Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Saa 552 za moto Ligi Kuu Bara

LIGI KUU Pict

Muktasari:

  • Hii inaonekana kuwa ligi ngumu kwa timu zote kutokana na muda mchache wa maandalizi ambapo tangu leo zimebaki siku 23 tu ili ligi hiyo ianze na hivyo kila timu inahaha kuhakikisha kuwa inaweka mambo yake sawa.

IKIWA zimesalia siku 23, sawa na saa 552, kabla ya pazia la Ligi Kuu ya NBC 2026/27 kufunguliwa rasmi kwa mchezo wa ngao ya jamii, Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) imetangaza ratiba ya msimu huku vigogo Simba, Yanga na Azam FC wakikabiliwa na kazi ya kufanya katika mechi 10 za kwanza.

Hii inaonekana kuwa ligi ngumu kwa timu zote kutokana na muda mchache wa maandalizi ambapo tangu leo zimebaki siku 23 tu ili ligi hiyo ianze na hivyo kila timu inahaha kuhakikisha kuwa inaweka mambo yake sawa.

Kuna timu zitaanza maandalizi sasa na nyingine zilishaanza lakini yote ni kuhakikisha kuwa zinajiweka sawa kwa ajili ya ligi hiyo ambayo itakuwa na timu mbili mpya, Kagera Sugar pamoja na Polisi Tanzania.

Ndani ya raundi hizo za mwanzo, baadhi ya timu zimeonekana kunufaika na idadi kubwa ya mechi za nyumbani huku nyingine zikianza msimu kwa safari nyingi za ugenini zinazoweza kuongeza gharama za uendeshaji, uchovu wa wachezaji na kuathiri maandalizi ya kiufundi.

Timu zinazotoka maeneo ya mbali kijiografia ndizo zinazoonekana kuwa na kibarua kizito. Mashujaa FC ya Kigoma ndiyo inayoongoza kwa kuwa na ratiba ngumu zaidi ya safari katika mechi 10 za kwanza, ikitarajiwa kusafiri mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Tanga na Mbeya.

LIGI 05

Kagera Sugar na Geita Gold nazo zinakabiliwa na changamoto kama hiyo kutokana na nafasi zao kijiografia. Mbali na safari ndefu, timu hizo pia zitakutana mapema na baadhi ya wapinzani wanaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa msimu huu.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa ratiba ya mechi 10 za kwanza, Mashujaa ndiyo timu itakayokata umbali mrefu zaidi wa safari wa zaidi ya kilomita 8,200, ikifuatiwa na Kagera Sugar yenye zaidi ya kilomita 7,900, huku Geita Gold ikitarajiwa kusafiri karibu kilomita 7,850.

Hata hivyo, si kila timu yenye safari nyingi ina ratiba ngumu kwa ujumla. Baadhi zimepata nafuu kwa kucheza mechi nyingi zaidi nyumbani. Namungo FC, kwa mfano, itanufaika na idadi kubwa ya mechi kwenye Uwanja wa Majaliwa, jambo linaloweza kuipa nafasi nzuri ya kukusanya pointi mapema.

LIGI 02

VIGOGO WAANZA NA MTIHANI

Kwa Simba, Yanga na Azam FC, changamoto haitakuwa safari pekee, bali pia mpangilio wa ratiba unaowakutanisha mapema na mechi zinazoweza kuathiri kasi yao ya mwanzo wa msimu.

Simba itaanza kampeni yake kwa mechi tatu mfululizo za ugenini dhidi ya Kagera Sugar, Pamba Jiji na Singida Black Stars kabla ya kurejea nyumbani kuwakaribisha Coastal Union na Geita Gold. Baadaye itasafiri tena kwenda Chamazi kuvaana na Azam FC kabla ya Kariakoo Derby dhidi ya Yanga.

Yanga nayo itaanza kwa safari ya Lindi kuivaa Namungo FC kabla ya kucheza mechi tatu za nyumbani mfululizo dhidi ya Coastal Union, JKT Tanzania na Pamba Jiji. Kisha itasafiri kwenda kucheza na Fountain Gate kabla ya kuikaribisha Geita Gold na baadaye kuifuata Simba katika Kariakoo Derby.

Kwa Azam FC, mwanzo wa msimu nao si mwepesi. Baada ya kuanza ugenini dhidi ya Polisi Tanzania, itacheza na TRA United na Pamba Jiji nyumbani kabla ya safari mbili mfululizo za Geita na Bukoba kuvaana na Geita Gold na Kagera Sugar. Baadaye itakuwa mwenyeji wa Simba katika moja ya mechi kubwa za mwanzo wa msimu.

LIGI 03

MICHEZO MIKUBWA YA MAPEMA

Ratiba ya mechi 10 za kwanza tayari imepanga michezo kadhaa mikubwa inayotarajiwa kuongeza ushindani mapema msimu huu.

Mchezo wa kwanza mkubwa utakuwa Septemba 9, ambapo Azam FC itakuwa mwenyeji wa Simba SC kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Baada ya hapo, Oktoba 8, Pamba Jiji itavaana na Geita Gold kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza katika mchezo wa heshima ya Kanda ya Ziwa.

Siku inayofuata, Oktoba 9, Dodoma Jiji itawakabili Singida Black Stars kwenye Uwanja wa Jamhuri katika mchezo wa ushindani wa Kanda ya Kati.

Macho yote yataelekezwa Oktoba 10 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, ambapo Simba na Yanga zitakutana katika Kariakoo Derby ya kwanza ya msimu.

LIGI 01

MZIGO WA MWANZO

Kwa ujumla, mechi 10 za kwanza zinaweza kuwa na mchango mkubwa katika mwelekeo wa msimu. Timu zitakazoweza kuvuka kipindi hicho kwa mafanikio zitajijengea nafasi nzuri kwenye msimamo na kujiweka mapema katika mbio za ubingwa.

Kwa vigogo kama Simba, Yanga na Azam FC, presha ya kuanza vizuri itakuwa kubwa, huku timu nyingine zikitafuta kutumia ratiba hiyo kujikusanyia pointi muhimu dhidi ya wapinzani wao. Katika msimu ambao ushindani unatarajiwa kuwa mkali zaidi, uwezo wa kusimamia ratiba, kufanya safari bila kupoteza kasi na kutumia vizuri mechi za nyumbani unaweza kuwa miongoni mwa mambo yatakayobeba uzito mkubwa katika mbio za ubingwa wa NBC 2026/27.

LIGI 04

BODI YA LIGI

Ratiba hiyo ilizinduliwa jana jijini Dar es Salaam kwa mara ya kwanza kupitia mfumo wa kidijitali uliotumika kupanga mechi zote 240 za msimu mbele ya viongozi wa soka, wadhamini, makocha, waandishi wa habari na wadau mbalimbali.

Mtendaji Mkuu wa TPLB, Cornel Barnabas, alisema matumizi ya mfumo huo ni sehemu ya mkakati wa kuifanya Ligi Kuu ya NBC iendane na teknolojia zinazotumika katika ligi kubwa duniani.

“Malengo yetu ni kuendelea kuboresha ligi yetu ili iwe na ubora na mifumo ya kisasa inayokwenda sambamba na mabadiliko ya ulimwengu wa sasa,” alisema Barnabas.

Aliongeza kuwa ratiba imetolewa mapema ili kutoa muda wa kutosha kwa maandalizi ya klabu na pia kuendana na kalenda ya maandalizi ya AFCON 2027, ambayo Tanzania itakuwa mmoja wa wenyeji.

Msimu wa 2026/27 utakuwa na jumla ya mechi 240 zikizikutanisha timu 16 ambazo ni Simba, Yanga, Azam FC, Namungo, Mbeya City, Geita Gold, Pamba Jiji, Kagera Sugar, Singida Black Stars, Dodoma Jiji, Coastal Union, Polisi Tanzania, Fountain Gate, Mashujaa FC, JKT Tanzania na TRA United.