Kwa rekodi hizi ngoma bado mbichi CAF
Muktasari:
- Miamba ya Tanzania, Simba SC, TP Mazembe ya DR Congo, Pyramids FC ya Misri, Al Hilal ya Sudan na Atletico Petroleos ya Angola ni miongoni mwa vigogo waliojiweka katika nafasi nzuri baada ya kupata ushindi katika mechi za ugenini.
MASHINDANO ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2026/27 yanaingia katika hatua muhimu wiki hii, huku mechi za marudiano za raundi ya kwanza ya awali zikitarajiwa kuamua timu zitakazofuzu hatua inayofuata.
Miamba ya Tanzania, Simba SC, TP Mazembe ya DR Congo, Pyramids FC ya Misri, Al Hilal ya Sudan na Atletico Petroleos ya Angola ni miongoni mwa vigogo waliojiweka katika nafasi nzuri baada ya kupata ushindi katika mechi za ugenini.
Matokeo yakionyesha jinsi tofauti ndogo zinavyoweza kuamua hatima ya timu katika raundi za awali.
Katika mechi 28 za kwanza zilizochezwa Ijumaa hadi Jumapili, jumla ya mabao 43 yalifungwa, huku timu za nyumbani zikishinda mara 11, za ugenini mara saba na michezo 10 kumalizika kwa sare.
Mechi za marudiano zitachezwa kati ya Septemba 11 na 13, huku timu nyingi zikiwa bado na nafasi ya kusonga mbele.
TIMU SABA ZASHINDA UGENINI
Kushinda ugenini katika mashindano ya klabu Afrika si jambo rahisi, lakini timu saba zilifanikiwa kufanya hivyo katika mechi za kwanza.
Zamalek ya Misri ilikuwa ya kwanza baada ya kuifunga AS Port mabao 2-1 nchini Djibouti, kabla ya Al Hilal Omdurman na Teungueth FC nazo kupata ushindi wa ugenini Jumamosi.
Jumapili kulikuwa na ushindi mwingine minne wa ugenini, ambapo Pyramids FC iliifunga Gor Mahia mabao 2-0, huku Petro Atlético, Simba SC na TP Mazembe zote zikishinda kwa bao 1-0 dhidi ya UD Songo, Mighty Wanderers na Medeama.
Hivyo, timu za ugenini zilishinda asilimia 25 ya mechi 28 zilizokamilika. Zaidi ya hapo, ushindi sita kati ya saba wa ugenini ulipatikana bila kuruhusu bao, huku Zamalek ikiwa ndiyo timu pekee iliyoshinda ugenini lakini ikaruhusu bao.
UKAME WA MABAO
Mechi 20 kati ya 28, sawa na zaidi ya asilimia 71, zilishuhudia angalau timu moja ikimaliza mchezo bila kufungwa.
Kwa jumla, kulikuwa na jumla ya ‘clean sheet’ 25 zilizopatikana na timu mbalimbali katika mechi hizo.
Michezo mitano ilimalizika kwa sare ya bila mabao, ikiwemo La Cure Waves dhidi ya Orlando Pirates, ASN Nigelec dhidi ya MC Alger na Colombe Sportive dhidi ya Stade Malien.
Michezo mingine iliyomalizika bila bao ni Aiglons dhidi ya Sidaama Buna na Star Sport Academy dhidi ya Medina United.
Ni mechi nane pekee kati ya 28 zilizoshuhudia timu zote mbili zikifunga.
USHINDANI MWEMBAMBA
Mechi 11 kati ya 28, sawa na asilimia 39, zilimalizika kwa ushindi wa bao 1-0.
Asswehly, JS Saoura, El Merriekh Bentiu, Al Merreikh, Club Africain, Aigles du Congo na Scottland zilishinda kwa bao 1-0 nyumbani, wakati Teungueth, Petro Atlético, Simba na TP Mazembe zilipata ushindi huo ugenini.
Ukijumuisha pia sare tano za bila mabao, zaidi ya nusu ya mechi za mwisho wa wiki, yaani 16 kati ya 28, zilikuwa na bao moja au chini.
VIGOGO WAKWAMA
Baadhi ya matokeo yaliyovutia zaidi mwishoni mwa wiki hayakuwa ushindi, bali ni namna baadhi ya timu zilizotajwa kuwa vigogo zilivyoshindwa kupata matokeo mazuri.
La Cure Waves, iliyokuwa ikicheza Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza, iliilazimisha Orlando Pirates ya Afrika Kusini sare ya bila mabao nchini Mauritius.
Matokeo hayo yameipa La Cure Waves matumaini kabla ya mchezo wa marudiano nchini Afrika Kusini, ingawa kazi itakuwa ngumu zaidi.
Gaborone United ya Botswana nayo ilikaribia kupata ushindi dhidi ya Yanga ya Tanzania baada ya Ambrosius Amseb kuifungia timu hiyo bao dakika ya 32.
Hata hivyo, Selemani Mwalimu aliinusuru Yanga kwa kusawazisha dakika ya sita ya muda wa nyongeza.
ASN Nigelec ya Niger pia iliishikilia MC Alger ya Algeria kwa sare ya bila mabao mjini Niamey, ikionyesha kuwa ukubwa wa jina la klabu hauwezi kuamua matokeo wakati raundi za awali zinapoanza.
TIMU MBILI ZAFUNGA MABAO MANNE
Timu mbili zilifunga mabao manne katika mechi zao za kwanza na kujipa faida kubwa kuelekea marudiano.
Wiliete ya Angola ilipata ushindi mkubwa zaidi baada ya kuichapa Foresters ya Shelisheli mabao 4-0.
Maghreb Fes ya Morocco nayo ilifanya vizuri kwa kuifunga Rahimo ya Burkina Faso mabao 4-1 nyumbani.
Katika ushindi huo, Maghreb Fès ilipata mabao kutoka kwa wachezaji wanne tofauti, Adam Brika, Soulaïman Allouch, Titus na Christopher Ibayi.