Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kagame Cup 2025 vita nyingine ya kombe inayoanza Dar

KAGAME Pict

Muktasari:

  • Michuano hiyo yenye historia ndefu ikiasisiwa 1967 kisha kusimama kwa muda hadi 1974 ilipokuja kwa kasi kubwa na kupigwa mfululizo, inaandaliwa na Baraza la Vyama vya Michezo vya Nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) itafikia tamati Septemba 15.

MSIMU wa 47 ya michuano ya Kombe la Kagame unaanza rasmi leo Jumanne ikihusisha klabu 12, zitakazoumana kwenye viwanja viwili vya Meja Jenerali Isamhuyo na KMC Complex vilivyopo jijini Dar es Salaam na kwa kuanza zinapigwa mechi mbili.

Michuano hiyo yenye historia ndefu ikiasisiwa 1967 kisha kusimama kwa muda hadi 1974 ilipokuja kwa kasi kubwa na kupigwa mfululizo, inaandaliwa na Baraza la Vyama vya Michezo vya Nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) itafikia tamati Septemba 15.

Kama ilivyokuwa msimu uliopita ilipofanyika pia jijini Dar es Salaam, wenyeji Simba na Yanga zimechomoa kushiriki kutokana na kubanwa na ratiba, lakini Singida Black Stars na KMC zimechukua nafasi katika michuano hiyo mikongwe barani Afrika.

Msimu uliopita Red Arrows ya Zambia ilibeba ubingwa wa michuano hiyo kwa kuifunga kwa penalti 11-10 APR ya Rwanda baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya 1-1, mabingwa hao wakishiriki kama timu alikwa, ambapo kwa msimu huu haishiriki.

Klabu 12 zilizopangwa katika makundi matatu yenye timu nne kila moja ni Singida BS, Garde-Coters (Djibouti), Coffee (Ethiopia) na Polisi FC (Kenya) zilizopangwa Kundi A, wakati Kundi B lina timu za KMC (Tanzania Bara), Mlandege (Zanzibar), APR (Rwanda) na Bumamuru ya Burundi.

Kundi C lina timu za Al Hilal ya Sudan, Mogadishu City (Somalia), Al Ahly Wad Madani (Sudan) na Kator FC ya Sudan Kusini.

KAGA 01

Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo ni kwamba mechi za makundi zitapigwa kuanzia leo Jumanne hadi Septemba 10 na timu tatu zitakazoongoza makundi hayo na mshindwa bora moja zitacheza nusu fainali katika mechi zitakazopigwa Septemba 12.

Washindi wa mechi hizo za nusu fainali zitaumana fainali itakayopigwa Septemba 15, ikitanguliwa na mechi ya kusaka mshindi wa tatu itakayopigwa pia mapema siku hiyo hiyo.


SIMBA BALAA

Licha ya kutoshiriki michuano ya pili mfululizo, Simba ndio wababe wa Kagame iliyopewa jina hilo baada ya Rais wa Rwanda, Paul Kagame kudhamini kuanzia mwaka 2002 akiweka kiasi cha Dola 60,000 (zaidi ya Sh 150 milioni), ikiwa imetwaa mataji mengi zaidi tangu 1974.

Simba imebeba mataji sita, la mwisho likiwa ni mwaka 2002, ikilingana na AFC Leopards ya Kenya, huku Yanga, Gor Mahia ya Kenya na Tusker Kenya zikifuatia nyuma zikiwa na mataji matano kila mmoja.

Katika michuano ya msimu huu, ni APR pekee ndio waliowahi kubeba ubingwa katika timu shiriki, ikiwa imetwaa mara tatu sawa na SC Villa ya Uganda na Al Merrikh ya Sudan, lakini ikiwa pia imefika fainali nyingine sita tofauti ikiwamo ya msimu uliopita ilipopoteza mbele ya Red Arrows.

KAGA 02

AZAM FC WAMO

Ukiondoa Simba na Yanga zilizobeba mara nyingi taji la michuano hiyo tangu 1974, lakini Azam FC nayo wamo ikiwa ndio timu ya mwisho ya Tanzania Bara kutwaa ubingwa ikifanya hivyo mwaka 2018. Azam pia ilitwaa ubingwa kwa mara ya kwanza 2015 michuano ikifanyikia Tanzania.

Timu hiyo iliweka rekodi tamu katika michuano ya Kagame kwa kucheza fainali tatu mfululizo kati ya nne ilizowahi kufika ikiwamo ya kwanza mwaka 2012 na kupoteza mbele ya Yanga kwa kulala mabao 2-0.

Katika fainali hizo tatu mfululizo Azam ilianza kwa kuvaana na Gor Mahia ya Kenya mwaka 2015 na kushinda kwa mabao 2-0, kisha ikarudia tena 2018 kwa kuifumua Simba kwa mabao 2-1 na 2019 ikacheza tena, lakini safairi hii ilikwama mbele ya KCCA ya Uganda iliyowanyoa  bao 1-0.

KAGA 04

SINGIDA, KMC KIBARUANI

Kutokana na rekodi hiyo ya Azam ni wazi Singida Black Stars, Mlandege na KMC zinazoiwakilisha Tanzania katika michuano ya msimu huu zina kazi ya kufanya mbele ya wapinzani wengine tisa wanaoshiriki fainali hizo za 47.

KMC inayojiandaa na Ligi Kuu Bara sambamba na Mlandege zimepangwa kundi moja la B, wakati Singida BS ipo Kundi A.

Mlandege na Singida BS zitaitumia michuano hiyo kwa ajili ya maandalizi ya mechi za kimataifa za CAF za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika itakayoanza siku chache baada ya kumalizika kwa Kombe la Kagame.

Mlandege ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) itashiriki Ligi ya Mabingwa ikianza kibarua dhidi ya AS Port ya Djibouti, wakati Singida itacheza Kombe la Shirikisho ikipangwa kuanza na Rayon Sports ya Rwanda.

Msimu uliopita Singida BS pia ilishiriki michuano hiyo sambamba na JKU ya Zanzibar na Coastal Union ya Tanzania Bara, lakini zote ziliambulia patupu.

KAGA 01

UDHAMINI MNONO

 Michuano ya  msimu huu imedhaminiwa na kampuni ya ubashiri ya Betika kwa dau la Dola 42 milioni za Kenya (zaidi ya Sh 814 za Kitanzania) sambamba na Times FM itakayotangaza redioni.