Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Shemeji’ yetu Aziz Ki na Yanga wanalazimika kupendana

JICHO Pict


AZIZ Ki aende wapi? Morocco anaweza kutembea na baunsa? Haiwezekani. Libya anaweza kutembea na baunsa? Haiwezekani. Libya anaweza kuimbwaimbwa kama hapa Tanzania? Haiwezekani.


Nilimuona Aziz juzi jukwaani akiwa na tajiri wa Yanga, Ghalib Said Mohamed pamoja na Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said. Ilikuwa lazima tukio hilo lilete uvumi wa Aziz kurudi Yanga hasa ukizingatia kwamba katika siku za karibuni amekuwa akihusishwa kurudi Yanga.


Wale jamaa wawili Ghalib na Hersi ndio walipambana wakati ule kumtoa Aziz ASEC Mimosas na kumletea mitaa ya Twiga na Jangwani. Baadae walimlea kama mtoto wao wa nyumbani na kama ilivyo kawaida kwa wachezaji wengi wa Yanga baadae huwa wanatengenezewa DNA ya klabu hiyo. Aziz ni miongoni mwao. Siku hizi amekaa Kiyangayanga zaidi kuliko zamani.

AZIZ Pict

Kikwazo kinaweza kuwa pesa tu endapo Waarabu wa Libya watataka kumuuza Aziz. Hata wakitaka kumuuza kwa dola laki tatu tu kwetu ni nyingi na kwao ni kidogo. Bado pesa yetu ya madafu inasuasua. Bado pia utajiri wa Waarabu unatusumbua katika mpira.

Wao wakimtaka mchezaji wetu kwa dola laki tatu ni kiasi kikubwa kwetu. Tunaichukua haraka. Sisi tukimtaka mchezaji wao na wakataka dola laki tatu ni kiasi kikubwa kwetu. Tunaanza kutafutana.

Kwa Aziz nahisi labda tatizo liwe pesa tu. Vinginevyo yeye na Yanga wanatamaniana. Tuanze upande upi? Nadhani ni wa Aziz mwenyewe. Wakati ule anaondoka akielekea Wydad nilijua wazi kwamba mpira wa waarabu ungekuwa mgumu kwa Aziz.

AZIZ KI Pict

Hatuhitaji kurudiarudia namna ambavyo wachezaji wa ligi yetu wamekuwa na wakati mgumu wakienda kucheza mpira wa Waarabu. Huku kwetu tunacheza na timu nyingi dhaifu lakini kule ni vita kuanzia mazoezini hadi katika mechi. Inabidi uwe na nidhamu ya Simon Msuva.

Nje ya uwanja maisha pia ni magumu kama uliwahi kupita nchi inayoitwa Tanzania kisha ukaenda Morocco. Niliwahi kumtembelea Simon Msuva wakati anacheza Morocco na niliona namna ambavyo maisha hayakuwa rahisi baada ya mazoezi na mechi.

Inabidi uwe makini tu na kitu kilichokupeleka. Vinginevyo muda wote unakaa ndani tu. Hawa wachezaji wetu wakubwa nje wamekuwa wakijirusha katika sehemu za starehe kadri wanavyojisikia. Wakati mwingine na starehe zao zinalipiwa na mashabiki.

KI Aziz Pict

Ukitoka Tanzania kwenda kucheza Morocco maisha yanakuwa magumu ndani na nje ya uwanja. Sikumuona Aziz kama atadumu sana kule kwa Waarabu. Uvumi wa kwamba anataka kurudi Yanga nauelewa kwa asilimia zote.

Hata kama hawezi kurudi Yanga lakini ukimwambia Aziz arudi hata Simba au Azam atakubali tu ili mradi awe nchini. Apate amani ya moyo. Kwanza ni shemeji yetu. Amemuoa dada yetu wa Kitanzania.

Kwa upande wa Yanga? Juzi Aziz alikuwa akiitazama Yanga wakikaribia kuchukua ubingwa wao mwingine wa ligi kuu. Tangu yeye awasili nchini Yanga wamekuwa wakitawala mpira wetu. Na tangu yeye aondoke Yanga pia wameendelea kutawala mpira wetu.

Tatizo lililojitokeza ni kuna Wanayanga, wachambuzi na washikadau wengine wanaamini Yanga ya Aziz na Yanga hii vina utofauti kidogo. Kwamba kwa namna moja au nyingine Yanga wameshuka hata kama kesho watachukua ubingwa pale kwa Meja Isamuhyo.

AZIZ KI Pict

Kuondoka kwa Aziz mwenyewe kulionekana kuwa tatizo. Kuondoka kwa Khalid Aucho kulipunguza umiliki wa mpira pale Katikati. Kuondoka kwa Fiston Mayele kulipunguza kitu. Kuumia kwa Clement Mzize kulipunguza kitu. Wachezaji wengi pia ambao wamesajiliwa katika madirisha ya karibuni hawakuleta kitu kikubwa.

Timu imeendelea kuwategemea akina Pacome Zouzoua ambaye wakati mwingine ameonekana kusuasua na kiwango chake sio kile cha Pacome ambaye tunamfahamu. Hapo ndipo inapoaminika kwa huenda Yanga wanamtamani shemeji yetu Aziz ili aendelee pale walipoishia.

Tatizo linaweza kuwa pesa lakini nataka niwaambie watu wa Yanga pamoja na klabu nyingine mbili kubwa nchini. Simba na Azam. Umefika wakati sasa wakaendelea kutanua goli. Sawa bajeti zao ni kubwa lakini inabidi ziwe kubwa zaidi.

AZIZ Pict
AZIZ Pict

Sio kwa Aziz tu, bali kwa wachezaji wengine ambao wanaonekana ni wa maana na wanaweza kuisaidia timu basi pesa ndefu itengwe ili walau tuwe katika nafasi nzuri ya kushindana na wakubwa wa kule Afrika Kaskazini pamoja na Mamelodi Sundowns.

Tunafurahia kuuza wachezaji wetu kwa bei mbaya lakini umefika muda pia tuanze kununua wachezaji kwa bei mbaya. Hakuna jinsi. Ili mradi mchezaji anaweza kuleta kitu kikubwa katika timu basi klabu hizi zijichimbe mfukoni na kutoa chochote.

Usajili ni kamari. Inaweza kulipa au isilipe lakini kila nikifikiria matumizi ya wenzetu wanaotoa dola milioni mbili kwa mchezaji mmoja kama Mamelodi nachelea kusema itatuchukua kupambana nao.

AZIZ Pict

Kuna wakati unajaribu kuwafikia na unadhani haupo mbali lakini ghafla wanaibuka tena na kukukumbusha pengo lililopo. Mfano mzuri ni Mamelodi iliyowadhulumu Yanga bao la Aziz Ki pale Pretoria jinsi ilivyokuwa tofauti na Mamelodi ya leo ambayo imetwaa ubingwa wa Afrika.

Walipoona akina Yanga wanawasogelea wakatia pesa tena. Kuanzia pale Mamelodi wamekwenda juu na nahisi Yanga wameshuka. Kuanzia lile pambano la Pretoria ambalo Aziz alinyimwa bao lake naona wazi kwamba Yanga haijawa ile tena wakati Mamelodi wamekwenda juu zaidi.

Labda ndio maana uvumi kama wa Aziz kurudi zake Yanga unakwenda juu kila kukicha. Tunaona kabisa wanatamaniana na wana sababu lukuki za kufanya hivyo. Tuache tuone itakavyoishia. Sisi yetu macho.