku akijulikana kwa namna anavyojibeba katika maisha ya kawaida. Kwa mujibu wa rekodi za BoxRec zilizoripotiwa na Mwanaspoti Juni 2026, Kiduku alikuwa amepigana mapambano 37, akishinda 26, kupoteza 10 na kutoka sare moja. Kati ya ushindi huo, 10 aliupata kwa KO.

Mbali na masumbwi, Kiduku ana upande mwingine wa maisha. Amewahi kujihusisha na uigizaji, upigaji wa ngoma za asili, u-DJ na muziki wa Singeli.

Hapo ndipo unapopata picha ya bondia ambaye maisha yake hayajaishia kwenye glovu pekee, bali pia ana uwezo wa kujitambulisha kupitia vipaji vingine.


HAWA NEWTON

Hawa Newton ni miongoni mwa mabondia wanawake wanaovutia macho katika mchezo huo.

Alianza kupigana mwaka 2022 na anashiriki uzani wa Lightweight. Kwa mujibu wa taarifa za Mwanaspoti za Agosti 2026, alikuwa ameshacheza mapambano sita, akishinda manne, kutoka sare moja na kupoteza moja.

Hata hivyo, kinachomfanya aingie kwenye mjadala huu si matokeo ya mapambano pekee, bali pia taswira yake nje ya ulingo inayotofautiana na ukali unaohitajika wakati wa kupambana. Katika mchezo ambao unahitaji nguvu, nidhamu na uvumilivu, Hawa anaonyesha kuwa mwanamke anaweza kushiriki masumbwi huku akiendelea kujitunza na kujiweka kwa namna anayopenda.

REHEMA MAFUNDO

Rehema Mafundo ni jina la kuongeza kwenye orodha ya mabondia wanawake wenye mvuto na rekodi zinazovutia.

Mwanaspoti lilipomzungumzia katika makala Agosti 2026, lilieleza kuwa nje ya ulingo anaweza kuonekana kama mtu wa kawaida, lakini anapokuwa kazini ndani ya kamba nne anabadilika na kuwa mpambanaji wa kweli. Mbali na muonekano wake, Rehema ana rekodi inayostahili kuangaliwa. Katika mapambano 14 aliyokuwa ameshacheza, alikuwa ameshinda 13 na kutoka sare moja bila kupoteza pambano lolote.

Bondia huyo wa uzani wa Welterweight pia amewahi kueleza kuwa pambano lake dhidi ya Happy Daudi mwaka 2017, alilolishinda kwa TKO katika ubingwa wa PST, limebaki kuwa moja ya mapambano muhimu katika safari yake. Huyo ni mfano wa bondia ambaye haiba yake ya nje haiondoi makali yake ya kazi.


SELEMANI KIDUNDA

Kidunda, anayefahamika pia kama Mamba, ni miongoni mwa mabondia waliowahi kuiwakilisha Tanzania katika majukwaa makubwa ya kimataifa.

Alishiriki Michezo ya Olimpiki ya London mwaka 2012, jambo linalomweka katika kundi la wanamichezo wenye historia muhimu kwenye ndondi za Tanzania. Kwa mujibu wa takwimu za WBA, Kidunda ana rekodi ya mapambano 10, akishinda tisa, saba kati ya hizo kwa KO, na kutoka sare moja bila kupoteza pambano. Pia amewahi kutwaa mkanda wa WBF Intercontinental Super Middleweight mwaka 2022 baada ya kumshinda Erick Katompa kwa uamuzi wa majaji.

Kwa muonekano wake wa kimichezo na uzoefu alioupata katika miaka yake ya kupambana, Kidunda ana nafasi yake katika orodha ya mabondia wanaoweza kutambulika hata wanapokuwa nje ya ulingo.