Julio hajakosea kutoa ahadi ngumu
Muktasari:
- Akiwa Mwadui FC aliwahi kuahidi kitu kama hicho lakini kwa kumbukumbu ambazo zipo hapa kijiweni, kocha huyo hakutimiza ahadi hiyo kwani aliendelea na kazi ya ukocha katika klabu tofauti na timu za taifa.
JAMHURI Kihwelo ‘Julio’ kwa mara nyingine ametoa ahadi moja ya kibabe ambayo aliwahi kuitoa miaka kadhaa hapo nyuma lakini hakuweza kuitimiza.
Ahadi hiyo ni ile ya kustaafu rasmi kazi ya ukocha ikiwa timu yake ya Mashujaa itakuwa miongoni mwa zitakazoshuka daraja katika Ligi Kuu msimu huu ambayo imefikia raundi ya 21.
Akiwa Mwadui FC aliwahi kuahidi kitu kama hicho lakini kwa kumbukumbu ambazo zipo hapa kijiweni, kocha huyo hakutimiza ahadi hiyo kwani aliendelea na kazi ya ukocha katika klabu tofauti na timu za taifa.
Jambo hilo ndilo limefanya kundi kubwa la watu hapa kwenye kijiwe lisiamini Julio atafanya hivyo iwapo litatokea kwani tayari alishawahi kuahidi siku za nyuma lakini hakutekeleza hivyo wanaona kama aliamua kufurahisha genge.
Hata hivyo kwa kinachoendelea kufanyika katika Ligi Kuu ya NBC, unaweza kubaini Julio hajakosea kutoa ahadi hiyo na huenda isitimie msimu huu kwa vile hakuna dalili zinazoweza kuashiria uwezekano wa Mashujaa FC kushuka daraja.
Timu nyingi zilizo chini yake katika msimamo wa ligi, hazionekani kama zinaweza kutengeneza presha kwa Mashujaa FC kwa vile kadri siku zinavyozidi kusonga mbele, zimekuwa zikizidi kuangusha pointi badala ya kuongeza.
Hakuna hata moja ambayo inaonyesha inaweza kupata ushindi angalau katika mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu ambazo zitaipatia pointi tisa zinazoweza kuifanya iikute, iisogelee au iipiku Mashujaa FC katika msimamo wa ligi.
Lakini kingine ambacho naamini kinampa jeuri Julio ni matokeo mazuri ambayo timu yake imekuwa ikiyapata katika Uwanja wake wa nyumbani wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Katika mechi nne ilizobakiza za ligi kucheza nyumbani, Mashujaa inaonekana inaweza kukusanya walau pointi sita ambazo zitazidi kuwaweka salama.