Kuna zaidi ya kufanya AFCON 2027, mliopewa dhamana fanyeni kweli
Muktasari:
- Kwake Waziri wa Michezo ni muhimu akakaa eneo hilo kwa muda mrefu ili maandalizi yamkae kichwani na aelewe kwa mapana na marefu kila kinachoendelea. Lakini akazungumzia Mkurugenzi wa Michezo na wengine ambao ni watendaji wa serikali katika eneo hilo.
KUNA wakati nilikuwa nazungumza na mdau mmoja wa soka kuhusu maandalizi ya fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) za mwaka 2024 na zile za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027. Kwa maoni yake alisema tuombe kusitokee mabadiliko ya viongozi wa michezo wa kiserikali.
Kwake Waziri wa Michezo ni muhimu akakaa eneo hilo kwa muda mrefu ili maandalizi yamkae kichwani na aelewe kwa mapana na marefu kila kinachoendelea. Lakini akazungumzia Mkurugenzi wa Michezo na wengine ambao ni watendaji wa serikali katika eneo hilo.
Alisema hao ndio walipata nafasi ya kwenda kuangalia fainali zilizofanyika Cameroon kupata picha halisi ya nini cha kufanya kama mwenyeji na nini cha kukiacha.
Uzoefu huo wa AFCON ungesaidia kuandaa vizuri CHAN na AFCON ya 2027 fainali ambazo tunaandaa pamoja na Kenya na Uganda kama ilivyokuwa kwa CHAN 2024 japo zilichezwa mwaka huu.
Tangu wakati huo walishabadilika mawaziri na watendaji wakuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, yaani alikuwepo Innocent Bashungwa, Damas Ndumbaro na sasa Palamagamba Kabudi.
Nilipokumbuka hayo nikawa na wasiwasi zaidi kwamba Uchaguzi Mkuu wa 2025 unaweza kuja na waziri mpya na hivyo wasiwasi wa yule mdau ukatimia.
Lakini ni bahati kwamba Kabudi amerejea tena katika kiti hicho kuendeleza kile alichokifanya katika maandalizi na wakati wa CHAN iliyopita, ambayo wenyewe Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) walisema fainali hizo zilikuwa na mafanikio makubwa kuliko nyingi zilizopita.
Kuna makosa mengi tuliyaona wakati wa CHAN 2024, hasa mahudhurio ya mashabiki viwanjani tofauti na wenzetu wa Uganda na Kenya, ambako walilazimika kushauri mashabiki waende kuangalia mechi hizo kwenye runinga zilizosimikwa katika maeneo ya mashabiki (fans park) kutokana na viwanja kujaa kupitiliza, hadi mashabiki kuvamia mageti na kuvunja.
Tunajua suala hili litatiliwa maanani wakati wa AFCON 2027 ambazo kwa hapa pia zitafanyika mkoani Arusha ambako kunajengwa uwanja mpya rasmi kwa ajili ya mashindano hayo makubwa kuliko yote ya soka barani Afrika.
Hakuna dawa nyingine kubwa ya kukosekana kwa mashabiki viwanjani zaidi ya kuwakikishia usalama na kuwajengea mazingira ambayo yatawafanya wawepo uwanjani kwa muda mrefu badala ya hii ya kukimbizana barabarani na kubanana milangoni wakati muda wa kuanza mechi umekaribia.
Sehemu zote duniani mashabiki wanaweza kufika mapema viwanjani kwa kuwa wanajua kuna maeneo wanaweza kukaa na wengine kubadilishana mawazo huku wakila na kunywa na wanakuwa ndani ya uzio wa uwanja wakiwa wameshahakikiwa tiketi zao. Huingia ndani kabisa ya uwanja kukaa dakika chache kabla ya mchezo kuanza.
Wale wa kada ya juu, huwa na uhakika wa kufanya vikao vyao ndani ya jengo la uwanja, ambako kwa kawaida huwa na huduma za hoteli za kuanzia nyota tatu hadi tano. Uwanja wa Benjamin Mkapa una maeneo mengi ambayo watu wanaweza kukutana kabla ya mechi kufanya vikao vyao na kwenda kwenye viti mechi inapokaribia kuanza.
Lakini ni maeneo machache ambayo hufunguliwa kiasi kwamba asilimia kubwa ya jengo hilo inakuwa haitumiki kama ilivyokusudiwa.
Kwa mantiki hiyo ni nadra sana kumshawishi mtu aende uwanjani kwa ajili ya dakika tisini tu halafu aanze purukushani za kutoka uwanjani, foleni barabarani na kero nyingine nyingi.
Usafiri wa umma pia ni muhimu sana kuwezesha mashabiki kusafiri kwa uhakika na kupunguza idadi ya magari yanayoelekea uwanjani hapo, ambayo husababisha waandaaji kuegesha lori kubwa Chuo cha Elimu Chang’ombe kuzuia magari yasiyo na kibali kukaribia eneo la uwanja.
Kitu kizuri ni kwamba angalau miundombinu ya mabasi yaendayo kasi imeshafika Chuo cha Elimu na mingine kurasini na ni matumaini kwamba hadi wakati huo huduma za mwendokasi zitakuwa zimeshaanza na hivyo kuwahakikishia mashabiki usafiri wa uhakika kwenda uwanjani na kurudi.
Kuzunguka na spika za kuuzia laini za simu ili kushawishi mashabiki kwenda uwanjani ni kushusha thamani ya mashindano na mchezo wenyewe. Watu hawaendi kwa wingi viwanjani si kwa sababu hawajashawishiwa au hawajahamasishwa, bali kwa sababu wanaona mambo mengi hayako sawa.
Kwa hiyo, tuna imani kwamba Mheshimiwa Kabudi atakuwa ameyaona na kuyaorodhesha mapungufu yote ya CHAN 2024 ili AFCON ya 2027 iwe bora zaidi si machoni pa viongozi wa CAF pekee, bali wapenda michezo kwa ujumla.
Na hayo yafanyike bila kusahau malengo mengine ya kukubali kuaandaa fainali hizo, hasa yale ya kiuchumi na kijamii. Bado hatujaona ripoti ya jinsi tulivyofanya CHAN 2024, kiuchumi, kijamii na kimichezo. Ni matumaini yetu kuwa baada ya AFCON 2027 tutakuwa na ripoti nzuri inayoeleza ni kwa kiasi gani malengo hayo yote yamefanikiwa na hivyo kuwa na hamu ya kuandaa mashindano mengine makubwa.
Karibu tena Mheshimiwa Kabudi katika sekta ya michezo. Tuna imani na umahiri wako katika maeneo mbalimbali na Rais Samia Suluhu hajakubakiza Wizara ya Michezo kwa bahati mbaya, bali kwa kujua kuwa utaweza kuibeba michezo vizuri mabegani mwako na hasa AFCON 2027.