Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ligi Kuu England ilivyoacha rekodi kali 2024/25.

REKODI Pict
REKODI Pict

Muktasari:

  • Msimu wa Ligi Kuu England ulifika tamati Jumapili, ambapo Mo Salah ameibuka kuwa kinara wa mabao baada ya kutikisa nyavu mara 29, akimaliza msimu kwa mabao sita juu zaidi ya mchezaji aliyemfuatia kwenye nafasi ya pili, straika wa Newcastle United, Alexander Isak.

LONDON, ENGLAND: SUPASTAA wa Liverpool, Mohamed Salah ameweka rekodi tamu kwenye Ligi Kuu England msimu huu wa 2024/25 baada ya kunyakua tuzo ya Kiatu cha Dhahabu na ile ya Playmaker wa msimu baada ya kuongoza kwa asisti katika mikikimikiki hiyo.

Msimu wa Ligi Kuu England ulifika tamati Jumapili, ambapo Mo Salah ameibuka kuwa kinara wa mabao baada ya kutikisa nyavu mara 29, akimaliza msimu kwa mabao sita juu zaidi ya mchezaji aliyemfuatia kwenye nafasi ya pili, straika wa Newcastle United, Alexander Isak.

Huu ni msimu wa nne tofauti kwa Mo Salah kumaliza msimu wa Ligi Kuu England akiwa kinara wa mabao, akilingana na gwiji wa Arsenal, Thierry Henry kwenye rekodi hiyo ya Kiatu cha Dhahabu.

Na tuzo ya Playmaker inatolewa kwa mchezaji aliyeasisti mara nyingi. Salah amemaliza msimu huu akiwa na asisti 18, sita zaidi ya anayemkaribia kwenye hilo, staa wa Newcastle, Jacob Murphy.

 Hii ni mara ya pili kwa Mo Salah kushinda tuzo zote mbili Kiatu cha Dhahabu na Playmaker ndani ya msimu mmoja, alipofanya hivyo pia msimu wa 2021/22, akifunga mabao 23 na asisti 13.

Ni mchezaji mmoja tu aliyewahi kufanya hivyo kubeba tuzo hizo mbili ndani ya msimu mmoja, straika Harry Kane, aliyebeba msimu wa 2020/21 akiwa Tottenham Hotspur, alipofunga 23 na kuasisti 14.

Andrew Cole alipokuwa Newcastle United 1993/94 na Jimmy Floyd Hasselbaink alipokuwa akikipiga Leeds United msimu wa 1998/99, nao walimaliza msimu wa Ligi Kuu England wakiongoza kwa mabao na asisti, lakini tuzo ya Playmaker ilianza kutolewa msimu wa 2017/18.

Wakati Mo Salah akitamba kwenye eneo hilo, kipa wa Arsenal, David Raya na yule wa Nottingham Forest, Matz Sels kwa pamoja ndio walioshinda tuzo ya Golden Glove, ambayo inatolewa kwa makipa walioongoza kucheza mechi nyingi bila ya kuruhusu nyavu zao kuguswa. Raya na Sels kila mmoja alicheza mechi 13 bila ya kuruhusu nyavu zake kuguswa kwenye Ligi Kuu England. Hii ni mara ya tatu tangu tuzo hiyo ilipoanza kutolewa 2004/05 kushuhudia makipa wawili wakilingana na kushinda pamoja. Raya, ambaye alishinda msimu uliopita na kisha kuitetea msimu huu ameingia kwenye anga za Pepe Reina, Joe Hart na Ederson.

Siku ya mwisho ya msimu ilishuhudiwa vita kali ya kuwania tiketi ya kucheza michuano ya Ulaya kwa msimu ujao, ambapo sasa timu za Liverpool, Arsenal, Man City, Chelsea, Newcastle na Spurs zimefuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku timu ya Aston Villa na Crystal Palace zitacheza na Europa League wakati Nottingham Forest itakipiga kwenye Conference League, ikiwa mara yao ya kwanza kurudi kwenye michuano ya Ulaya baada ya miaka 21.

Ligi Kuu England imetia nanga huku ikiacha rekodi kibao tamu za kutamba nazo.

REK 04

WAKALI WA MABAO

Kwenye vita ya Kiatu cha Dhahabu kwa maana ya mkali wa mabao, Mo Salah ameibuka kinara baada ya kufunga mara 29, akifuatiwa na Isak, aliyefunga mabao 23, huku Erling Haaland akifunga mara 22 na tano bora inakamilishwa na Bryan Mbeumo na Chris Wood, waliofunga mara 20 kila mmoja kwenye mchakamchaka huo wa Ligi Kuu England.


WAKALI WA ASISTI

Katika kutambua mchango wa wapiga pasi za mwisho za mabao, Ligi Kuu England imekuwa ikitoa tuzo kwenye eneo hilo na Mo Salah ameibuka mshindi baada ya kuasisti mara 18, akifuatiwa na Jacob Murphy mwenye asisti 12, wakati Anthony Elanga ameasisti mara 11, huku tano bora ikikamilishwa na Bruno Fernandes na Antonee Robinson, walioasisti mara 10 kila mmoja - sawa na Mikel Damsgaard, Morgan Rogers na Bukayo Saka.

REK 04

WAKALI WA PASI

Unaweza kuona sababu ya Liverpool kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu kutokana na mastaa wake kufanya vizuri, ambapo beki wa kati, Virgil van Dijk akiongoza kwa pasi nyingi, akipiga 2,923 na kufuatiwa na Levi Colwill wa Chelsea pasi 2,595, William Saliba wa Arsenal pasi 2,547 huku tano bora ikikamilishwa na wakali wawili wa Man City, Josko Gvardiol pasi 2,528 na Ruben Dias aliyepiga pasi 2,309.


WAKALI WA CLEANSHEET

Kipa wa Arsenal, David Raya ametetea tuzo ya kucheza mechi nyingi bila ya kuruhusu nyavu zake kuguswa baada ya msimu huu kuwa na mechi 13, sawa na ilivyotokea kwa kipa Matz Sels wa Forest. Jordan Pickford amecheza mechi 12 bila ya kuruhusu bao, huku tano bora ikikamilishwa na Dean Henderson na Robert Sanchez, ambao wamecheza mechi 11 na 10 wakiwa na vikosi vyao Palace na Chelsea mtaliwa bila ya kuruhusu nyavu zao kuguswa.


MABAO MENGI

Kwa upande wa timu, Liverpool ndiyo iliyoongoza kwa kufunga mabao mengi, ilipomaliza msimu ikiwa imefunga mara 86 na kufuatiwa na Man City iliyofunga 72, Arsenal mara 69, Newcastle mabao 68 huku Brentford ikikamilisha tano bora ya klabu zilizofunga mabao mengi kwenye Ligi Kuu England msimu huu baada ya kutikisa nyavu mara 66.

REK 02

KULALA YOMBO SANA

Kizazi kipya kinaweza kisifahamu kulala yombo ni kitu fani, lakini hii ni kupiga takolini, ambapo Manchester United ndiyo iliyokuwa kinara, ikifanya hivyo mara 817, ikifuatiwa na Wolves mara 801, Palace mara 767, huku tano bora ikihitimishwa na timu za Everton, iliyopiga 732 na Leicester City 728.


USHINDI MARA NYINGI

Kwenye msimu wa mechi 38, Liverpool ndiyo iliyofunika timu nyingine kwa kushinda mara nyingi ndani ya msimu huu, mara 25, ikifuatiwa na Man City iliyoshinda mechi 21, huku Arsenal na Chelsea kila moja ikishinda mechi 20 sawa na ilivyokuwa kwa Newcastle inayokamilisha tano bora ya timu zilizoshinda mechi nyingi kwenye Ligi Kuu England, ilipofanya hivyo mara 20.

REK 05

KUPOTEZA MECHI NYINGI

Kwenye ushindi mara nyingi, kuna kinyume chake - ambacho ni kupoteza mechi nyingi, taji ambalo kwenye Ligi Kuu England msimu huu linashikiliwa na Southampton, iliyopoteza mechi 30 na ndiyo maana imeshuka daraja, sambamba na Leicester City iliyopoteza mechi 25 na Ipswich Town mechi 24, huku timu zote hizo zikiwa zimeshika daraja msimu huu. Spurs imepoteza mechi 22, huku inayokamilisha tano bora ya timu zilizopoteza mechi nyingi ni Wolves, ambayo imechapwa mara 20. Kinachochekesha kuhusu Spurs ni kwamba imo kwenye orodha ya timu zilizopoteza mechi nyingi kwenye Ligi Kuu England, lakini itakuwapo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, ikifuzu baada ya kubeba taji la Europa League kwa kuichapa 1-0 Man United katika mchezo wa fainali uliofanyika Bilbao, Hispania, wiki iliyopita.