Kinachowakwamisha mabondia kimataifa
Muktasari:
- Katika michezo hiyo, ngumi za kulipwa nchini Tanzania nazo zinaendelea kushuhudia kukua kwa vipaji vinavyofanya vizuri ndani na hata nje ya mipaka ya nchi.
KWENYE ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazozidi kupiga hatua katika michezo mbalimbali, hususani soka.
Katika michezo hiyo, ngumi za kulipwa nchini Tanzania nazo zinaendelea kushuhudia kukua kwa vipaji vinavyofanya vizuri ndani na hata nje ya mipaka ya nchi.
Lakini nyuma ya maendeleo hayo kuna changamoto zinazowakabili baadhi ya mabondia wa Kitanzania wanapokwenda kupigana nje. Visa vya kutokutendewa haki, mikataba yenye masharti yasiyoeleweka na changamoto za kisaikolojia katika nchi za kigeni vimekuwa sehemu ya kilio kinachoweza kuvuruga ndoto za vijana wanaotafuta mafanikio kupitia mchezo huo.
Mwanaspoti inakuchambulia baadhi ya changamoto zinazowakwamisha mabondia wanapokwenda kupigana nje ya nchi, ikiwemo ukosefu wa elimu ya mikataba, usimamizi dhaifu, maandalizi yasiyotosheleza na kutofahamu mifumo ya ngumi katika nchi wanazoenda.
SHIDA IPO HAPA
Changamoto ya bondia anapokwenda kupigana kimataifa haianzi siku anayopanda ulingoni, bali kwenye maandalizi ya safari yenyewe. Bondia anaweza kuwa na uwezo mkubwa wa kupigana, lakini kama hana meneja anayejua taratibu za kimataifa, mkataba uliopitiwa na mtaalamu na mtu wa kusimamia maslahi yake akiwa ugenini, anakuwa katika mazingira magumu.
Tatizo lingine ni elimu ndogo kuhusu mikataba. Baadhi ya mabondia huangalia zaidi fedha ya pambano bila kuangalia vipengele vingine vinavyoweza kuamua mustakabali wa safari yao. Ni muhimu kujua nani analipia usafiri, malazi na chakula, muda wa kufika nchini, masharti ya uzito, vipimo vya afya, malipo ya pambano na nini kinatokea endapo pambano litabadilishwa au kusitishwa.
Hapo ndipo umuhimu wa meneja, promota na mwanasheria wenye uzoefu wa ngumi za kimataifa unapohitajika. Bondia anapokuwa na timu inayojua taratibu za nchi anayoenda, anakuwa na nafasi kubwa ya kuelewa haki na wajibu wake kabla ya kukubali pambano bila maandalizi hayo, bondia anaweza kujikuta akitumia nguvu nyingi kupambana na mambo yaliyo nje ya ulingo.
Pia kuna suala la maandalizi ya kimwili na kisaikolojia. Kupigana ugenini kunahitaji bondia kujiandaa na mazingira tofauti ya mazoezi, chakula, hali ya hewa, usafiri na presha ya mashabiki wa nyumbani. Mabadiliko yasiyotarajiwa katika ratiba yanaweza kuongeza presha, hasa kama bondia hana mtu wa karibu wa kumshauri na kusimamia masuala hayo.
Nyingine ni changamoto ya kutofahamu mifumo ya ngumi ya nchi mwenyeji ambayo imekuwa ikiwatesa mabondia wengi nchini. Taratibu za usajili, leseni, vipimo vya afya, uzito na mambo mengine ya pambano vinaweza kutofautiana kutoka nchi moja kwenda nyingine. Bondia ambaye hajajiandaa na mambo hayo anaweza kuchelewa, kuvurugwa au kukabiliwa na mazingira ambayo hakuyatarajia.
Kwa hiyo, kama Tanzania inataka mabondia wake waepuke changamoto hiyo, haitoshi kuwazalisha mabondia wenye vipaji tu. Inahitaji pia kujenga mfumo unaowaandaa kwa mapambano ya kimataifa; kuanzia elimu ya mikataba, usimamizi, maandalizi ya safari, taratibu za kimataifa hadi ulinzi wa haki zao.
WASIKIE HAWA
Akisimulia mkasa aliowahi kukutana nao bondia Jesca Mfinanga nchini Afrika Kusini anasema hakukuwa na utaratibu mzuri kuanzia kwenye maandalizi hadi wakati wa kupanda ulingoni.
“Kusema ukweli tuliyopitia kule Sauzi yanasikitisha sana. Unafika ugenini unakuta mazingira ni tofauti kabisa na kile mlichokubaliana kwenye mkataba. Chakula unachopewa, mazingira ya mazoezi na hata ratiba ya kupima uzito inabadilishwa ghafla ili tu kukuvuruga kisaikolojia. Wanajua huna mwakilishi au mwanasheria wa kukupigania, kwa hiyo wanatumia fursa hiyo kukukandamiza ili bondia wao wa nyumbani ashinde.”
Bondia Fadhili Majiha maarufu zaidi kama Kiepe Nyani anasema kila nchi ina taratibu zake na vitu kama hivyo vinatokea mara nyingi kwenye nchi za ugenini.
“Mfano Indonesia nilipowahi kucheza Heri Amol mwaka 2016 unajua walikuwa na desturi ya kukupa pambano pamoja na malipo ambayo unatakiwa kulipwa na mtu anajikuta anapanda ndege halafu hajui chochote ambacho kinafanyika kwenye ndege.
“Sasa ikawa ile ukinywa chai au kahawa na chochote utakachokula ndiyo mtu utasikia anakwambia unaona vile ambavyo umekula kwenye ndege, nimekulipia vyote hivyo nakata kwenye pesa yako na wewe hauna unachokijua unaona sawa,” anasema Majiha.
Bondia mwingine anayepigana ngumi za kulipwa nchini, Egine Kayange, anaeleza kuwa funzo alilolipata akiwa Afrika Kusini limemfungua kuhusu udhaifu wa usimamizi wa mabondia pindi wanapokuwa ugenini.
“Ilinifundisha somo kubwa sana. Nimejifunza kwamba katika nchi za nje au michezo ya kimataifa, huwezi kumwamini kila mtu. Lazima uhakikishe mikataba yako imenyooka kabisa,” anasema.€
MSIKIE KASEBA
Mwenyekiti wa Chama cha Mabondia wa Kulipwa Nchini (TPBA), Japhet Kaseba, anasema changamoto hizo zimeanza kupungua, lakini bado elimu kwa mabondia kuhusu haki zao na namna ya kujilinda wanapokwenda kupigana nje ni jambo linalohitaji kupewa kipaumbele.
“Shida ziko nyingi, ingawa sasa hivi zimeanza kupungua. Sisi wadau na taasisi tunatakiwa kuhakikisha mabondia wanapata uelewa kwa sababu bado hawana uelewa mkubwa wa kutosha ili waweze kujitetea na kulinda haki zao,” anasema Kaseba.na kuongeza:
“Wanashindwa kujichanganua wenyewe, sasa watu wachache wanawavunja nguvu, wanakata tamaa na kuona ngumi ni ngumi, mwisho wanaacha.”