Leicester ingekuwa Ligi Kuu ya Tanzania tungeoga kauli chafu
Muktasari:
UMEWAHI kuifikiria dunia ambayo wanaishi wachezaji wa Leicester City kwa sasa? Ni dunia tofauti. Dunia iliyojaa raha. Wachezaji wa Leicester City wana raha zote duniani. Kina Riyad Mahrez, Ngolo Kante, Jamie Vardy ni kama wafalme kwa sasa.
UMEWAHI kuifikiria dunia ambayo wanaishi wachezaji wa Leicester City kwa sasa? Ni dunia tofauti. Dunia iliyojaa raha. Wachezaji wa Leicester City wana raha zote duniani. Kina Riyad Mahrez, Ngolo Kante, Jamie Vardy ni kama wafalme kwa sasa.
Kocha wao, Claudio Ranieri ni mtu mwenye furaha pia. Amewezaje kutengeneza timu ya bei rahisi, lakini inaviadhiri vigogo na mpaka kufikia tarehe ya leo, inaongoza kwa tofauti ya pointi tano. Mchezaji mmoja wa Manchester City anaweza kugharimu kikosi chote cha Leicester.
Pamoja na uhodari wao uwanjani, pamoja na kumshangaza kila mtu, pamoja na kusifiwa sana, lakini Leicester wametulia sana na wala hawana mbwembwe. Nilikuwa natafakari kama Leicester wangekuwa Tanzania wakifanya mambo haya wakiwa timu ya kawaida kabisa ambayo sio Simba, Azam, Mtibwa Sugar wala Yanga.
Ni wazi tungesikia matusi na kejeli nyingi dhidi ya vigogo hawa. Kama namuona msemaji wa timu hiyo, kitu ambacho angekuwa anazungumza kama vipindi vya michezo vya redio mbalimbali usiku. Kama namuona kocha wao angekuwa anazungumza na kila mwandishi.
Hata hivyo, Leicester wanadhihirisha uzungu wao na tabia yao ya weledi mkubwa katika maisha yao ya kila siku. Claudio Ranieri anaongoza katika kufanya mahojiano ya kiungwana ambapo bado anawapa heshima kubwa vigogo wa soka England.
“Sitaki kufikiria kama tutatwaa ubingwa. Mawazo yangu yapo katika mechi inayofuata dhidi ya Arsenal. Itakuwa mechi ngumu yenye wachezaji wazuri. Hata hivyo, bado tunataka kupigana. Tunajua ni Ligi ya ajabu lakini tutajaribu. Hata hivyo, kuna timu kubwa ambazo zinaweza kuchukua ubingwa huu,” hii ilikuwa kauli ya Ranieri nusu saa tu baada ya kuifunga Manchester City mabao 3-1 ugenini.
Hapa unamzungumzia kocha ambaye kabla hajaichapa City alikuwa ameichapa Liverpool mabao 2-0 ya uhakika akiwa nyumbani. Na ushindi huu dhidi ya City ulikuwa wa uhakika zaidi huku wakimaliza mechi katika ubora wao.
Kama ingekuwa kocha wa mzawa aliyetoka kuichapa Simba au Yanga mabao 3-1 Uwanja wa Taifa, huku akiongoza kwa tofauti ya pointi sita, tungesikia kelele nyingi za matusi zilizojaa kejeli na kashfa huku heshima ikiwekwa kando.
“ Simba na Yanga ndio nini? Mimi nakwambia hawa huwa wanabebwa tu na ndio maana wanashinda mechi zao. Wanapoteza pesa bure kununua wachezaji wa bei ghali wakati mitaani wachezaji wapo kibao,” hizo ndio zingekuwa kauli za kocha mzawa, dunia tofauti kabisa na ile ya Ranieri.
Iliwahi kutokea msimu uliopita wakati Mtibwa Sugar ikiongoza Ligi Kuu mwanzoni mwa msimu. Rafiki yangu Mecky Mexime baada ya kuichapa Yanga pale Morogoro alitoa maneno mengi ya kashfa dhidi ya wakocha Wazungu.
“Hata sisi tunaweza. Mimi nashangaa wanapoteza pesa bure tu kwenda kuchukua makocha wa kizungu kwa bei mbaya wananuanua wachezaji kwa bei mbaya,” alisikika Mecky. Msimu ulipomalizika Yanga ilikuwa bingwa na kocha wao Mzungu, Azam ilishika nafasi ya pili na kocha wao Mzungu, Simba ilishika nafasi ya tatu kocha wao akiwa Mzungu.
Uliwasikia nahodha wa Coastal Union, Ally Ahmed ‘Shiboli’ na Kocha wake Ally Jangalu baada ya kuichapa Yanga Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wiki iliyopita? Je, umefuatilia matokeo yao kwa mechi mbili zilizofuata baada ya tambo na kejeli nyingi kwa vijana wa Jangwani? Ebu fuatilia uone tofauti ilivyo kwetu.
Achana na hayo ya makocha. Napenda kumsikiliza Riyad Mahrez ambaye ameiteka Ligi Kuu ya England kwa sasa na kuna uwezekano mkubwa akachaguliwa kuwa mchezaji bora wa msimu mwishoni mwa msimu huu.
Kila nikisikiliza mahojiano yake, Mahrez anaishia kuwasifu wachezaji wenzake na jinsi ambavyo wanajitahidi kupambana na timu kubwa. “Tunacheza kadiri tunavyoweza kufanikisha hili. Sio suala la mchezaji mmoja mmoja bali, ni juhudi ya timu nzima. Tumekuwa tukizingatia sana mazoezi na mechi kila siku.”
Hii ndio kauli ya mchezaji staa wa timu. mchezaji ambaye anaimbwa na vyombo vyote vya habari duniani. Inatia kinyaa kusikiliza mahojiano ya mchezaji mmoja aliyeng’ara kwa wiki mbili tu, huku akizifunga Simba na Yanga.
“Siri ya uwezo wangu ni mazoezi na kujituma. Ticha akiendelea kunipa nafasi mimi nitaendelea tu kutamba kwa sababu najua mabeki wengi hawaniwezi, sema basi tu utakuta sisi wachezaji wa mikoani tunadharauliwa,” anasema mchezaji huyo huku akiwa amesahau kuwashukuru wachezaji wenzake. Soka sio mchezo wa mtu mmoja mmoja. Soka sio tenisi. Ni mchezo wa timu. Unawasahau vipi wenzako?